The House of Favourite Newspapers

Naibu Waziri Mavunde: Sasa sanaa Kuwainua vijana

0

MAVUNDE

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Peter Mavunde hivi karibuni alifanya mahojiano na Wahariri Wetu, Elvan Stambuli na Sifael Paul katika Hoteli ya Atriums jijini Dar es Salaam akazungumzia mengi kuhusu ajira, vijana na walemavu. Ungana nasi katika makala haya sehemu ya pili:

Kila mara kuna migomo ya wafanyakazi inayotokana na kunyanyaswa au kupunjwa haki zao na waajiri, je wizara yako ina mpango gani kuondoa changamoto hiyo?

Jibu: Waajiri wanatakiwa kutii sheria namba 6 ya mwaka 2004,  wengi hawaifuati na hii ndiyo inaelekeza haki kwa pande zote mbili. Wizara ina mpango wa kurekebisha sheria bungeni ili sasa waajiri wasiotekeleza sheria waadhibiwe palepale badala ya kwenda kuwashitaki mahakamani. Hii itasaidia, kwa mfano, mfanyakazi anayestahili kuvaa gloves kazini akikutwa hana, mwajiri apigwe faini palepale bila kupelekwa mahakamani. Hii itasaidia ninavyoona mimi.

Walemavu wengi wanalalamika kukosa ajira licha ya baadhi yao kuwa na elimu na ujuzi, je wizara inawasaidiaje watu hawa?

Jibu:Ni kweli wengi wa walemavu wana uwezo na uelewa mkubwa na bahati nzuri mimi ofisini kwetu tunaye mmoja Naibu Waziri, Mheshimiwa Abdallah Possy, ana uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi kwa weledi. Tunafanya tathmini ili kuwafahamu walemavu wenye elimu na ujuzi mbalimbali ili nao wapewe nafasi za ajira na kuweza kutumikia nchi yao kama watu wengine wasio na ulemavu.

Wafanyakazi wengi wa serikali walitegemea mishahara kupanda siku ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi mwaka huu lakini haikuwa hivyo, unalizungumziaje hilo?

JIBU: Ni kweli hakukuwa na kupandishwa kwa mishahara lakini mheshimiwa rais alitangaza punguzo kubwa la kodi kwenye mishahara. Niwaombe tu wafanyakazi waendelee kuipa nafasi serikali ya kutafakari hilo. Niwahakikishie tu kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli ana dhamira ya kuleta neema kwa wananchi hapa nchini.

Kuna tatizo la ombaomba karibu kila miji mikubwa nchini, wizara ina mikakati gani ya kuondoa tatizo hilo?

JIBU: Ni tegemeo la serikali kutoona watu hawa (ombaomba) barabarani. Mbaya zaidi wengi ni watoto ambao hawapati elimu. Niwasihi walezi wao kwamba wasiwatumie watoto kuomba badala yake wawapeleke wakapate elimu kwa sababu siku hizi elimu ni bure, hivyo wazazi au walezi wawarudishe watoto wao shuleni. Nitumie nafasi hii kumshukunu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa jitihada zake za kuwaondoa. Ombaomba wote wakumbuke kuwa rais alisema kila mtu afanye kazi na watoto wanaopaswa kusoma narudia tena, warudi shuleni wakasome.

Nchi nyingi duniani zinatumia sanaa kama njia mojawapo ya kuongeza ajira na kipato, je wizara yako ina mpango gani wa kuhakikisha sanaa inanufaisha vijana kwa kuwaongezea ajira na kipato?

JIBU: Kwanza serikali inatambua kuwa asilimia 80 ya wanaojishughulisha na sanaa nchini ni vijana. Na Nape (Nape Nnauye ni Wazari wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo) na mimi ni kama mapacha. Tunatengeneza mikakati ili kuifanya sanaa kama kazi na siyo anasa ndiyo maana Nape anakomaa na hati miliki. Mimi nataka ingewezekana kitu kama THT kiwe mikoa yote ili kukuza na kuibua vipaji vya vijana waweze kujiajiri kupitia sanaa. Tunataka wafaidike na sanaa, iwainue kimaisha na waifanye professional (taaluma). Asilimia 71 ya vijana nchini wanatumia muda wao kwa kukaa bure vijiweni. Nawasihi vijana kuwa sasa tuhakikishe tunafanya kazi za kujenga nchi na maisha yetu.

Una changamoto gani unazokumbana nazo kwenye jimbo lako la uchaguzi la Dodoma mjini?

JIBU: Changamoto kubwa ni upatikanaji wa maji salama. Kwa hiyo nafanya juhudi kuhakikisha maji salama yanapatikana. Pili Njaa. Jimboni kwangu kuna tatizo la upatikanaji wa mvua hivyo kusababisha njaa kwa wapiga kura wangu. Tuna mpango wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji. Tulikuwa na changamoyo ya madawati 11,000 lakini tuna mikakati ya kupata 10,000, tatizo hili tutalimaliza hivi punde.  Kuhusu umeme kuna baadhi ya vijiji havina lakini REA watatusaidia kusambaza.

Kwa kusikiliza mahojiano haya tembelea  Global Tv kwa kubofya www.globaltv.tz

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply