The House of Favourite Newspapers

NATURE, ROMA, MAN FONGO LEO NI MOTO DAR LIVE, KUANZIA SAA 5 ASUBUHI

Roma Mkatoliki na Man Fongo (kushoto).

KISHINDO kikubwa cha aina yake kitasikika leo Jumapili Jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi maarufu wa Dar Live ulioko Mbagala.

Wale washindi wa Shindano la Tusua Maisha na Global linaloendeshwa na Kampuni ya Global Publishers, leo wanakabidhiwa zawadi zao katika Ukumbi huo namba moja kwa burudani Jijini.


Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Global Group yaliyopo Sinza Mori, Meneja Mkuu Abdallah Mrisho amethibitisha kwamba mastaa wa muziki Juma Nature, Roma Mkatoliki na Man Fongo watapamba shoo hiyo ya bure.


“Tupo karibu zaidi na jamii kwa kuwa wao wamekuwa nasi katika kazi zetu hasa magazeti yetu ambayo ni Amani, Risasi, Championi, Uwazi, Ijumaa, Spoti Xtra na Ijumaa Wikienda hivyo nasi hatuna budi kusema asante kwa mashabiki wetu.

 

“Tutatoa zawadi kwa washindi wa droo ya pili na tatu ambapo mchakato huo utaambatana na burudani kubwa kutoka kwa Roma Mkatoliki, Man Fongo mfalme wa Singeli pamoja na mkongwe Juma Nature,” anasema Mrisho.

 

Meneja wa Dar Live, Rajab Mteta (KP) naye alisema kwa kuwa Jumapili kutakuwa na fainali ya Kombe la Dunia, kutakuwa na nafasi ya mashabiki kushuhudia mchezo huo kupitia runinga kubwa itakayowekwa ukumbini hapo kwa udhamini wa Kampuni ya Sokabet ambayo imedhamini Shindano la Tusua na Global.

 

Mratibu wa Sokabet, John Joseph, alisema kuwa watatoa elimu kwa wateja wake kuhusu ushiriki wa kubashiri matokeo na kusisitiza udhamini wao katika shindano hilo ni kutaka kuifikia jamii kwa ukaribu zaidi kwa kuwa Global ni kampuni kubwa na inawafikia mamilioni ya watu wengi kupitia magazeti yao na vyombo vingine vya habari wanavyomiliki.


Kuhusu burudani, Roma anasema mashabiki wake watarajie mambo makubwa kwa kuwa amejiandaa vizuri na kusisitiza kama kawaida yake anaamini anabeba kijiji atakapo-panda jukwaani.

Lakini Man Fongo anasema shoo ya leo ni moto wa kuotea mbali na kwamba hiyo ni sehemu nzuri kwake kuendelea kuwa karibu na watu wake hasa wa Uswahilini na wasomaji wa magazeti ya Global ambayo yanaongoza kwa kupendwa Tanzania.

 

WASHINDI HADI RAHA

Mkulima na mfanya-biashara wa mazao, Solomon Mapunda, mkazi wa Majohe jijini Dar es Salaam, ameng’ara katika droo ya tatu ya Shindano la Tusua Maisha na Global baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa pikipiki.

 

Mapunda alitangazwa mshindi wa wiki ya tatu wa pikipiki, akifuata nyayo za washindi wengine waliojishindia pikipiki, ambao ni Richard Tanganyika, mkazi wa Mdaula, Chalinze mkoani Pwani na Amiri Bakari, mkazi wa Ubungo National Housing jijini Dar.

 

Washindi wengine katika droo hiyo ya tatu iliyochezeshwa Jumanne ya Julai 10, 2018 na kurushwa moja kwa moja (Live) na Kituo cha Global TV Online ni Oswald Kiyawa, mkazi wa Mtongani Kunduchi jijini Dar es Salaam aliyejishindia jezi, Amour Twalibu wa Ukonga Magereza aliyejishindia headphones za kisasa, Beats by Dre na Rajabu John wa Mbagala Chamazi aliyejinyakulia dinner set.

 

“Tayari washindi wa droo ya kwanza, wameshakabidhiwa zawadi zao lakini kwa washindi wa droo ya pili ambao ni Amiri Bakari, Kenedy Ngubuya, Daniel Jackson na Mwita Matogoro sambamba na washindi wa droo ya tatu, wao watakabidhiwa zawadi zao leo katika Ukumbi wa Dar Live,” anasema Mrisho.

Comments are closed.