Nilivunja Ndoa Yangu na Shetani-28
ILIPOISHIA:
Nakumbuka siku moja baada ya kuchukua chakula changu na kusogea pembeni ya jalala chini ya mti wakati nakula, alitokea chizi mmoja wa kiume aliyenipora chakula. Kabla ya kunipora alinitandika makofi mawili mazito ambayo yalinifanya nione kizunguzungu.
SASA ENDELEA…
Lakini kwa vile nilikuwa kwenye ulinzi mzito, mlinzi aliyekuwa akinilinda aliwahi kabla sijadhuriwa zaidi na kumshikisha adabu yule chizi mpaka akapiga magoti kuomba msamaha. Kwa kweli siku ya pili sikuweza kutoka kutokana na maumivu ya kichwa.
Nilitoka baada ya siku tatu ndipo niliporudi kazini, siku zilizobakia nilikuwa makini sana na yule chizi kamili ambaye alifanya vitu kutokana na akili inavyomtuma. Siku nyingine usiku nikiwa naelekea kwenye kiza ambako ndiko nilipokuwa napandia gari, chizi yule alitokea na kunipiga ngwala kama nisingekuwa kwenye ulinzi angenibaka kutokana na kunichania nguo na yeye akiwa tayati amejiandaa kunibaka.
Kama kawaida walimuwahi ila siku ile niliwakataza wasimpige, walimshika na kumuondoa. Hapo ndipo nilipojua kumbe hata wendawazimu nao huwa na hisia za mapenzi. Siku zilikatika huku watu wakinizoea na kuiita kichaa mrembo.
Kwa vile nilifanya vitu katika mipangilio siku ya mwisho nilihamia maeneo ya Pangani kulipokuwa na kanisa kubwa la Fold of The Lord (Zizi la Bwana) ikiwa na maana anakusanya kondoo waliopotea. Lilikuwa kanisa kubwa ambalo lilikuwa likimilikiwa na Papaa ambaye alitambulika kama Mtume na Nabii Mutombo kutoka DR Congo.
Siku zote nilikwenda kwa ratiba na maelekezo ninavyoelekezwa nifanye kituko gani na saa ngapi hasa mbele za watu kufanya watu wanijue. Kama ‘script’ ya mchezo wangu ilivyonielekeza nifanye, nami niliigiza vilevile na kuongeza vyangu.
Hatua iliyokuwa inafuata ilikuwa kwenda eneo la kanisa na kufanya fujo waamini kweli mimi ni kichaa kisha nikamatwe na kuingizwa kanisani ambako Mtume Mutombo ataniponya.
Kama kawaida niliteremshwa sokoni na kuvuta muda mpaka kulipo pambazuka. Ilipofika saa moja na nusu asubuhi nilijongea eneo la kanisani na kukaa karibu kabisa.
Watu walikuwa wengi sana waliokuwa wakienda katika Kanisa la Zizi la Bwana.
Magari ya kifahari niliyaona yakiingia katika uzio wa kanisa, kwa kweli kanisa lile lilikuwa na watu wengi. Nikawa nimesimama nikijipanga kufanya igizo langu ambalo lilikuwa la mwisho. Niliwaza mengi na kujiuliza wingi wa watu wale nini wanachokifuata ikiwa kabisa pale hakuna mahubiri ya kweli.
Nikiwa bado nimejikalia huku nikizidi kustaajabu, gari la kifahari aina ya Hummer lilinipita likiwa limeongozwa na pikipiki mbili mbele na nyuma gari moja na pikipiki moja. Ulikuwa msafara mdogo lakini ulikuwa ukionesha mtu anayeingia pale ni mtu wa hadhi ya juu.
Aliyeingia muda ule alikuwa Mtume na Nabii Mutombo aliyekuwa akiabudiwa kama Mungu. Baada ya kuingia kulipigwa muziki wa Injili uliowanyanyua vitini watu wengi ambao walipita mbele na kuanza kucheza huku wengine wakiendelea kuingia.
Baada ya muda, Nabii na Mtume feki alianza kuhubiri huku sauti yake ikisambaa kila kona kutokana na kuwa na spika za kisasa zenye nguvu za kurusha sauti mbali. Baada ya muda alikuja mtu na kunipa ishara kuwa nianze kazi tulikuwa tumejipanga sawasawa.
Nilibeba fimbo yangu nikaanza kupiga kelekea pale kwenye geti la kanisani huku baadhi ya waumini waliokuwa wakiingia wakinishangaa na wengine kunikimbia. Ulinzi wa pale ulikuwa mzito kama unaingia ikulu, lakini nilipita na fimbo yangu bila kuzuiwa na mtu na kuingia kanisani na kuanza kuwatandika waumini wa siti za nyuma.
Ghafla pakawa na ghasia kutokana na watu kukimbia hovyo, niliwatandika hasa fimbo migongoni mwao wala sikuwa naigiza. Walitokea walinzi walionikamata ili kunitoa nje lakini Nabii Mutombo alipaza sauti na kusema: (kumbuka kila kitu kilikuwa maigizo kasoro maumivu ya fimbo yaliwapata hasa.)
“Msimtoe nje huyu ni mmoja wa kondoo aliyeingia ndani ya zizi letu hivyo anahitaji huduma yetu. Ameeen?”
“Ameeni,” waliitikia wote.
Nilibebwa juu na kupelekwa mbele kwa ajili ya kuombewa nitokwe mapepo. Nilipofikishwa mbele, nililazwa chini huku wakiwa bado wamenishikilia. Baada ya muda niliachiliwa baada ya kauli ya mchunguaji kusema niachiwe.
“We nani?” aliuliza kwa sauti kubwa.
Nikijifanya mapepo yamenipanda nilimvamia Mtume Mutombo kwa kushika vazi lake kwa nguvu mpaka nikalichana.
Kwa vile nilikuwa kazini nilifanya nilichoelekezwa kwa ustadi mkubwa ili ionekane pepo langu lina nguvu kuliko yote yaliyotangulia.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa simulizi hii katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

