The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike-20

ILIPOISHIA

Sikuuona msaada wowote wa mlinzi kwani wakati watu hao wakiingia, yeye alikuwa amelala kitu kilichonifanya kukosa amani, wakati mwingine nikahisi kwamba hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya kufa.

“Ngo…ngo…ngo..” nilisikia mlango ukigongwa.

“Nyie ni wakina nani?” niliuliza huku nikitetemeka.

“Ngo…ngo…ngo..” nilisikia tena ukigongwa.

ENDELEA NAYO

Wakati nikiwa najiuliza kama ilipaswa nifungue mlango au la, mara nikauona mlango huo ukifunguliwa taratibu. Nilishangaa sana, niliufunga mlango kwa ufunguo, sikusikia wakivunja kitasa, sasa kama kuufungua mlango huo waliwezeaje? Nikabaki nikitetemeka, wakaingia na kuanza kuniangalia usoni. Nilitamani ardhi ipasuke niingie ndani.

“Sisi ni wageni wako leo,” aliniambia mwanaume mmoja.

“Wageni wangu?”

“Ndiyo!”

“Usiku huu?”
“Ndiyo!”
“Ila siwajui, nyie ni wakina nani na mnahitaji nini? Naomba mniambie mnataka kiasi gani niwape ila mniache hai,” niliwaambia, kabla ya kujibu, wakaanza kucheka, walicheka sana kitu kilichonifanya niwashangae kwani nilihisi kwamba walikuwa majambazi waliokuwa wakiiba kwa kutumia uchawi.

“Sisi si wezi wala majambazi.”
“Kumbe ni wakina nani?”
“Tumekuja kukuletea vitu!”
“Vitu gani?”

Mwanaume aliyeshika mfuko ule mweusi akaufungua na kutoa nguo mbili, yalikuwa ni kama madela ila yale yalikuwa na rangi mbili tofauti, yaani kulikuwa na vazi moja lililokuwa na rangi nyekundu na nyingine rangi nyeusi.
Mwili wangu ulisisimka sana, sikufahamu mavazi yale yalikuwa ni ya nini, akaniambia nimsogelee na kuchukua, nikafanya hivyo. Niliyachukua na kuanza kuyaangalia, yalionekana kuwa mazito ambayo kwa kifuani kulikuwa na alama ya nyota kubwa ambayo ilizungukwa na miale ya moto.

Kiukweli niliogopa sana, mbali na mavazi yale, watu wale walinipa fimbo ndogo. Kiukweli ukiniuliza mahali walipoitoa ile fimbo ndogo, sifahamu kwani kipindi walichokuwa wameingia ndani, hawakuwa na fimbo yoyote, ila kwenye kunipa, nikashangaa wakiwa na fimbo.

“Hii ni ya nini?” niliwauliza huku nikiichukua fimbo ile.

“Hii ni ya kutoa kafara!”
“Kutoa kafara?”
“Ndiyo! Utakapokuwa pamoja nasi, kuna kipindi utahitajika kutoa kafara. Sisi huwa hatuna masharti kwamba unapotaka uwe tajiri uwe unaishi maisha fulani ya kukubana, yaani usilalie kitanda chako au usivae viatu au kula nyama, unapokuwa pamoja nasi, upo tayari kufanya kitu chochote kile, kwenda popote pale, ila tunachokitaka ni wewe kutoa kafara kila tutakapohitaji damu, si kafara za ndugu zako pekee, hata watu wengine,” aliniambia mwanaume huyo.
“Sawa. Nimeelewa.”
Nilibaki nikizungumza na wale watu kwa dakika zaidi ya tano, baada ya hapo wakaniambia wanaondoka, wakatoka nje huku nikiwasindikiza kwa macho, walipotoka nje ya geti tu, nayo yale manyunyu ya mvua yakaisha muda huohuo, nikashangaa.

