The House of Favourite Newspapers
gunners X

Raia wa Kenya Aliyehukumiwa Kukatwa kichwa Saudi Arabia Aachiwa Huru

Stephen Abdulkareem Munyakho, raia wa Kenya aliyekuwa akikabiliwa na adhabu ya kifo nchini Saudi Arabia

Stephen Abdulkareem Munyakho, raia wa Kenya aliyekuwa akikabiliwa na adhabu ya kifo nchini Saudi Arabia, hatimaye ameachiliwa huru baada ya juhudi za muda mrefu kuzaa matunda. Munyakho alikuwa amehukumiwa kunyongwa kwa upanga kufuatia shtaka la kuhusika katika tukio lililosababisha kifo cha raia wa Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, utekelezaji wa hukumu hiyo ya kifo ulikuwa umeahirishwa mara kadhaa kwa sababu ya juhudi za kidiplomasia na ombi la serikali ya Kenya kupewa muda zaidi ili kutafuta fidia kwa familia ya marehemu, kama inavyotakiwa chini ya sheria ya Qisas nchini Saudi Arabia.

Katika mfumo wa sheria wa Saudi Arabia, Qisas huruhusu familia ya mwathirika kutoa msamaha kwa mhalifu iwapo fidia – maarufu kama “diyya” – italipwa. Kwa kesi ya Munyakho, familia ya marehemu ilikubali kusamehe kwa masharti kwamba fidia ya dola milioni moja (takriban shilingi milioni 130 za Kenya) ilipwe.

Kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali, taasisi za kidini, watu binafsi na serikali, fedha hizo zilifanikiwa kukusanywa na hatimaye kulipwa. Hatua hiyo ilifungua mlango wa msamaha kutoka kwa familia ya marehemu, na kusababisha kuachiwa huru kwa Munyakho, ambaye sasa anatarajiwa kurejea nchini Kenya baada ya miaka kadhaa gerezani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imeeleza kuridhishwa na uamuzi huo, na kupongeza mashirika yote na raia waliotoa msaada wao kwa hali na mali kuhakikisha maisha ya Mtanzania huyo yanasalimika. Serikali pia imesisitiza kuwa itaendelea kuwasaidia raia wake wanaokumbwa na changamoto katika mataifa ya kigeni.

Kisa cha Munyakho kimeibua hisia kali miongoni mwa Wakenya, wengi wakielezea mshikamano na kupongeza mshikamano wa kitaifa uliofanikisha hatua hiyo ya kuokoa maisha ya raia mwenzao.

Comments are closed.