The House of Favourite Newspapers

PENZI LA AUNT E ZEKIEL, IYOBO KIZUNGUZUNGU

 

 

NI KAPO iliyobamba vilivyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kuvutia mashabiki wengi wa muziki wa Bongo Fleva na Bongo Muvi.

Uhusiano wao uliwavutia wengi kutokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ni ile ya Aunt Ezekiel, mrembo bei mbaya Bongo Muvi, kuachana na mapedeshee wa mjini na kutua kwa dansa wa Wasafi Classic Baby (WCB), iliyo chini ya mnyama mkali, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Mose Iyobo.

Penzi la wawili hao liliendelea kuwaka kama nyota kiasi cha kujaliwa kupata mtoto wa kike aitwaye Cookie. Lakini zipo tetesi kuwa penzi lao limeingia mdudu na kwamba kila mmoja anaishi kivyake.

Risasi Jumamosi liliwasaka mastaa hao na kufanya nao mahojiano kuhusiana na kuvunjika kwa penzi lao kama inavyodaiwa na wadau mbalimbali, ambapo Aunt alikuwa wa kwanza kupatikana na kufunguka mengi, ikiwemo suala la fumanizi.

Fuatilia mahojiano kamili hapa chini;

Risasi Jumamosi: Lakini Aunt, hebu kuwa mkweli, hizi tetesi kuwa wewe na mzazi mwenzio, Mose Iyobo mmetengana zina ukweli?

Aunt: Hivi kwa nini watu wanapata shida kiasi hicho? Kama wanajua tumeachana, itakuwa wanapajua mpaka nyumbani, wangekuja ili wathibitishe ndio waseme hilo.

Risasi Jumamosi: Wengine wanasema wewe ndio umeamua kuondoka na kumuachia nyumba Iyobo, ikoje hii?

Aunt: Ndio maana nikakuambia, kwa nini watu wanasema tu huko nje? Waje nyumbani ndio watagundua nini kinaendelea.

Risasi Jumamosi: Kuna tetesi kuwa mume wako wa kwanza, Sunday Demote, ametoka jela, ndio maana visa vimeanza kwa Mose ili urudi kwake, kuna ukweli katika hilo?

Aunt: Hivi wanaosema Sunday katoka sijui maneno wameyatoa wapi? Lakini hata kama ametoka ana shida gani kwenye uhusiano wangu? Maana anajua kila kitu na alikubali kwa sababu mimi ni mwanamke kama walivyo wengine, nisingeweza kukaa kwa muda wote huo.

Risasi Jumamosi: Kwani kuna tatizo gani labda kati yenu… mlishawahi kufumaniana?

Aunt: Kwenye mapenzi hilo halikwepeki kabisa au siwezi kusema haliwezi kutokea. Ni mambo ya kawaida.

Risasi Jumamosi: Kwa hiyo unataka kusema bado mko kwenye uhusiano mzuri na mzazi mwenzio?

Aunt: Sasa sijui katika hilo naliwekaje maana hata nikisema ndio bado hawataamini maana kama mwanzo waliamini ndivyo watakavyoendelea.

Risasi Jumamosi: Lakini mbona sasa hivi humuweki tena kwenye mitandao ya kijamii kama ilivyokuwa huko nyuma?

Aunt: Kwa hiyo mtu usipomuweka kwenye Instagram yako mmeachana? Mapenzi ni ndani sio mtandaoni.

Risasi Jumamosi: Ulishawahi kupigwa na Mose?

Aunt: Ndio kwenye mapenzi kawaida mbona.

Risasi Jumamosi: Vipi mna mpango wa kuongeza mtoto mwingine?

Aunt: Hiyo sasa ni mipango yangu mimi mwenyewe.

Risasi Jumamosi: Vipi mpango wa kufunga ndoa, maana mmekaa muda mrefu sasa.

Aunt: Hivi sasa kuna mtu anafikiria ndoa kweli? Sina mpango huyo kwa kweli.

Baada ya gazeti hili kumalizana na Aunt, lilimsaka Iyobo, ambapo swali la kwanza kuulizwa ni ukweli kuhusu madai ya kuachana na Aunt.

Iyobo anafunguka: “Hayo maneno nimeshayazoea sana kwa hiyo kuna wakati naona kama ni nyimbo.

Risasi Jumamosi: Kwa hiyo hakuna tatizo na mnaishi wote?

Mose: Sasa nikaishi wapi na yule ndio mama watoto wangu? Watu waache tu kusikiliza maneno, wangekuja nyumbani wangetukuta wote.

Risasi Jumamosi: Asante sana

Mose: Karibu tena.

Risasi Jumamosi linaendelea kufuatilia kwa karibu sakata hili. Tutawahabarisha kinachoendelea, ikiwa tutapata jambo jipya kutoka katika uhusiano wa wawili hawa.

 

 

MAKALA: IMELDA MTEMA

 

Comments are closed.