The House of Favourite Newspapers

Sasa mtaijua Yanga, Yaifuata Mbeya City Kwa Ndege

Wachezaji wa timu ya Yanga wakiwa katika ndege wakienda Mbeya leo alfajiri wakitokea Dar es Salaam.

YANGA ina dakika ngumu 180 kuthibi­tisha kwamba hawakuwa wakibahati­sha kwenye mzunguko wa kwanza.

Timu hiyo itakayopata viongozi wapya kwenye uchaguzi mkuu wa Januari 13, kwa sasa inatamba kutokana na kutopoteza mchezo hata mmoja. Wamewaacha Simba nyuma kwa pointi 17.

 

Kikosi hicho cha Mwinyi Zahera hadi sasa kimecheza mechi 17 na kati ya hizo imeshinda 15 ikiwa imepata alama 47. Lakini kibarua kizito kinakuja kukamilisha mzunguko wa kwanza. ambapo ni ni dhidi ya Mbeya City na Azam FC.

Endapo Yanga itafanikiwa kushinda mechi hizo mbili, itakuwa imefikisha alama 53 na kuvuta pumzi kidogo kabla ya kuingia mzunguko wa pili.

 

Kitakwimu katika misimu ya hivi karibuni, Yanga imekuwa ikitamba dhidi ya Mbeya City ugenini lakini mechi na Azam huwa ni pasua-kichwa.

 

Mbeya City tangu ipande ligi kuu 2013/14 hadi sasa imewahi kuifunga Yanga mara moja katika uwanja huo msimu wa 2016/17 ambapo ilishinda 2-1 baada ya hapo matokeo yamekuwa ni sare na ushindi kwa upande wa Yanga.

 

Katika uwanja huo, Yanga imepata ushindi mara mbili na kutoa sare mara mbili uwanja wa Sokoine na inaenda kukutana na Mbeya City yenye njaa ambayo katika mechi zake 17 za msimu huu imepoteza tano na kushinda sita huku hadi sasa Yanga haijapoteza mechi yoyote.

Yanga ikiwa katika Uwanja wa ndege wa Songwe Mbeya, Tanzania.

Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na mabao 33 na Mbeya City mabao 20 huku timu zote vinara wao wa mabao wote, kila mmoja ana mabao tisa.

 

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesisitiza kwamba hawaachi kitu na hawaangalii wanakutana na nani na anaamini kuwa michezo hiyo watavuka salama hasa kutokana na kuongezeka kwa Haruna Moshi ‘Boban’ kikosini.

 

Ikimalizana na Mbeya City, inarudi Dar es Salaam kwa Azam FC ambao kwa sasa ndiyo wanachuana nao vikali katika usukani wa ligi ambao wote wawili hakuna ambaye anataka kupoteza rekodi yake.

 

Azam na Yanga wamekuwa wakitumia uwanja mmoja katika kucheza isipokuwa msimu uliopita kwa mara ya kwanza Yanga walicheza katika Uwanja wa Azam Complex.

 

Kikosi hicho kinanolewa na Mholanzi, Hans van der Pluijm, ambaye tayari amenukuliwa akisema: “Nataka kumaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza ili niwe na rekodi bora zaidi kwa timu za Simba na Yanga ambazo bado sijakutana nazo.”

Kuanzia msimu wa 2013/14 hadi sasa timu hizo zimekutana mara 10 katika uwanja mmoja isipokua mechi moja na Yanga imeshinda mara mbili tu na kutoa sare mara 5 huku ikipoteza mara tatu.

Na msimu huu mechi ambazo watakutana Yanga na Azam zitaendelea kupigwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Azam haijapoteza mechi hadi sasa msimu huu. Chagizo la mechi dhidi ya Azam ni ingizo la Obrey Chirwa na Donald Ngoma ndani ya Azam ambao ni wachezaji wa zamani wa Yanga.

STORI NA MARTHA MBOMA | SPOTI XTRA

Comments are closed.