The House of Favourite Newspapers

Rostam Awa Mfalme Yanga

ROSTAM Aziz ni kama mfalme kwa sasa Yanga hii ni baada ya mastaa wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Sekilojo Chambua kuupongeza ushauri alioutoa kwa klabu hiyo.

 

Juzi Alhamisi, Rostam alijitokeza hadharani na kuweka wazi mikakati yake ya jinsi gani ataisaidia Yanga ili iweze kutoka hapa ilipo na kupiga hatua kubwa kiuchumi kama zilivyo klabu nyingine kubwa Barani Afrika.

 

Rostam ambaye alichangia Sh mil 200 kwenye harambee ya Kubwa Kuliko ambayo iliandaliwa na klabu hiyo Jumamosi iliyopita, alisema ataisadia Yanga kama mpenzi na shabiki wa timu hiyo lakini siyo kama mfadhili au mmiliki.

 

Hali hiyo imepokelewa kwa mikono miwili na wapenzi na mashabiki wa Yanga kwa kudai kuwa itaifanya Yanga kuwa kubwa na ambayo itakuwa ikijiendesha yenyewe pasipo kumtegemea mtu mmoja Wakizungumza na Championi Jumamosi, Chambua na Jembe Ulaya walisema Rostam ametua Yanga kwa wakati muafaka hivyo sasa Yanga itapiga hatua kubwa zaidi kisoka.

 

“Rostam amekuja katika kipindi ambacho tunaamini kuwa atakuwa na msaada mkubwa kwa Yanga katika kuhakikisha inapiga hatua zaidi kiuchumi pasipo kumtegemea mtu mmoja au mfadhili. “Lakini pia mfumo wake wa kutaka kuiona Yanga ikiendelea kuwa chini ya wanachama kwa asilimia 100 utaisaidia kuifanya timu kuendelea kuwa karibu kabisa na wanachama wake kama ilivyo zamani.

 

“Kwa hiyo mpaka anafikia hatua ya kusema hivyo na kuhaidi kuwa yupo tayari kwa hali na mali kuisaidia Yanga ili iweze kuwa katika mfumo bora wa kujiendesha yenyewe kuna jambo ameliona, binafsi namuunga mkono katika hilo na ninamkaribisha Yanga kwa ajili ya kuwa mdhamini na siyo mfadhili wala mmiliki,” alisema Malima. Naye nahodha wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema: “Mfumo ambao Rostam amekuja nao ni mzuri. Pia utapunguza migogoro kama ambayo hivi sasa tumekuwa tukiisikia huko upande wa pili.”

 

“Kikubwa inatakiwa tu
kufanyike marekebisho ya katiba yetu na kuweka vifungu ambavyo vitatusaidia katika kuhakikisha mipango hiyo ya Rostam ya kuruhusu wadhamini wengi kuja kudhamini timu yetu inatekelezeka bila ya kuwepo kwa vikwazo vyovyote.”

 

MZEE AKILIMALI AMSAPOTI ROSTAM Naye Mzee Ibrahim Akilimali ‘Mzee Akilimali’ ambaye ni Katibu Baraza la Wazee wa Yanga, ameunga mkono hoja ya Rostam na kusema Yanga haiwezi kumilikiwa na mtu mmoja.

 

“Kwa kweli mimi nimefurahishwa na kauli ya Rostam na ninamkubali sana kwani klabu kubwa kama Yanga ambayo ina wanachama wengi huwezi kuimilikisha na mtu mmoja kwani kufanya hivyo ina maana kila kitu atakuwa nacho yeye. “Mimi jana (juzi) nilimsikiliza mwenyewe na timu kama Yanga inatakiwa iongozwe na wanachama sasa kama mwanachama umeenda pale na kudhani kuwa kuna mdhamini uache kuchangia basi wewe hufahi kuwa mwanachama, mwanachama unatakiwa uchangie.”

Comments are closed.