The House of Favourite Newspapers

Simba Malizieni Kazi Uwanja wa Taifa Leo

Kikosi cha timu ya Simba.

HII ni wikiendi ya kimataifa, Yanga tayari amecheza jana Jumamosi dhidi ya St Louis ya Shelisheli kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya awali.

 

Ilikuwa ni mechi kali ambayo Yanga walipambana kuonyesha uwezo wao na bado wana nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi ni Wydad Casablanca ya Morocco.

 

Simba wao wanaingia uwanjani leo kuikabili Gendemarie ya Djibouti katika Kombe la Shirikisho, mechi hii ni muhimu kwa Simba ambayo mashabiki wao hawajaiona kwenye michuano ya kimataifa tangu mwaka 2012.

 

Simba ilikuwa kwenye kipindi cha mpito ambapo ilikuwa ikihaha kusaka tiketi hiyo huku Azam na Yanga zikimiliki nafasi hizo kwa kipindi hicho.

Mchezo wa muhimu kwani katika mashindano hayo kila timu hujidhatiti ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kujitahidi kutengeneza matokeo mbele ya mashabiki wake.

 

Timu nyingi zimekuwa zikitumia faida ya nyumbani kutokana na figisu ambazo zimekuwa zikitokea mara nyingi ugenini, kwani kila mmoja anataka kufanya vizuri kwenye mashindano hayo yenye faida nyingi.

 

Miongoni mwa faida za michuano hiyo kwanza ni klabu kujijengea hadhi kimataifa, kujisogeza karibu na wadau wakubwa kibiashara, kutangaza na kuuza wachezaji pamoja na kujitengenezea utajiri kupitia zawadi mbalimbali ambazo zipo kwenye kila hatua kuanzia makundi.

 

Hivyo ni muhimu kwa Simba na Yanga kupambana kwa kila hali kuonyesha uwezo na umahiri wao katika eneo hilo kwani wamekuwa kwenye soka kwa miaka mingi sasa.

 

Huu ni wakati wa timu zote mbili kutumia vizuri faida ya uwanja wa nyumbani kutengeneza matokeo mazuri kwa kutegemea kwamba lolote lile linaweza kutokea ugenini kwa vile timu zote zilizofuzu zina vigezo na ubora stahiki.

 

Maoni yetu ni kwamba timu zetu zionyeshe uzalendo zipambane na ifike mahali tabia ya kuzomeana au kusapoti timu za wenzetu iishe. Hii zomeazomea haisaidii kujijenga inawaharibu wachezaji kisaikolojia na mwisho wa siku timu ikiondolewa ni hasara kwa Taifa.

 

Timu zetu zote zikifuzu kwenye hatua ya makundi kwa mfumo wa mashindano hayo ulivyo sasa inamaanisha zitakuwa bize kimataifa mpaka mwezi Septemba kwavile zitacheza kwa mfumo wa ligi.

 

Zikifuzu zote itasaidia kuziimarisha zaidi hata kiuchezaji na kimiundombinu, kwavile zitapata fedha nyingi na zitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusajili wachezaji wa maana zaidi.

Simba na Yanga zimecheza sana kwenye ligi ya ndani, huu ni wakati wa kufanya vizuri kimataifa kuionyesha dunia kwamba wao ndio wakongwe na wajuaji kwenye soka la Tanzania.

Tunawasihi wajiwekee mikakati imara ya kupambana mchezo mmoja baada ya mwingine, wasishike mambo mengi kwa wakati mmoja yatawaelemea. Wakishapita hii hatua ya awali, waanze mkakati wa mechi ijayo ya raundi ya kwanza. Hivyo ndivyo zinavyofanya klabu nyingi zilizoendelea hususani Arabuni.

Lakini yote kwa yote ushirikiano wa sekta zote ni muhimu kwani klabu peke yake hazitaweza, shirikisho, serikali na wadau watoe sapoti stahiki.

Comments are closed.