Mlinzi akashtuka kutoka usingizini, sikuwa na uhakika kama alikuwa amelala, nilijua kwamba kulikuwa na nguvu fulani iliyokuwa imemfanya kulala namna ile, yeye mwenyewe alishangaa sana, nilipomwambia kwamba alikuwa amelala, aliniomba msamaha.

“Naomba unisamehe shangazi,” aliniambia mlinzi.

“Wala usijali, nimekusamehe,” nilimwambia na kurudi ndani.

Niliondoka na kuelekea chumbani, nilipofika nikayaangalia vizuri yale mavazi niliyopewa. Hayo yalikuwa sare kwa ajili ya wanafunzi ambao walijiunga na dini ile ya kishetani, niliyachukua na kuyavaa kwa zamu kwani nilitaka kuona yanafafanaje.

Huo ndiyo ulikuwa muda wa kujiunga na hiyo dini, ndugu yangu, ninayaandika haya nikiwa na uchungu mkubwa, shetani ana nguvu mno, niliyachukulia kuwa kawaida lakini asikwambie mtu, kumtumikia shetani kuna hasara na hakuna faida yoyote ile.

Asubuhi ilipofika nikaamka na kufanya mambo yangu, sikutaka kutoka kwenda sehemu yoyote ile, nilitulia nyumbani kwani nilijisikia furaha na mchoko wa ajabu.

Ilipofika mchana, kama saa nane hivi nikapigiwa simu na wasimamizi wa biashara zangu kwamba siku hiyo kulikuwa na wateja wengi sana walikuwa kwenye maduka yangu, wao wenyewe walishangaa kwani haikuwa kawaida hata kidogo.
Waliponiambia hivyo, akili yangu ikaanza kupata jibu juu ya kile kilichotokea, mafanikio makubwa yakaanza kuonekana mbele yangu, sikuamini, yaani kujiunga na dini ile, tena siku ya kwanza tu, basi biashara zangu zikaanza kupata wateja wengi.

Kwa sababu nilikuwa kwenye dini yao ya kumtumikia shetani, wafanyabiashara wale wakubwa ambao niliwaona kule wakataka kuonana na mimi, walitaka kuniambia nini cha kufanya ili niwe bilionea mkubwa.

Nikakutana nao na kuzungumza pamoja, walifurahi mno kuniona. Waliniambia nini cha kufanya ili nitajirike zaidi, nilifurahi, mbinu zao zilikuwa kabambe ila wakaniambia kwamba ni lazima nihakikishe najituma na kusaidia watu, ningetajirika zaidi ya nilivyokuwa. Walizungumza kama watu waliomwamini Mungu, kumbe nyuma ya pazia, walimwabudu shetani kwa nguvu zote.

****

Miezi sita ilipita, nilikuwa kwenye mafanikio makubwa mno, Zakia yule hakuwa huyu tena, huyu alikuwa na pesa ndefu ya kufanya kila kitu alichotaka kukifanya. Niliona raha sana, kuna kipindi nilijiona mimi kuwa Mungu kwani niliweza kufanya kila kitu nilichotaka kukifanya.

Kwa kawaida, huwa tunafanya ibada kila siku ya Ijumaa, ibada hiyo huanza saa sita usiku mpaka saa kumi huku kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi tukipewa kazi kubwa ya kutoa kafara.

Hii haimaanishi kafara ya ndugu zako, huwa na maana ya kafara ya watoto, si lazima wawe watoto wako, watoto wowote wale na ndiyo maana mitaani huwa kuna kesi nyingi za kupotea kwa watoto.

Baada ya kukutana katika Ijumaa ya mwisho wa mwezi, hapo ndipo niliambiwa kwamba ilikuwa zamu yangu kutoa kafara kwani ndiyo ilikuwa sheria ya kule tulipokuwa tukikutania.

Kwanza nilishangaa, sikujua kama zamu yangu ingefika kwa haraka namna hiyo, sikutaka kufanya hivyo lakini ugumu ulikuja baada ya kuona kwamba nilitamani kuendelea kuwa tajiri, hivyo isingewezekana kukataa, na kama ningekataa basi ni lazima wangeniambia kwamba wanautaka utajiri wao.

