The House of Favourite Newspapers

Polepole Awazungumzia Viongozi Wa Dini

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole.

KATIBU  wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole amesema Askofu Zakaria Kakobe  na viongozi wengine wa dini  hawajazuiwa kuongea na kwamba wako huru kutoa maoni yao.

Polepole alisema hayo jana wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni  aliposema hakuna mtu ambaye ametishwa kwa kusema ukweli juu ya jambo fulani ambalo huenda lipo au linatokea Tanzania.

“Hakuna mtu amezuiliwa kuongea ukweli  Tanzania, hakuna mtu ametishwa kwa kusema ukweli na hasa katika uongozi wa awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.  Anayesema kuna mtu kazuiwa kuzungumza atakuwa na matatizo,  ila nachofahamu ni kwamba mtu kuzungumza lugha ya matusi, kwa mujibu wa katiba yetu na sheria zetu ni makosa,” alisema Polepole

Polepole aliendelea kusisitiza kuwa viongozi hao wa dini wapo wazi na huru kusema chochote kile kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Mst. Projest Rwegasira, ilitoa onyo na kuwataka viongozi wa jumuiya za kidini kutotumia mahubiri yao ya ibada kwa kufanya uchambuzi wa masuala ya siasa.

Comments are closed.