The House of Favourite Newspapers

Namna Bora a Kusherehekea Sikukuu na Umpendaye

  NDUGU zetu Waislamu, baada ya kupitia katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, hatimaye Sikukuu wa Eid el Fitr imewadia na kwa sababu sote ni ndugu, sikukuu hii haiwahusu Waislam pekee bali hata watu wa dini nyingine.

Ni kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana leo nimeamua kuja na mada ya jinsi ya kusherehekea sikukuu ukiwa na umpendaye. Kabla sijaendelea, napenda niweke sawa jambo moja kwamba kwa kipindi cha mwezi mzima, kama ulikuwa umefunga, haina maana kwamba msimu wa sikukuu ndiyo ulipizie yale yote uliyokuwa ukiyakosa kipindi cha mfungo.

Na mada hii ni mahsusi kwa wale ambao wapo kwenye uhusiano halali. Najua kipindi cha mfungo kilikuwa kigumu kwako wewe uliyefunga na kuna baadhi ya mambo ulilazimika kuyaacha ili kupata rehema za Mungu.

Kitu cha kwanza, lazima utambue kwamba sikukuu ni maalumu kwa ajili ya kuzileta familia karibu na nitapenda zaidi kuzungumza na wanaume.

Kama wewe ni mwanaume na Mungu amekujalia kuwa na watoto, msimu huu wa sikukuu unapaswa kuwajali watoto wako kwa kuwanunulia nguo nzuri, chakula kizuri kwa kadiri ulivyojaaliwa na mahitaji mengine muhimu.

Lakini si watoto pekee, mkeo naye anayo nafasi yake muhimu. Mjali kwa kumpa mahitaji yake anayotaka ili apendeze. Wanaume wana kawaida ya kuchukulia poa kwamba sikukuu si itapita tu? Kama hujui, ukifanya makosa madogo kwenye kipindi hiki unaweza kuweka ufa mkubwa kwenye penzi lako.

Kwa hiyo hatua ya kwanza ni kama nilivyokueleza, itimizie familia yako mahitaji muhimu na wanawake wengi huwa wanazidisha upendo kwa waume zao endapo watapewa kile wanachokihitaji katika msimu wa sikukuu.

Jambo la pili ni muda wako. Hata kama unafanya kazi na hupati muda wa kupumzika, siku ya sikukuu unatakiwa kushinda na familia yako. Hebu ipe nafasi ya kwanza familia yako, mpe nafasi ya kwanza mwenzi wako kwa kuweka mambo mengine yote pembeni ili upate muda wa kukaa naye.

Sikukuu huwa inanoga zaidi kama utasaidiana na mwenzi wako kuhakikisha maandalizi yote yanakwenda vizuri. Unaweza ukaona kama ni jambo lisilo na maana kumsaidia mwenzi wako kazi ndogondogo za nyumbani lakini wataalam wa mapenzi, wanakwambia kwamba hakunakitu kinachoongeza ukaribu nakuamsha hisia za mapenzi kati yenu, kama kumsaidia umpendaye kazi za nyumbani.

Yawezekana huna kawaida ya kujumuika na familia yako mezani kwa ajili ya chakula, basi itumie sikukuu hii kukaa nao meza moja, kula na kufurahi pamoja. Si tu utaongeza ukaribu kwa familia yako lakini pia utamfanya mwenzi wako azidi kukupenda.

Baada ya yote hayo kukamilika, suala la mwisho na muhimu zaidi ni suala la mtoko. Watu wengi huwa wanaamini kwamba ili mtoke ‘out’ lazima uwe pochi iwe imetuna!

Hapana, baada ya kula na kupumzika, mnaweza kutoka na familia yako kwa matembezi ya kawaida, mnaweza kwenda hata ufukweni tu au sehemu iliyotulia mkiwa pamoja. Achana na ubize wako wa simu, toa muda wako kwa ajili ya uwapendao.

Wengi hudhani kwamba sikukuu inanoga wakiwa viwanja na marafiki. Ukweli ni kwamba sikukuu itakuwa na maana zaidi kama utaitumia kikamilifu na familia yako. Ni matumaini yangu kwamba utakuwa umenielewa vizuri na sikukuu hii itakuwa chachu ya kuboresha ndoa yako na kuimarisha mapenzi na umpendaye.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Comments are closed.