Sikuwa na jinsi lakini sikujua ni kwa namna gani natakiwa kutoa kafara kama walivyokuwa wakifanya. Walichoniambia ni kwamba haikuwa kazi ngumu hata kidogo, walinipa shilingi elfu tano na kuniambia kwamba hiyo ndiyo ingetumika katika kumchukua mtoto.

Haikuniingia akilini kabisa lakini wao walisisitiza kwamba ile ndiyo njia nyepesi ya kufanya kile nilichotakiwa kukifanya. Nikakubaliana nao na hivyo baada ya ibada hiyo, nikaondoka zangu na kuahidi kwamba Ijumaa ya siku hiyo ningekwenda na mtoto hapo kanisani.

Nilipofika nyumbani, usiku sikulala, nilibaki nikijifikiria ni kwa namna gani ningeweza kukamilisha kile nilichoambiwa. Muda ulizidi kwenda mbele, nakumbuka vizuri kabisa kwamba usiku wa siku hiyo sikulala, nilibaki nikifikiria namna ya kufanya.

Mtaa niliokuwa nikiishi hakukuwa na watoto wengi, tena hao wachache waliokuwa wakiishi mtaa huo walikuwa ndani ya nyumba zao, ilikuwa ngumu sana kukamilisha kile nilichotaka kukifanya hivyo nilitakiwa kwenda katika mitaa ya uswahili, sehemu kulipokuwa na watoto wengi na kisha kufanya kile nilichotaka kukifanya.

Nikaondoka nyumbani na kuelekea huko. Kumbuka kwamba sikuwa mtu maarufu, yaani kama ningekuwa maarufu basi ningewatumia vijana kwenda kutafuta mtoto ila kwa kuwa sikujulikana, nikaona si tatizo kama nikienda mimi mwenyewe.

Wazazi wenye watoto wenu wadogo, kuweni nao makini, uchawi upo na bado watoto wanaendelea kutolewa kafara kwa sababu tu wanaachwa peke yao mitaani hivyo kuwapa nafasi watu wabaya kuwaiba na kuondoka nao.

Nakumbuka nilifika Tandale Kwa Tumbo, huko, mimi mwenyewe nilishangaa, kulikuwa na idadi kubwa ya watoto barabarani na hakukuwa na mtu yeyote aliyejali, walionekana kama watoto waliotelekezwa lakini ukweli ni kwamba walikuwa na wazazi wao na kila giza lilipokuwa likikaribia kuingia, waliondoka na kuelekea nyumbani.

Nililipaki gari mbali kabisa na sehemu iliyokuwa ikionyesha video hapo Tandale, nakumbuka iliitwa Tandale kwa Tumbo. Nilijua kwamba ndani kulikuwa na watoto wengi, sikuteremka, nilikuwa nangalia huku na kule, tena nikiwasubiri hao ambao walikuwa ndani.

Nakumbuka nilikaa kwa dakika kama thelathini, nikaona watu wakitoka ndani ya ukumbi ule huku kukiwa na watoto wengi tu. Nikaufungua mlango na kutoka nje, nikamfuata mtoto mmoja wa kiume aliyekuwa mchafumchafu, nikamuita.

“Hujambo mtoto mzuri?” nilimsalimia.

“Sijambo! Mambo anti!” alinisalimia.

Kwanza nikashtuka, alikuwa mtoto kama wa miaka saba, sasa ilikuwaje asiniamkie na mwisho wa siku kunipa salamu ambayo kijana alipaswa kumpaka kijana mwenzake?

Sikutaka kujiuliza sana kwani sikufika hapo ili niamkiwe bali nifanye kile nilichokuwa nimekifuata. Nikaingiza mkono mfukoni na kuitoa ile elfu tano.

“Unaitwa nani?”

