The House of Favourite Newspapers

PROFESSOR JAY KUIUNGANISHA KENYA, UGANDA

Joseph Haule ‘Professor Jay’

MBUNGE wa Jimbo la Mikumi, mkoani Morogoro, ambaye hujiita Mbunge wa Watu na Wanyama, Joseph Haule ‘Professor Jay’ au Mgodi Unaotembea, ni miongoni mwa wanamuziki wa kitambo kwenye gemu la Bongo Fleva, ambaye pia amefanya mengi.

Ujio wake mpya aliouachia miezi ya karibuni wa Pagamisa, akiwa amemshirikisha Prodyuza Mr. T- Touch, huku mkali wa michano Young Dee akitia vionjo pia.

Professor, amepata nafasi ya kuzungumza na Risasi Jumamosi kuhusu kazi zake za muziki na mambo mengine, ungana naye kwenye mahojiano;

Risasi: Ninakumbuka uliwahi kuzungumza na Global TV, ukaeleza albamu utaachia kuanzia Agosti, kwa sasa umefikia wapi?

Professor: Nimefika sehemu nzuri tu. Lakini hasa ninasubiri vikao vya bunge viishe. Vikimalizika tu, Agosti ninaingia kwenye kazi hiyo ya albamu miguu miwili.

Risasi: Uliwahi kuzungumzia pia ujio wa Jaguar pamoja na Bobi Wine, umefia wapi?

Professor: Tupo kwenye mazungumzo mazuri. Kikubwa tunasubiri bunge lipumue hapa na kwao huko wapate nafasi, halafu tutamaliza, maana kwenye mpango huu yumo hadi Sugu. Pia, si ujio tu, bali mpaka ziara. Tutaiunganisha Kenya na Uganda.

Risasi: Kutokana na kuwa ‘busy’, bungeni na muziki, ni muda gani hasa unapata nafasi ya kuwa na familia?

Professor: Ninapokuwa mapumziko. Wikiendi na siku nyingine ambazo ninajipangia niwe karibu na familia yangu. Kwa hiyo muda wangu ninaugawa vizuri tu wala hakuna tatizo.

Risasi: Kipi unapenda hasa kufanya zaidi unapokuwa na nafasi?

Professor: Yapo mengi kiukweli na si jambo moja. Zaidi ninapendelea kuandika mashairi, kusikiliza nyimbo na kuwa karibu na watu wangu ninaowapenda.

Makala : Boniphace Ngumije

Comments are closed.