The House of Favourite Newspapers

SAKATA LA KUTELEKEZA WATOTO, VIGOGO HAWA MATUMBO JOTO!

HII ni aibu ya karne! Mamia ya wanawake waliojitokeza juzi Jumatatu kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakidai kutelekezwa baada ya kuzalishwa na wanaume wao, wameibua mshtuko mkubwa na kuthibitisha kuwa tatizo hilo ni kubwa na lipo ‘seriaz’, Risasi Mchanganyiko lina ripoti kamili.

Mapema alfajiri, kundi la wanawake hao lilishuhudiwa likizingira geti la kuingilia ofisini kwa mkuu huyo wa mkoa iliyopo Ilala-Boma jijini Dar ambalo pia hutumiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.

 

“Tunawaomba mkae kule ng’ambo ya barabara hadi saa 2:30 asubuhi. Ndiyo muda wa kuanza kazi, lakini hapa getini mnazuia majukumu mengine na hasa usalama wa viongozi wetu wakifika,” alisikika mmoja wa walinzi getini hapo akiwazuia wanawake hao waliodamkia kwenye ofisi hizo.

Ulipofika muda wa kuanza kazi huku Makonda akiwa ameshawasili ofisini kwake, ndipo wanawake hao wakaruhusiwa kuingia ndani ya fensi ya eneo hilo ambapo palikuwa hapatoshi kutokana na wingi wao.Kilichofuata baada ya hapo ni vurugu

 

zilizosababishwa na kusukumana kwa wanawake hao huku kila mmoja akitaka kumuona Makonda ili amwelezee kisa chake cha kutelekezewa mtoto na wengine watoto kwa sababu wapo waliotelekezewa zaidi ya mtoto mmoja.Kufuatia hali hiyo, ilibidi walinzi wafunge mageti ili wahudumiwe kwanza waliokuwa ndani ambapo baadhi ya waliofungiwa nje walikuwa wakipaza sauti kuomba kumuona Makonda.

 

“Makonda naomba unisikilize baba… nilitelekezewa watoto wanne kwenye nyumba ya kupanga, nimekuwa ombaomba ili niwalee wanangu, nakuomba Makonda usikie kilio changu..,” alisikika mmoja wa wanawake hao akiwa amewabeba wanaye wawili wa kiume akichungulia kwenye ukuta wa fensi ya ofisi ya Makonda.

 

“Mimi nimelala hapahapa, hawa walioingia walifika alfajiri ya saa 10, lakini wao wamebahatika kuingia, mimi siondoki hapa hadi nimuone Makonda,” alisikika mama mwingine akiangua kilio. Baadaye wasaidizi wa Makonda walitoa utaratibu kuwa, wataanza na zoezi la kujiorodhesha ndipo watakapopangiwa vyumba maalum vya kusikilizwa.

Wakati zoezi la kuorodheshwa likiendelea ndipo wanawake wawili wakaibua gumzo la aina yake baada ya kudai kuzaa na mastaa wakubwa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

ALIYEDAI KUTELEKEZWA NA KIBA

Kwa upande wake, mwanamke aliyedai kutelekezwa na Kiba aliyejitambulisha kwa jina la Khadja Hassan naye alikuwa miongoni mwa wanawake hao akitaka Makonda amsaidie ili Kiba amsaidie kumlea mtoto wa kike aliyedai kutelekezewa na staa huyo.

 

…WA DIAMOND

Mwanamke mwingine ambaye amekuwa akilalamika na kuhangaika Ustawi wa Jamii, Pansheni Salama, raia wa Kenya alikuwa miongoni mwa wanawake hao ambaye naye aligeuka gumzo baada ya kusikika akisema kuwa, mwanaye wa kike amezaa na Diamond aliyemtelekeza.

 

…WA MCHUNGAJI MWANSASU

Selina ni mwanamke anayedai kuzaa watoto wawili na kutelekezwa na mwimbaji wa Injili na Mchungaji wa Kanisa la Hosana Life Mission, Ephraim Mwansasu ambaye naye aliungana na wenzake kudai kuwa haki itendeke kwani anateseka kulea mwenyewe.

 

JOYCE KIRIA AIBU YAKE

Katika hali ya kushangaza, Mtangazaji wa Kipindi cha Wanawake Live, Joyce Kiria, naye alikuwa miongoni mwa wanawake hao. Joyce anamtuhumu aliyekuwa mumewe, Henry Kileo kumtelekeza baada ya kumzalisha watoto wawili, jambo ambalo lilitafsiriwa kuwa ni kumuaibisha kigogo huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye ni katibu mkuu wa chama hicho wa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Joyce ndiye aliyerusha video ya tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii hadi alipomfikia Makonda na kumweleza kilio chake kuwa anahangaika kulea wanaye wawili baada ya kutelekezwa na Kileo.

Kufuatia tukio hilo ambalo hata wanawake wa mikoa mingine walitinga kufikisha vilio vyao, liliibua kihoro mitaa ya jijini Dar ambapo wake za watu walikuwa makini kufuatilia waume zao kama watatajwa kutelekeza watoto.

 

VIONGOZI WA DINI NA WANASIASA

Baadhi ya viongozi wa dini na wanasiasa viwembe walidaiwa kuwa presha juu, wakihofia kuwa huenda wakatajwa kwenye sakata hilo.Kutokana na wingi wa wanawake hao, baadhi ya walioorodheshwa walipewa fomu maalum za kujaza kuhusiana na wanaume waliozaa nao ambapo leo (Jumatano), watuhumiwa wataanza kuitwa kwa ajili ya kutoa maelezo.

 

NENO LA MAKONDA

Hivi karibuni, Makonda aliwatangazia wanawake wote waliotelekezwa na wanaume wao na hawapatiwi fedha za matunzo ya mtoto kufika ofisini kwake Siku ya Jumatatu ya Aprili 9, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa msaada wa kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Makonda, jopo la wataalam wa sheria, maafisa wa ustawi wa jamii na polisi wa Dawati la Jinsia, walijipanga ipasavyo kuwahudumia wanawake hao na kuhakikisha wazazi wenzao wanatoa fedha za matunzo ya watoto.

MTAALAM WA SAIKOLOJIA

Kutokana na kujitokeza kwa wingi wa wanawake hao, Mtaalam wa Saikolojia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki alisema kuwa, kinachoonekana tatizo ni kubwa mno kwani utafiti unaonesha kuwa, katika kila nyumba kumi, kuna wastani wa watoto wawili waliotelekezwa hasa vijijini.“Kuna shida kubwa, kuna tatizo la malezi, lisiposhughulikiwa, tuendako kunaweza kuwa kubaya zaidi,” alisema Dk Mauki.

 

MCHUNGAJI

“Ni kweli kama wengine wanavyosema ni aibu ya karne, kuna kitu hakipo sawa na sisi wachungaji na watu wa Mungu tunapaswa kufanya kazi ya ziada,” alisema Nabii James Nyakia ambaye ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda- Kinyantira jijini Dar ambako nako kuna tatizo hilo.

Stori: Waandishi Wetu, Dar.

Comments are closed.