“Naitwa Mudi.”
“Unaishi wapi?”
“Naishi hapo mbele…”

Wakati amejibu maswali hayo, nikampa ile elfu tano, akaipokea, nikalifuata gari na kuanza kuondoka kwa mwendo mdogo kuelekea lilipokuwa soko la Tandale.

Wakati naendesha, macho yangu yalikuwa yakiangalia nyuma kupitia kioo kidogo, nikamuona yule mtoto akianza kulifuata gari langu huku akikimbia, sikuendesha kwa mwendo wa kasi, mwisho wa siku nikaona nilisimamishe kumsubiria.

“Anti…” aliniita, nikamfungulia mlango.

“Unasemaje Mudi?”
“Naomba twende wote!”

“Wapi?”
“Unapokwenda wewe!” alinijibu.

“Sawa. Ingia.”

Hakuwa na hofu hata kidogo, nilijua kwamba ile noti ilibadilisha kila kitu, basi hapohapo akaingia ndani ya gari, watu hawakuwa wakitujali sana, kila mtu alikuwa bize na mambo yake, nilichokifanya ni kumwambia afunge mlango, baada ya hapo, hao tukaondoka zetu huku nikiwa nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Ilibaki kumtoa kafara mtoto huyo.

****

Niliondoka naye nikiwa na matumaini makubwa sana kwamba tayari nilimpata mtoto wa kumtoa kafara. Niliendesha gari mpaka nyumbani ambapo nililiingiza gari na kumteremsha na kumpeleka ndani.

Ile noti ilimlevya na hakujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea, hakuwa na akili ya kurudi nyumbani wala kuondoka nyumbani hapo. Nilikuwa na uhakika wa kufanikisha kile ambacho niliambiwa, niliendelea na maisha yangu huku Mudi akiendelea kuwa ndani ya nyumba yangu.

Hakuuliza swali lolote wala hakupaulizia nyumbani kwao. Mara kwa mara marafiki zangu wale mabilionea walinipigia simu na kuniuliza kama tayari nilimpata mtoto, nikawajibu tayari nilikuwa naye.

“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Wewe hatari sana, sisi huwa tunapata tabu sana mpaka kupata watoto, yaani wewe ndani ya siku mbili tu tayari! Heshima kwako,” aliniambia waziri mkuu.

Ilipofika Ijumaa ya kutoa kafara, nikamchukua Mudi na kuondoka naye kuelekea kanisa. Kiukweli nilimuonea huruma kwani nilijua kwamba alikuwa akienda kuuawa lakini hakukuwa na jinsi, ili niendelee kuwa tajiri ilimpasa atolewe kafara kama ilivyokuwa kwa watoto wengine.

Nilionekana shujaa mkubwa, tulipoingia kanisani tu, wanaume wawili wakatokea, hao hutumika kuwashika watoto na kuwapeleka katika chumba fulani, huko huwavua nguo na kuwaleta mbele yetu kisha kuwalaza kwenye meza iliyokuwa maalumu kwa ajili ya kutolea kafara.

Kuna vitu vikitokea, kama binadamu wa kawaida ni lazima uwe na huruma, ndivyo ilivyotokea ndani ya kanisa lile. Wakati Mudi ameshikwa na watu wale, alilia sana, alitaka aachiwe lakini hakukuwa na mtu aliyemwachia, wakamchukua na kuondoka naye kwenda katika chumba kile ambapo akaandaliwa tayari kwa kutolewa kafara.

Mimi na watu wengine tulikaa pale kanisani huku tukiwa na mavazi yetu, tuliendelea kumwabudu shetani pale tulipokuwa huku tukisubiria kila kitu kiendelee.

Baada ya dakika kadhaa, wanaume wale wakaja mahali pale huku wakiwa na Mudi, sikujua walimfanya nini kwani hakubisha wala hakupiga kelele, walipomlaza katika meza ile, kilichofuata ni kuchukua kisu tayari kwa kumtoa kafara.

