The House of Favourite Newspapers

Serikali Yavamia Instagram, Wenye Kurasa Tata Kukiona Cha Moto

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza.

Kimenuka! Ndivyo unavy­oweza kusema baada ya serikali kuamua kulivalia njuga suala la maadili kwa kuhakikisha, kila anayeposti picha kwenye mtandao wa Instagram na mingineyo, zinakuwa na maadili.

 

Kutokana na mwamko huo wa serikali, sasa hivi mastaa matumbo joto kwani wameonekana kuogopa kuposti picha zao zilizokuwa zikikiuka maadili huku wengine wakiamua kujitoa kabisa kwenye mitandao ya kijamii.

Gigy Money

Awali, tamko la kuvalia njunga suala la maadili lilianza kutolewa na Rais Dk John Pombe Magufuli alipokuwa mjini Dodoma kwenye Mkutano wa Jumui­ya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mwishoni mwa mwaka jana.

 

Rais Magufuli alivitaka vy­ombo vinavyohusika kuhak­ikisha vinasimamia maadili hususan kwa wanawake ambao wamekuwa waki­jianika nusu utupu kwenye mitandao ya kijamii na video za nyimbo mbalimbali.

 

Akizungumza na Amani juzi, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alisema, tayari ameshatan­gaza kuwa yeyote atakaye­posti picha isiyokuwa na maadili kwenye mitandao ya kijamii, atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

                                        Jane Rimoy ‘Sanchi’.

“Nimeshatoa tamko tangu Desemba mwaka jana hivyo tunafuatilia kuanzia hapo, kama mtu aliposti humo Instagram na kwingineko kabla ya tamko langu hatutamshughulikia lakini kwa wale walioposti baada ya mimi kutamka, lazima watakumbana na mkono wa sheria,” alisema Shonza na kuongeza:

 

“Tunafahamu kurasa zao za mitandao hiyo hivyo tuta­washughulikia mmoja baada ya mwingine, lakini haya yote tunafanya kwa ajili ya kuifanya jamii yetu iwe na maadili na si vinginevyo.”

Alisema, kuonesha kwamba anachozungumza wanamaanisha, Januari 7 mwaka huu, alimfungia msanii Suzan Michael maarufu kama Pretty Kind kujihusisha na sanaa kwa muda wa miezi sita na kutoposti picha yoyote mtandaoni kwa miezi hiyo, kutokana na msanii huyo kutoa wimbo uitwao Viduduwasha usio na maadili pamoja na kuposti picha ya nusu utupu mtandaoni, huku akiwaita mastaa wengine kufika katika ofisi yake.

 

Mastaa hao walioitwa katika ofisi yake ni wale ambao wanaosifika kwa kuposti picha za utupu katika mtandao wa Instagram, Gift Stanford maarufu kama Gigy Money na Jane Rimoy ‘Sanchi’.

Gigy alitii agizo hilo Januari 8, mwaka huu kwa kufika katika ofisi za Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kutii wito huo.

 

Alipoulizwa kama zoezi hilo linawahusu mas­taa peke yake, waziri Shonza alisema kwa sasa wameanza na watu hao maarufu lakini panga hilo litawaangukia pia watu wengine muda wowote.

Akizungumzia hali hiyo, msanii wa sinema za Kibongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ alisema, anam­pongeza waziri huyo kwa hatua hizo anazochukua kwani kwa sasa, wasanii wamenyooka tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

“Sasa hivi mambo ni moto. Watu wamenyooka na wengine wanaendelea kunyooka. Hali ilikuwa mbaya sana huko nyuma. Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kusimamia maadili na tunaona sasa kumbe inawezekana,” alisema Dude.

Stori: Waandishi Wetu, Amani

Comments are closed.