Afrika Kusini Yapinga Kuahirishwa kwa Kesi Dhidi ya Israel Baada ya Makubaliano ya Amani

CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI — Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amethibitisha kwamba makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Palestina, yaliyosimamiwa na Marekani, hayataathiri kesi ya mauaji ya kimbari ambayo nchi yake imeifungua dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Akizungumza bungeni jijini Cape Town, Ramaphosa alisema serikali yake itaendelea na mchakato wa kisheria ulioanzishwa mwaka 2023, akisisitiza kwamba “haki lazima itendeke bila kuathiriwa na diplomasia.”
“Mkataba wa amani hautaathiri kesi iliyo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki,” alisema Ramaphosa. “Israel italazimika kujibu hoja zetu ifikapo Januari 2026.”
Afrika Kusini iliwasilisha kesi hiyo Desemba 2023, ikiituhumu Israel kutenda vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Gaza. Hati kamili ya madai hayo, yenye zaidi ya kurasa 500, iliwasilishwa rasmi Oktoba 2024.
Kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwaka 2027, huku hukumu ya mwisho ikitarajiwa mwishoni mwa 2027 au mapema 2028.
Mahakama ya ICJ tayari imetoa amri za muda ikiiamuru Israel kuzuia vitendo vya kimbari na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza — ingawa utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua. Kwa mujibu wa mamlaka za afya za Palestina, zaidi ya watu 67,000 wamepoteza maisha tangu mapigano kuanza Oktoba 2023.
Ramaphosa alisisitiza kuwa hatua hiyo si tu ya kisheria, bali pia ni ya maadili.
“Haki ni nguzo muhimu ya maridhiano ya kweli,” alisema. “Hatuwezi kusonga mbele bila uponyaji unaohitajika, na huo utatokana na kesi hii kusikilizwa ipasavyo.”
Mbali na kesi hiyo, Afrika Kusini inashirikiana na mataifa mengine kupitia kundi la kimataifa lijulikanalo kama “The Hague Group,” lililoanzishwa Januari 2025, likiwa na lengo la kushinikiza uwajibikaji wa Israel kwa kutumia njia za kisheria, kidiplomasia na kiuchumi.

