The House of Favourite Newspapers

SAKATA LA DNA: Makonda Awataka Vigogo Hawa Wasimjaribu – VIDEO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, leo Jumamosi Aprili 14, 2018 amefunguka kuhusu oparesheni yake maalum ya kuwasaidia wanawake waliotelekezewa watoto na wazazi wenzao huku akiweka wazi kwamba jumla ya familia 290 zimepatana na sasa wanalea watoto wao vizuri.

 

“Kila kitu tunachokifanya kina interest (maslahi), jambo hili interest ya kwanza ni haki za mtoto ambaye anapaswa kupata elimu, afya, matunzo, malezi na mambo mengine ya muhimu anayopaswa kupewa. Haijalishi mtoto kazaliwa na house girl, mama kabakwa, au vyovyote, tunachokiangalia ni haki ya mtoto kwanza. Hatutetei ma-house girl au mabaamedi kuzaa na baba mwenye nyumba, tunatetea haki ya mtoto.

 

“Familia zaidi ya 290 zilizofika kwa mkuu wa mkoa, zingeenda mahakamni unadhani hizo kesi zingeisha lini? Nakumbuka mahakamani wangehitaji mawakili.  Mawakili siku hizi siyo huduma tena ni biashara, huyu mama maskini aliyetelekezewa mtoto wake angefanyaje?

“Wapo waliotelekezwa na wageni wakiwemo wa Zambia, Mozambique, China na Oman. Huyu Mchina nimeshawapa taarifa Ubalozi wa China na wameshatuma huko kwa ajili ya kufuatiliwa. Oman napo inaonekana kuna wazazi wengi sana wa kiume wametelekeza watoto wao hapa Tanzania.

 

“Kuwaficha watoto ndiyo kunasababisha matatizo kwenye misiba. Mtaani wanakoishi hawa watoto jamii inajua kwamba hawa ni watoto wa akina nani, wenye dhambi wanapenda mambo yao yabaki gizani, sisi hatujafanya kosa kuwaanika watoto kwani hakuna siri tena.

 

“Akina mama hawa ni wa kupongezwa, hawajatoa mimba, hawajatupa watoto, wamepambana mpaka sasa wanatafuta haki za watoto wao. Wenye matatizo ndiyo wanaendelea kuficha iwe siri. DNA itahusika endapo maelezo ya malalamikaji au mlalamikiwa yatakuwa hayajajitosheleza, hii itahitaji vipimo vya kitaalam ili kuondoa mashaka kuhusu nani mzazi halisi wa mtoto husika.

 

“Ninawapa pole wanaosema hawataitikia wito wa Ustawi wa Jamii ambayo iko chini yangu au kugoma kupima DNA wasinijaribu, wanajua naweza kuwaweka ndani muda wowote. Bahati nzuri wananifahamu, sifanyi jambo la kisiasa, watajua mimi ni mkuu wa mkoa au mtoto wao.

 

“Kwa wale ambao kipimo cha DNA kitaonesha wamesingiziwa (watoto si wa kwao), wanaweza kufungua kesi mahakamani kudai fidia kwa kudhalilishwa. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ustawi wa Jamii na wanasheria wangu tutakuwa mashahidi wake namba moja,” alisema Makonda.

Akizungumzia oparesheni na mikakati yake ambayo amekuwa akiianzisha na kuitekeleza katika mkoa huo ikiwemo ya walimu kupanda mabasi na treni bure ili kuwahi katika vituo vyao vya kazi, Makonda amesema:

 

“Wanaosema nimekurupuka kwenye hili zoezi huo ni mtazamo wao kwa sababu hatukuwashirikisha kuanzia siku ya kwanza. Sisi hatukurupuki, hii ni moja ya kazi zetu za kila siku, siwezi kufanya kazi mafichoni. Hawajaitwa mafichoni, wameitwa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

 

“Tuna mpango wa kuwa na mabasi 100 kwa ajili ya wanafunzi na walimu wa mkoa wa Dar es Salaam, lakini kuna wengine wanabeza na kudharau tunachokifanya, nawaasa Watanzania wanyanyuke na kusaidia jamii.

 

“Tunatengeneza utaratibu mpya wa kuwapelekea barua waajiri wa wazazi waliowatelekeza watoto wao, tunaangalia pia mchakato wa kupeleka mapendekezo ya sheria bungeni ili ofisa wa ustawi wa jamii aweze kumpeleka mahakamani moja kwa moja mzazi aliyemtelekeza mtoto,” amesema Makonda.

 

LIVE: MAKONDA AFUNGUKA A-Z ALIYOJIONEA ZOEZI LA WANAWAKE WALIOTELEKEZWA

Comments are closed.