The House of Favourite Newspapers

Simba SC Kumfanyia Sapraizi JPM Taifa

Emmanuel Okwi

STRAIKA namba moja nchini, Emmanuel Okwi, ameandaa sapraizi ambayo ni zawadi maalum ya mabao atakayomkabidhi leo Jumamosi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kwenye Uwanja wa Taifa, Simba itakapocheza na Kagera Sugar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Okwi amesema kwamba wachezaji wote wamejipanga na mechi ya leo itakuwa ya aina yake. Mchezo huo utakaoanza saa 8:15 mchana, Simba itakabidhiwa kombe lao wanalobeba kwa mara nyingine baada ya kulikosa miaka mitano na mgeni rasmi ni Rais Magufuli ambaye atasindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mohammed Dewji ‘Mo’.

Simba imeweka rekodi ya kubeba kombe hilo bila kupoteza mchezo, ambapo leo kiingilio cha chini kimefanywa Sh 2000 ili mashabiki kibao waingie kuishangilia timu yao.

 

Okwi anayeongoza kwa mabao 20, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, mechi ya leo ina umuhimu mkubwa na amepata taarifa kuwa Rais Magufuli hajawahi kuhudhuria katika mechi uwanjani hapo miaka ya hivi karibuni hivyo amepanga kumkaribisha kwa kumpa zawadi ya kufunga mabao zaidi ya mawili ili avunje rekodi ya Amissi Tambwe aliyoiweka msimu wa 2015/16 ya kufunga mabao 21 akiwa na Yanga.

Okwi alisema amepanga kuhakikisha yeye na wenzake wanacheza kwa nguvu ili wasifungwe kwenye mchezo huo na kulinda heshima yao ya kutofungwa mpaka sasa.

 

“Itakuwa muhimu sana kwa kuwa nimesikia Rais Magufuli hajawahi kukanyaga uwanjani hapa kwenye matukio ya kimichezo hivyo kama timu tumemuandalia zawadi kubwa ikiwemo ya mimi kufunga mabao zaidi ya mawili.

 

“Lakini pia pamoja na hiyo zawadi pia tutamfanya aendelee kutuamini ili siku nyingine ikitokea tumemualika asikatae kuja uwanjani lakini kubwa mchezo huu unachagiza na yeye kuwepo uwanjani hivyo kama timu hatutamuangusha,” alisema Okwi ambaye ni raia wa Uganda aliyewahi kuichezea Yanga.

 

Baada ya shamrashamra za Uwanja wa Taifa, Simba watakwenda kujirusha wakifurahia kwenye viwanja mbalimbali ambapo habari ambazo Championi lina uhakika nazo ni kwamba kombe atakalokabidhiwa Mnyama leo gharama yake ni zaidi ya Sh10milioni.

 

Gharama hizo zinalifanya kombe hilo kuwa la kipekee ambapo, habari za ndani zinasema kuwa Simba wamelikomalia kuhakikisha kwamba wadhamini na TFF wanatoa kitu kikali chenye hadhi yao kwani walilikosa kwa miaka mingi.

STORI MUSA MATEJA | CHAMPIONI JUMAMOSI

Comments are closed.