The House of Favourite Newspapers

NMB Yakabidhi Gawio la Shilingi Bilioni 10.48 kwa Serikali

Waziri wa Fedha na Mipango – Dr. Philip Mpango, akipokea gawio la shilingi Bilioni 10.48 kwa Serikali, ikiwa ni sehemu ya faida ya benki ya NMB kwa mwaka 2018 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi Joseph Semboja (pili kutoka kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Albert Jonkergouw na Afisa Mkuu wa Fedha Ruth Zaipuna.

 

 

 

Benki ya NMB jana ilikabidhi gawio la shilingi Bilioni 10.48 kwa Serikali ikiwa ni sehemu ya faida ya Benki hiyo ya mwaka 2018.

 

Akikabidhi hundi kwa Waziri wa Fedha na Mipango – Dr Philip Mpango, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB Albert Jonkergouw alisema fedha hizo ni sehemu ya hisa ambazo ni asilimia 31.8 zinazomilikiwa na serikali ndani ya benki ya NMB. Pamoja na gawio hilo, pia NMB imelipa serikalini jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 168.8 ikiwa ni kodi tofauti tofauti kama kodi ya mishahara ya wafanyakazi, kodi ya bidhaa, kodi uendelezaji ufundi stadi (SDL) na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

 

“Tupo imara sana kama Benki ambayo vitabu vyetu vya hesabu vinaonyesha mwelekeo chanya unaosababishwa na utoaji huduma bora za kifedha,” alisema Bw Jonkergouw, na kuongeza kuwa mazingira ya kufanya biashara nchini bado yana fursa mbalimbali na NMB kama Benki yenye mtandao mkubwa ipo katika nafasi nzuri zaidi ya kuiunga mkono jumuiya ya wafanyabiashara nchini ili kufikia malengo yao.

 

 

Akipokea gawio la serikali, Dr. Mpango alifurahi kupokea gawio hili kutoka NMB na kutoa changamoto kwa makampuni na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano.

 

“NMB ni mfano wetu mzuri wa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika ubinafsishaji nchini, wamekuwa wakifanya vizuri sana wakati wengine wamekuwa wakilalamika tu bila na kuacha kuzitumia fursa nyingi zilizopo nchini kama wanavyofanya NMB katika kupanua zaidi biashara zao,” aliongeza.

 

 

Katika mkutano mkuu wa wanahisa uliofanyika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam, wanahisa walipitisha kiasi cha shilingi bilioni 33 kama gawio ambalo limegawanywa kwa wanahisa ikiwa ni sawa na shilingi 66 kwa hisa moja. Katika kipindi cha mwaka uliopita, NMB iliweza kupata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 142 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3 kutoka shilingi bilioni 138 katika mwaka uliotangulia.

 

 

Bw Jonkergouw alisema Benki inaendelea kuweka uwiano mzuri katika kutoa gawio kwa wanahisa na pia kuwekeza ili kuimarisha biashara ya benki na kuifanya ichangie zaidi katika uchumi. NMB ni moja ya makampuni yaliyobinafsishwa na serikali na kuweza kupata mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka kumi imeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni 118 kwa serikali kama gawio.

 

 

“NMB imekuwa ikifanya vizuri sana katika biashara na itaendelea kujizatiti ili kuwa imara na kutoa huduma bora zaidi. Ili kutekeleza hili, NMB itaendelea kujiimarisha kiuwekezaji katika mifumo yake ya malipo ili kuwawezesha wateja kupata huduma bora zaidi na kuchangia ukuaji wa Uchumi,” alisema.

MAJERUHI WA AZAM HOI KITANDANI AZUNGUMZA – VIDEO

Comments are closed.