Siku 28 tu, Amunike Atimuliwa El Makkasa ya Misri
Klabu ya El Makkasa ya nchini Misri imemfuta kazi aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Amunike kutokana na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.
Amunike aliyewahi kuwa Kocha wa taifa Stars, alijiunga na El Makkasa Februari 2, 2020, na katika mechi zake zote alizoingoza klabu hiyo kama kocha mkuu hajashinda hata mchezo mmoja.
“Tumemteua Ehab Galal kuwa Kocha Mkuu wetu kwa sasa ambaye ataanza kukinoa kikosi kuanzia Jumatatu (leo) kujiandaa na mchezo dhidi ya Aswan, Ligi Kuu ya Misri. Amunike atabaki kuwa Mkurugenzi wa Academy zetu ambazo tumezianzisha ikiwemo moja ambayo imezinduliwa hivi karibuni nchini Tanzania,” umesema uongozi wa El Makkasa.
Amunike ameiongoza El-Makkasa katika michezo mitatu tangu ajiunge nao, dhidi ya Smouha na Al Entag Al Harbi ambazo zote alitoa sare ya 1-1 huku akifungwa bao 0-1 na Tala’ea El Gaish kwenye Ligi Kuu ya Misri. El-Makkasa inapambana ijinusuru kushuka daraja ikiwa nafasi ya 16 na pointi 14.


