
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya Shilingi laki nane raia mmoja wa China, anayekabiliwa na shtaka la kutoa rushwa kiasi cha shilingi laki moja ili arejeshewe mashine yake ya kuchezeshea mchezo wa bahati nasibu.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo Theopista Sivoke, baada ya raia huyo wa China anayefahamika kwa jina la Sheng Bing Lin, kukiri kutenda kosa hilo kwa kumshawishi Afisa Mtendaji ampe rushwa ili amrudishie mashine yake.
Awali akitoa taarifa ya kukamatwa kwa raia huyo wa kigeni Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, Daudi Ndyamukama, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Sheng Bing Lin alifanikiwa kulipa faini hiyo na kubaki huru.
TAARIFA YA TAKUKURU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, imemkamata raia wa China Bwana SHENG BING LIN (40) kwa kosa la kushawishi na kutoa rushwa kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) ambapo ni kinyume na Kif cha 15 (1) (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Raia huyo wa China ambaye ni Msimamizi (Supervisor) wa kampuni wa JX BETTING alishawishi na kutoa rushwa ya shilingi 100,000/= kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa wa California-Nyegezi (jina limehifadhiwa) ili aweze kumrejeshea mashine yake ya kuchezeshea mchezo bahati nasibu.
Mchina huyo alishawishi na kutoa rushwa baada ya mashine yake ya kuchezeshea bahati nasibu (Betting) kukamatwa kwa kosa la kutokuwa na kibali, kuchezesha nje ya muda uliopangwa na serikali pamoja na kuwahusisha watoto chini ya umri wa miaka 18 katika mchezo huo.
Mashine hiyo ilikamatwa mwanzoni mwa mwezi Juni, 2020 katika maeneo ya Nyegezi Calfonia na kupelekwa katika kituo cha polisi Nyegezi. Hata hivyo, Mchina huyo alipokuwa akitakiwa kufika kituoni kutoa maelezo kuhusiana na kosa hilo hakuweza kutii amri hiyo badala yake alipiga simu na kumshawishi Afisa mtendaji ampe rushwa ili amrejeshee mashine yake.
Hapo ndipo mtego ulifanyika, mnamo tarehe 2 Juni 2020 Mchina huyo alikamatwa na Maafisa wa TAKUKURU katika maeneo ya Lakairo Hotel – Kirumba wakati anatoa rushwa ya shilingi laki moja kwa Afisa huyo wa serikali.
Bwana SHENG BING LIN (40) anafanya kazi hii ya kuchezesha mchezo huo wa bahati nasibu (Betting) katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini katika Mkoa Mwanza. Uchunguzi wa tuhuma hii umekamilika na leo tarehe 06 Juni, 2020 Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Aidha, tunampongeza mtumishi huyu mzalendo ambaye ametimiza wajibu wake wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, kwa kutoa taarifa na kufanikisha kukamatwa kwa mchina huyo. Tunaendelea kuwahimiza wananchi wote wasikae kimya, wawe tayari kukemea vitendo vya rushwa pindi vinapojitokeza kwa kutoa taarifa TAKUKURU.
“Kwa taarifa za vitendo vya rushwa fika ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu nawe, tumia TAKUKURU APP, piga simu ya dharura namba 113 au tuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au Piga *113# fuata maelekezo” Huduma hii ni ya BURE.

