The House of Favourite Newspapers

Namna ya Kukabiliana na Msongo wa Mawazo (Depression)-2

0

Wiki iliyopita tulianza kueleza kuhusu tatizo la msongo wa mawazo na jinsi linavyowasumbua watu wengi.

TULIANZA kwa kutazama dalili za tatizo hilo, leo tunaendelea kuanzia pale tulipoishia, kuhusu dalili za msongo wa mawazo na namna ya kukabiliana na tatizo hili.

-Maumivu ya maeneo mbalimbali ya mwili ambayo hayana maelezo ya chanzo chake hasa.

-Matatizo ya tumbo hasa udhaifu wa usagaji na mmeng’enyo wa chakula, pia tatizo la kukosa choo.

-Kuumwa na kichwa mara kwa mara na wakati mwingine maumivu huwa makali zaidi.

-Kukosa hamu ya kula au kuwa na tabia ya kulakula ovyo

-Kuwa na mawazo ya kutaka kujiua.

-Kuwa katika hali ya kukata tamaa na kuona maisha hayana maana.

-Kukosa uwezo wa kuzingatia mambo.

-Kusoma na kujifunza au mazungumzo na wengine huwa magumu sana.

-Kujitenga na kukimbia majumuiko au mikusanyiko ya aina mbalimbali. Mtu anakuwa na tabia ya kujifungia ndani muda wote akiogopa watu.

-Shughuli za utendaji kwa ujumla zinashuka kwani mawazo yanakuwa kwenye maumivu ambapo kila kitu kinakosa maana mabadiliko ya usingizi, mtu analala kupita kiasi au anakosa usingizi.

-Kukosa hamu ya tendo la ndoa. Mtu mwenye msongo anaweza kupoteza kabisa hamu ya tendo la ndoa. Wanaolaumiwa na waume zao kuwa wanatoka nje kwa sababu hawana hamu ya kufanya nao mapenzi, wakati mwingine wanakabiliwa na msongo.

-Malalamiko ya mara kwa mara ya kuumwa mwili au viungo ambapo hospitalini hawaoni matatizo yoyote.

-Kupoteza kujiamini au mtu kujiuliza mara zote kuhusu thamani yake, hivyo kujishusha kithamani.

-Kuchokozeka kirahisi kwa maneno ya wengine hata kama ni maneno ya kawaida.

-Hasira za ziada za mara kwa mara, hasa pale inapotokea kukwazwa kidogo tu

-Kushtakiwa na dhamira mara kwa mara. Mtu aliyesongeka huamini kwamba yeye ndiye chanzo cha wengine kukosa furaha.

-Kuingia kwenye tabia za uharibifu katika kutafuta ahueni. Tabia hizi ni kama ulevi, umalaya na nyingine za aina hiyo.

Kumbuka kwamba dalili hizi zinaweza kuwa zinasababishwa na matatizo mengine mbali na msongo, hivyo unapaswa kujichunguza kwa makini ili kubaini chanzo cha dalili ulizonazo ni nini. Ili kupata uhakika unapaswa kumuona dakari mara unapohisi dalili ambazo si za kawaida na baada ya vipimo ndipo unaweza kuwa na uhakika kuwa tatizo linalokusumbua ni msongo.

Watu wengi hutumia nguvu kubwa kuimarisha afya za miili yao bila kuzingatia afya ya hisia zao (Emotional health) mpaka pale wanaposhauriwa kufanya hivyo na madaktari.

Kama jinsi afya ya mwili inavyojengwa na kuimarishwa, afya ya hisia pia huhitaji kujengwa na kuimarishwa kwa kutumia mbinu mbalimbali. Ili kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana na msongo, ni lazima uwe na afya nzuri ya hisia.

Unapokosa uimara katika hisia zako ni rahisi kupoteza kinga ya mwili na kuanza kushambuliwa na maradhi ambayo ungekuwa na uwezo wa kukabiliana nayo. Hisia tulivu humsaidia mtu kukabiliana na vikwazo maishani mwake, ambavyo wengine wasingeweza. Huwa na uwezo mkubwa wa kupitia shida na raha bila ya mwili wake kupata madhara yoyote.

Leave A Reply