Wote tuliambiwa tuviinamishe vichwa vyetu, tukafanya hivyo na nilichokisikia baada ya hapo ni kelele za maumivu za Mudi hivyo nikahisi kwamba muda huo ndiyo alikuwa akichinjwa na kutolewa kafara kama ilivyotakiwa kuwa.

Niliumia mno moyoni mwangu, sikuamini kama mwisho wa siku mimi ndiye nilisababisha kifo cha mtoto huyo. Nafsi yangu ikaanza kunihumu, nilijiona kuwa mtu anayestahili adhabu yoyote ile kwani kwa kile nilichomfanyia Mudi, hakika hakustahili mauaji hayo.

“Yote ni kwa ajili yako Zakia! Hivi unafikiri ukifa utazikwa na fedha zako? Mbona unafanya mambo hayo! Au unafikiri ukiwa na pesa ndiyo utanunua kila kitu! Wangapi wamekufa kwa magonjwa hospitalini na wakati walikuwa matajiri, unadhani pesa zao ziliwasaidia?” niliisikia sauti, haikuwa kichwani mwangu au moyoni, niliisikia kama kuna mtu alisimama mbele yangu ndipo akaanza kuniambia maneno hayo.

Nilishindwa kuvumilia kukiinamisha kichwa changu, nikakiinua kidogo kumwangalia mtu aliyekuwa akiniambia hivyo, sikumuona mtu yeyote yule.

“Wewe ni nani?” niliuliza kwa sauti ndogo kabisa.

“Huwezi kunijua, nipo dunianii kote, sionekani ila kazi zangu zinaonekana,” alinijibu kitu kilichonishtua sana.

Akili yangu ikahisi kabisa kwamba huyo alikuwa shetani, nilijipa uhakika huo kwani wakati tulipoinamisha vichwa vyetu, tuliambiwa hiyo ni ishara ya kumwabudu shetani hivyo hata sauti ile niliyoisikia, niliamini kwamba ilikuwa yake.

“Usitake kujiuliza mimi ni nani,” niliisikia tena ikiniambia.

“Ni lazima uniambie, je ni shetani ninayemuabudu?” niliuliza, nilianza kutetemeka kwa hofu, nilijishangaa kuona jasho likinitoka.

“Ninachukia kumuona binadamu niliyemuumba akimuabudu mwingine zaidi yangu. Sikukuumba kumwambudu shetani, nilikuumba uniabudu mimi,” alinijibu, sauti yake ilikuwa ni tofauti kabisa, haikuwa sauti ya ukali, ilikuwa ni ya kipole sana, sauti iliyoonyesha ni jinsi gani alinionea huruma.

“Wewe ni Mungu?” niliuliza, wakati nilipolitaja jina hilo tu, hapohapo nikasikia mahali pale kukianza kutetemeka, watu wote tuliokuwa mahali hapo tukaanguka, mtetemo wake ulikuwa ni kama tetemeko la ardhi.

“Ni nani amelitaja jina hilo?” nilimsikia yule mwanaume aliyekuwa mbele akiuliza huku akiwa anatetemeka kwa hasira.

Hakukuwa na mtu aliyejibu swali lake, kila mmoja akabaki kimya. Nilibaki nikijiuliza juu ya ya mahali pale kutetemeka. Wakati sijapata jibu, nikaisikia sauti ile ikiniambia tena:

“Jina langu ni kuu, jina langu lina utukufu. Kuna kipindi kitafika, nitakutoa katika shimo ulilokuwemo, wewe si mtu wa kuishi humo,” nilisikia sauti hiyo ikiniambia, ghafla nikasikia upepo mkali, hakukuwa na mtu mwingine aliyeusikia zaidi yangu, nikasikia ikiniambia maneno ya mwisho yasemayo:

“Nitakurudia tena muda na wakati kama huu.”

Ukimya ukatawala.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho mahali hapa

Comments are closed.