The House of Favourite Newspapers

Rayvanny Aibuka Sakata la Diamond na Shonza

Diamond na Rayvanny.

 

MSANII wa Bongo Fleva kutoka Lebo ya Wasafi, Rayvanny amevunja ukimya kuhusu sakata la bosi wake, Diamond Platnumz, kufungiwa baadhi ya nyimbo zake na Mamlaka ya Mawasiliano nchini  (TCRA) chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa madai kuwa zinakiuka maadili ya Kitanzania.

 

Akihojiwa Jumanne wiki hii kupitia kipindi cha The Play List kinachorushwa kupitia kituo cha Radio cha Times FM, Diamond alimshutumu Naibu Waziri wa Habari, Juliana Shonza, akidai kuwa hakujulishwa wala kuitwa kuhojiwa kabla ya kufungiwa nyimbo zake huku akisema muziki ndiyo unaompa kila kitu maishani hivyo kitendo cha kufungia nyimbo zake ni kumdidimiza na kuushusha muziki wa Tanzania badaa ya kuukuza.

 

Kwa upande wake Shonza alisema hawezi kujibizana na Diamond kupitia mitandao wala vyombo vya habari, kwani walishamwandikia barua nyingi na hakufika, hivyo wasingeweza kumvulimia. Alisema kama Diamond ana malalamiko afike ofisini kwake ama Baraza la Sanaa (BASATA) na si kwenye vyombo vya habari.

Wakati huohuo, Waziri wa Habari, Dkt. Harrison Mwakyembe ameelezea kushangazwa na matamshi ya Diamond kwa Naibu Waziri Shonza bila kujali kuwa alikuwa  anajibizana na mamlaka za serikali.

 

Baada ya hayo, Rayvanny ameamua kufunguka kuhusu jambo hilo kama ifuatavyo:

 

 

“Kuna vitu pengine unaweza ukawa unapatia au vingine unakosea, sitaki kuongelea hilo sababu we nawe ni binadamu, ila kwenye kusema ukweli nitasema. Si kwa sababu wewe ni bosi wangu, hapana, ila mara nyingi thamani ya mtu na umuhimu wa mtu wengi wanaujua akishaondoka.

 

“Muziki ni kazi na ni ajira, namaanisha kuna familia nyingi zinaishi kupitia huuhuu muziki. Diamond katika wasanii wote umekuwa chachu ya kuongeza thamani ya muziki, na kupitia wewe naamini wengi wanafanikiwa.

 

“Kujitoa kwako, kuamini katika umoja na pia kuthubutu ndiko kunafanya unafanikiwa. Ushaambiwa hujui kuimba ila ukaimba ukafanikiwa, ushaambiwa unavimba unaigiza maisha lakini sasa unayaishi hayo maisha, hakuna anayefanikiwa akakosa maadui, ndivyo dunia ilivyo.

 

“Mimi ulinisaidia, ulijua shida zangu, naamini Mungu alikutumia wewe ukawe mkombozi wangu, kwa hiyo kumbuka ‘ili mbegu iote lazima ioze’, sina muda wa kumsema mtu ila nakupa moyo, fanya kazi Simba, kama wewe unaamini katika upendo na si chuki.”

 

Comments are closed.