The House of Favourite Newspapers

OFM YANASA VYUO VIKIUZA VYETI KWA WATU BILA KUSOMA

UKISIKIA kuna baadhi ya vyuo vya elimu hapa nchini vinauza vyeti halisi kwa watu bila wao kusomea taaluma yoyote, si itakuwa ni kashfa nzito kwa vyuo husika?

Vuta pumzi; mazito yanashuka bila chenga; Risasi kupitia makachero wake wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ limebaini vyuo kibao jijini Dar es Salaam vyenye usajili serikalini vinauza vyeti kama njugu.

Iko hivi; kwa mfano hapa jijini Dar, ukitaka cheti cha udereva, usimamizi wa hoteli, mafunzo ya kompyuta na kozi nyinginenyingine, eti kwa ujanjaujanja tu unaweza kukipata bila hata kuingia darasani.

Usibishe! OFM kwa takriban miezi miwili wamefanya kazi ya uchunguzi katika vyuo mbalimbali na kubaini kuwepo kwa tabia ya uuzwaji wa vyeti hasa kwenye vyuo vinavyotoa ujuzi mbalimbali.

 

CHANZO CHA UCHUNGUZI

Chanzo cha OFM kuingia kazini kuchunguza kashfa ya uuzwaji wa vyeti ilianza siku chache tu baada ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuwatangazia kiama madereva wa mabasi ya abiria kuwa wasiokuwa na vyeti vinavyoonesha kuwa wamesomea udereva leseni zao zitakuwa matatani.

Kama hukumuona ndugu, rafiki, jamaa, jirani yako ambaye ni dereva akihaha kujinusuru na tangazo hilo la polisi basi ujue huko karibu na madereva, lakini ki ukweli hali ilikuwa tete na kila mtu asiyekuwa na cheti alitamani aamke awe kakipata ili kibarua kisiote nyasi.

 

Kutapatapa huko kwa madereva ndiko kulikoibua kashfa kwa baadhi ya vyuo vya udereva kuanza mtindo wa kuwauzia madereva vyeti bila wao kusomea chochote.

“Jamaa alikuwa vibaya sema nini, kuna rafiki yake kamsaidia kupata cheti,” Kamanda mmoja wa OFM alisikia mazungumzo haya kutoka kwenye kijiwe kimoja wanachokaa madereva eneo la Mwenge.

Kauli hiyo haikupita kama wimbo mzuri kwa kachero wa OFM bali ilikuwa ni tipu ya kuanza kufanyia kazi maswali ya inakuwaje mtu anaweza kusaidiwa kupata cheti?

Baada ya pekuapekua nyingi za dokezo za kihabari, Risasi lilibaini kuwepo kwa mchezo mchafu vyuoni ambapo liliwatuma wapambanaji wake kukusanya taarifa na ushahidi wa baadhi ya vyuo kuuza vyeti kwa watu ambao hata abc hawaijui.

“Uchunguzi wetu usiishie kwenye vyuo vya udereva, uende mbali zaidi ya hapo hasa kwenye hivi vyuo vidogovidogo vilivyosajiliwa kutoa mafunzo mbalimbali.

 

“Nadhani nikisema hivyo mnaelewa nasema nini, si mnajua kuna vyuo vinatoa mafunzo mengi, utakuta chuo kimoja kinafundisha kozi kibao.

Uhasibu, ushonaji, hotelia, upishi hivi vyote ni vyema tukapita kutazama kama navyo vinafanya mchezo huo,” kamanda mkuu wa OFM aliwaelekeza vijana wake ambao kwa maelekezo walianza na vyuo vya udereva.

 

VYETI VYAPATIKANA KIULAINI

Pengine kwa kuwa makachero wa OFM wamezoea kufanya uchunguzi wa mambo magumu, siku ya kwanza ambayo ilikuwa ni mwishoni mwa Agosti mwaka huu walipoanza kuvichunguza baadhi ya vyuo vya udereva jijini Dar walijikuta katika kazi rahisi kama kumsukuma mlevi.

