Mwili wa Mugabe Wawasili Zimbabwe

MWILI wa aliyekuwa kiongozi wa Zimbabwe, Robert Mugabe, umewasili katika uwanja mkuu wa ndege nchini humo ambapo siku ya mazishi yake bado ina utata kati ya watu wa familia yake na serikali.

Mugabe, aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 37 hadi alipong’olewa na jeshi lake Novemba 2017, alifariki nchini Singapore siku tano zilizopita.

Mpambano wa mahali gani azikwe unatishia kuleta mfarakano kati ya mrithi wake,  Emmerson Mnangagwa, na chama tawala cha Zanu-PF.

Mwili huo ulipokewa na watu wengi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa jijini Harare, wakiwa wamevaa nguo zenye sura yake na ya  Mnangagwa.

Mke wa Mugabe, Grace, na Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Kembo Mohadi, walikuwa miongoni mwa watu waliofuatana na mwili huo.

Leo (Alhamisi)  mwili huo utatolewa heshima katika uwanja wa soka wa Harare kabla ya kupelekwa kijijini kwao Kutama, kilomita 85 kutoka Harare.

Mnangagwa na chama chake wanataka Mugabe azikwe kwenye eneo maalum la mashujaa wa nchi hiyo walioongoza harakati za kupigana uhuru.


Loading...

Toa comment