Rais Samia Azungumza na Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani – (Picha +Video)

RAIS Samia Suluhu Hassan Aprili 15, 2022 amekutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris karibu na Ikulu ya Marekani ambapo ameliomba taifa hilo kubwa kuongeza mashirikiano ya sekta yake binafsi nchini Tanzania.
“Ombi langu la pekee hapa ni kuitaka serikali ya Marekani kuhimiza zaidi sekta binafsi kufanya kazi nasi,” alimwambia Kamala jijini Washington DC siku ya Ijumaa. “

“Serikali yangu ingependa kuona uhusiano wetu ukikua zaidi na kuimarishwa hadi kufikia kiwango cha juu.”
Mkutano huo wa kihistoria baina ya viongozi hao umekuwa wa kipekee ukiwaleta pamoja Rais Samia, Mwanamke wa kwanza kuongoza Taifa la Tanzania na Kamala Mwanamke Mweusi wa Kwanza kushika wadhifa wa Makamu wa Rais kwa Taifa hilo kubwa duniani.

Kabla ya mkutano wao, Kamala aliwaeleza waandishi wa habari kuwa majadiliano kati yake na Rais Samia yatahusu kuimarisha demokrasia, uwekezaji na ukuaji wa uchumi, na afya.

“Utawala wetu umejitolea sana kuimarisha uhusiano nchini Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla,” Harris alisema. “Hili limekuwa eneo la umakini na kipaumbele kwa rais [Joe Biden] na kwangu.”
Hii ni mara ya pili kwa Rais Samia kufanya ziara nchini Marekani. Mara yake ya kwanza ilikuwa pale alipo hotubia kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwezi Septemba 2021.
PICHA NA IKULU