CHUO CHA KWANZA

Walipofika kwenye chuo cha kwanza kilichopo Temeke, jina linahifadhiwa kwa sababu maalumu na kuonesha nia ya kupata cheti bila kusomea, walikubaliwa na gharama zake ilikuwa ni shilingi laki moja.

“Siku yoyote ukipata fedha wee njoo unione, usiende kwa mtu mwingine au kama vipi acha advance nikutengenezee kabisa ukija kumalizia ukute kiko tayari,” mkufunzi mmoja chuoni hapo alisema bila hofu.

 

CHUO CHA PILI

Kiko eneo la Buguruni, ambapo makachero wa kike wenye mvuto wa kikosi kazi cha OFM walipofika kutaka kupatiwa vyeti haramu, lilikuwa jambo rahisi kuliko hata kumeza tonge la ugali, huku bei ikiwa ni shilingi elfu sitini.

Kutokana na wepesi wa kazi hiyo siku ya kwanza, ya pili na ya tatu tayari OFM walikuwa wamekusanya takwimu za kutosha na kwamba kilichokuwa kimesalia ni kutoa fedha ili kupatiwa vyeti vya udereva.

UNUNUAJI VYETI WAANZA

Mara baada ya kupatikana kwa uhakika wa baadhi ya vyuo kuuza vyeti, timu ya Risasi ilikubaliana kukunua vyeti vichache vitakavyothibitisha uwezo wa mtindo huo mchafu ambapo ilifanyika hivyo.

Hata hivyo kioja cha aina yake ni pale mkurugenzi mmoja kutoka chuo cha udereva kilichopo Magomeni jijini Dar, alipotaharuki baada ya kubaini kuwa chuo chake kimeingia katika kashfa ya kuuza vyeti kinyume cha utaratibu.

 

ILIKUWAJE?

Mara baada ya ushahidi wa picha za mnato, sauti na video kuchukuliwa kwa siri na makachero wetu kutoka kwenye baadhi ya vyuo vilivyochaguliwa kubeba uthibitisho, kazi nyingine iliyofuata ni kurudi tena kwenye vyuo hivyo kama waandishi ili kufanya mahojiano laivu na wahusika.

Mapema wiki hii waandishi wetu wakiwa na vyombo vyao vya kukusanyia habari walifika kwenye chuo kimoja cha mfano kilichopo Magomeni kwa lengo la kufanya mahojiano maalumu na mkurugenzi wa chuo hicho ambaye tunamtaja kwa jina moja la Lyatuu, kwa sababu maalumu ambapo awali ilikuwa furaha kwake lakini baadaye ukaja uchungu.

 

MAHOJIANO LAIVU NA MKURUGENZI

OFM: Vipi hapa kwenye chuo chako mnatoa huduma gani?

Mkurugenzi: Sisi tunafundisha madereva wa magari madogo kuanzia tani moja mpaka tatu na nusu na magari mengine binafsi na ya mizigo.

OFM: Hivi karibuni serikali ilitoa agizo la madereva wote kupitia vyuo vya udereva kabla ya kupatiwa leseni, hilo unalizungumziaje?

Mkurugenzi: Hilo ni jambo jema sana maana udereva ni kazi inayotaka umakini wa hali ya juu hivyo ni muhimu dereva kupitia chuoni ili awe na elimu ya kutosha ikiwemo kujua alama za barabarani.

 

OFM: Sambamba na hilo la madereva kutakiwa kuwa na vyeti, imeibuka tabia ya vyuo kuwauzia vyeti watu bila kusomea na wengi wao siyo madereva na hawajawahi kuendesha gari hilo, nalo unalizungumziaje?

Mkurugenzi: Kwa kweli hao wanaofanya hivyo si waaminifu na hicho kitendo hata mimi nakipinga sana na hapa chuoni kwangu sitaki kitokee.

OFM: Sasa chuo chako ni miongoni mwa vyuo vinavyodaiwa kufanya mchezo huo mchafu.

Mkurugenzi: Aaah! Hilo hapa kwetu halipo kabisa.

 

OFM: Mkurugenzi ushahidi tunao, kabla ya sisi kufika hapa ofisini kwako sasa hivi kuna mwenzetu alikuja hapa kumnunulia cheti mtu ambaye hajasoma hapa na wala hata kukanyaga hapa hajawahi mkamuuzia cheti na anacho.

