The House of Favourite Newspapers

MTOTO AFA AKIMUAGA MAMA YAKE!

DAR ES SALAAM: AMA kweli hakuna ajuaye saa ya kufa kwake; anayebisha aungane na Risasi Jumamosi katika tukio hili la kusikitisha lililoondoa uhai wa mtoto aitwaye Alvin Tillya wa Goba jijini Dar es Salaam.

 

Mashuhuda kutoka ndani ya familia wanasema mtoto Alvin siku ya mkasa hakuwa anaumwa, hakuonekana mwenye huzuni wala dalili zozote zilizoashiria kwamba angeweza kupoteza maisha siku hiyo kwa kuangukiwa na geti la nyumba yao.

 

HABARI KAMILI NI HII

Habari kutoka eneo la tukio zinasema, Jumapili ya Julai 29, mwaka huu, mama wa Alvin aliiambia familia yake kuwa anakusudia kutoka majira ya saa kumi jioni kuelekea kanisani.

Baada ya kukubaliana; wakati anatoka Alvin kama kawaida yake huwa anapenda kuwapokea wazazi wake wanaporudi na kuwaaga wanapotoka na kwamba wakati mama yake anaondoka, aliongozana naye ili wakaagane getini.

 

“Walitoka wote, yeye, mama yake na msichana wa kazi, walipofika getini Alvin aliagana kwa furaha kubwa na mama yake. “Mama yake alifurahi akawaambia warudi ndani wakaendelee na mambo mengine na kwamba yeye angerejea baadaye,” ndugu wa familia hiyo ambaye hakutaka kutaja jina kwa sababu si msemaji wa familia alisema.

 

KILICHOTOKEA BAADAYE

Inadhaniwa kwamba hata baada ya kuagana na mama yake, Alvin na dada yake hawakufanya haraka kufunga geti kutokana na mtoto huyo kuendelea kumsindikiza kwa macho mama yake kama mtu anayesema: “Mama hautaniona tena.”

 

WAFUNGA GETI

Baada ya dakika chache kupita Alvin aligeuka kurudi ndani na hapo muda wa kufunga geti ulipofika; inaelezwa jukumu hilo walishirikiana yeye na dada yake.

Huzuni; wakati watoto hao wanafunga, geti hilo lilitoka kwenye reli yake kwa sababu lina magurudumu na kulifanya lipoteze pia vishikizo vingine vya juu ambapo liliporomoka zimazima. Kila mtu aliomba heri kwamba geti hilo lingeanguka peke yake lakini haikuwa hivyo lilimwelekea Alvin na kumfunika mzimamzima huku likimpitia dada yake kwenye mkono na kumuachia maumivu makali.

 

TAHARUKI YATAWALA

Mara baada ya tukio hilo kilichofuata ilikuwa ni taharuki na kilio cha dada wa kazi, majirani na wanafamilia wengine waliokuwa ndani walitoka na kuambiwa mtoto alikuwa amefunikwa na geti hilo.

AKUTWA AMEFARIKI

Bila kuchelewa jitihada za kuliondoa zilifanyika lakini tayari lilikuwa limeshauacha mwili wa Alvin ukiwa unatoka damu puani. Wengi waliamini huenda angerudiwa na uhai lakini haikuwa hivyo kwani tayari mtoto huyo alikuwa amefariki dunia.

 

MAMA ASHANGAA KUAMBIWA HABARI ZA MSIBA

Ikumbukwe kuwa mara baada ya mama Alvin kuagana na mwanaye hakutazama nyuma aliendelea na safari zake mpaka alipopigiwa simu kuambiwa arudi nyumbani kuna matatizo. “Alitaka kujua matatizo gani yanayomrudisha nyumbani lakini tulimficha; aliporudi na kukuta mwanaye amefariki alitaharuki, kusema kweli ni msiba mzito ambao umemshtua kila mtu,” chanzo cha ndani kilisema.

 

BABA WA ALVIN ALIA KAMA MTOTO

Kufuatia kifo cha mwanaye baba wa marehemu aitwaye Gabriel Tillya alishindwa kujizuia, aliangua kilio kama mtoto kumuombolezea mtoto wake.

Hata pale Risasi Jumamosi lilipofika msibani nyumbani kwa Gabriel na kujaribu kuzungumza naye ilishindikana, hata mama wa mtoto naye hakuweza kumudu kuongea kutokana na machungu waliyokuwa nayo. Mwandishi wetu aliweza kushuhudia geti lililoondoa uhai wa Alvin na kubaini kwa macho ya kawaida kuwa liko katika uimara.

“Mimi ni jirani yao naishi pale (anaonesha nyumba yake kwa kidole) nimeshangazwa sana, we geti kama hili linaleta ajali kubwa namna hii, nimeogopa sana,” alisema jirani wa familia ambaye jina lake linahifadhiwa.

 

FUNDI MAGETI AZUNGUMZA

Baada ya kutokea kwa ajali hiyo ya geti iliyomuua Alvin, Risasi Jumamosi lilimtafuta fundi wa mageti ili kujua nini kinaweza kusababisha geti kuhama kwenye reli mpaka kuanguka.

“Kwanza mageti yako ya aina nyingi lakini kwa hilo la magurudumu chini linaweza kuanguka endapo litafungwa kwa nguvu kubwa itakayofanya litikisike na kuviondoa kwenye njia yake vigurudumu vingine vya juu vinavyolifanya litembee.

 

“Vigurudumu hivyo vikiondoka basi ni rahisi kuanguka na kuleta madhara, kwa hiyo inashauriwa kuyafanyia ukaguzi mageti ili kujua kama hakuna kutu iliyoshambulia vyuma na kuvifanya vikose uimara.

“Lakini ufungaji nao lazima uwe na kiasi lakini ukiwa ni ule wa kulibamiza kila siku unaweza kutanua njia za geti na kulifanya lipoteze uimara wake,” alisema Said Juma, fundi mageti eneo la Sinza Afrikasana, Dar.

 

ALVIN AZIKWA

Mwili wa Alvin ulisafirishwa hadi Moshi mkoani Kilimanjaro, ambako uliwekwa katika nyumba yake ya milele Julai 2 mwaka, huu nyumbani kwa familia ya Tillya eneo la Urunjari Kyaurinde.

Mungu aieweke roho ya marehemu mahali pema peponi – Amina!

Comments are closed.