The House of Favourite Newspapers

MWANAMKE ‘ALIYEKUFA’ AKUTWA AKIPUMUA MOCHWARI

MWANAMKE aliyekuwa ametangazwa na madaktari kuwa amekufa katika ajali ya barabarani karibu na Jiji la Johannesburg, Afrika Kusini, alikutwa na mfanyakazi wa mochwari akiwa hai baada ya kuuvuta mwili wake kutoka kwenye friji la kuhifadhia maiti na kugundua kwamba alikuwa anapumua.

 

Mwanamke huyo ambaye jina lake halikufahamika, alikuwa mmoja wa abiria waliotangazwa kuwa wamekufa baada ya gari moja kupinduka karibu na mji wa Carletonville, magharibi mwa Johannesburg. Kwa mujibu wa gazeti la The Sowetan, mfanyakazi huyo aligundua hilo wakati wa kujaza fomu za kumbukumbu za mochwari ambazo huwekwa sehemu maalum ndani ya mafriji ya kutunzia maiti.

Alipouvuta mwili wa mwanamke huyo, alimwona anapumua, jambo ambalo lilimwacha mfanyakazi huyo akiwa amepigwa bumbuazi na kusema: “Ilikuwa ni ajabu kufungua friji la maiti na kumkuta mtu akiwa hai ndani yake. Hebu fikiria nini kingetokea iwapo tungekuwa tumenza kumfanyia upasuaji wa kujua sababu ya kifo chake?”

 

Mwanamke huyo aliyekuwa amepata majeraha makubwa kichwani alipelekwa Hospitali ya Leratong karibu na mji wa Krugersdorp ambako anaendelea kutibiwa.

 

Hata hivyo, maofisa wa hospitali hiyo wamesema hapakuwa na uzembe wowote uliofanyika na kwamba zana za hospitali zilionyesha mwanamke huyo hakuwa na uhai wakati anafikishwa hapo, hivyo kuonekana baadaye akiwa na uhai ulikuwa ni “muujiza”. Pamoja na yote hayo, mamlaka ya afya ya wilaya ya Gauteng italifanyia uchunguzi tukio hilo.

JPM Azungumza na Viongozi Wastaafu, Lowassa, Mkapa, Sumaye Ndani

Comments are closed.