Makurugenzi: Hebu nioneshe huo ushahidi.

(Mwandishi wa OFM anamuonesha Mkurugenzi huyo picha za video na mnato jinsi wa OFM alivyofika kwenye chuo hicho na kueleza shida ya kununua cheti hicho kwa shilingi 40,000/)

Katika picha hizo Mkurugenzi huyo akaoneshwa watumishi wa chuo hicho wanavyopokea pesa hiyo na kumuahidi kumtengenezea cheti hicho huku wakijinadi kwa OFM kuwa wameshawasaidia sana watu kwa njia hiyo.

 

“Ngoja tuondoe usumbufu cheti kipo hapa unaweza kukiona pia,” Mwandishi Wetu alimuonesha cheti kilichokuwa kimepigwa picha kwa simu huku kikiwa na sahihi ya mkurugenzi huyo.

OFM: Umejionea sasa Mkurugenzi.

Mkurugenzi: Duuuh… Isssh,” alishusha pumzi huku sura ya furaha ikitoweka kama moshi.

OFM: Vipi hawa unaowaona kwenye hizo picha unawatambua?

Mkurugenzi: Ndiyo, wote nawatambua huyu aliyesimama ni kijana ambaye yupo hapa ofisini kwetu.

OFM: Hiki cheti nacho unakitambua?

 

Mkurugenzi: Kweli hiki ni cheti chetu na hii hapa chini ni saini yangu kabisa, ofuuu!

OFM: Sasa kwa nini mnafanya hivi; hamjui kwamba kazi ya udereva ina jukumu kubwa la kubeba roho za watu?

Mkurugenzi: Ukweli hiki cheti sijakitoa mimi.

Anawaita wafanyakazi wake na kuwaonesha picha na cheti hicho, hawaambii lolote zaidi ya kuwaambia kakaeni.

OFM: Hata kama hujakitoa wewe lakini kina saini yako. Sasa baada ya kuona ushahidi unaiambia nini serikali?

 

Mkurugenzi: Kwa kweli ndugu waandishi kwa hili tumekosea na tunaomba mtusamehe hatutarudia tena. Naomba tusaidiane, tutakamatwa.

OFM: Lazima mtambue kuwa lengo letu sisi si kuharibu kazi za watu lakini ni kuilinda jamii na madudu kama haya.

Hivi ndivyo mazungumzo ya Mwandishi Wetu na mkurugenzi huyo yalivyomalizika kwa huzuni.

 

SI VYUO VYA UDEREVA TU

Kutokana na uchunguzi uliofanywa na OFM, madudu mengi ya uuzaji vyeti yaligundulika si kwa vyuo vya udereva tu bali hata hivi vinavyotoa fani mbalimbali kwa ngazi za cheti na diploma.

Pengine kitu kinachotofautisha namna ya uuzaji vyeti katika baadhi ya vyuo hivyo ni vingine huuza kirahisi na vingine walau vinalazimika kufuata taratibu nyingine za usajili kama mwanafunzi kisha baadaye hutoa vyeti bila kujali kama mhusika hajasoma chochote.

 

WAZIRI AWA MBOGO

Baada ya kufanya uchunguzi huu wenye kashfa kwa baadhi ya vyuo, Risasi lilimtafuta Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako ambaye aligeuka mbogo na kutaka apelekewe ushahidi ili vyuo hivyo vifutwe mara moja.

“Unataka kauli ya serikali? Mimi nasema kauli ya serikali ni hii, lete ushahidi huo haraka tuvifute vyuo hivyo mara moja. “Hivi karibuni tumefuta vyuo vitano, tumefungia vingine saba, serikali hii haitaki mchezo kuhusu suala la elimu,” Waziri Ndalichako alisema kwa kufoka.

 

KUTOKA KWA MHARIRI

Magazeti Pendwa ya Global Publishers ambayo ni Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi na Amani yamedhamiria kufichua maovu, hivyo kama unaona kuna sehemu imeoza na ungependa OFM ipafanyie kazi, wasiliana nasi kwa namba 0658798787.

Stori:Mwandishi Wetu, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.