The House of Favourite Newspapers

Simba Yamzuia Asante Kwasi Kwenda Polisi

Beki mpya wa Simba Mghana, Asante Kwasi (kulia).

SIMBA ni kama wameshtukia kitu vile, ni baada ya mabosi wa timu hiyo kumzuia beki wao mpya Mghana, Asante Kwasi kufanya mazoezi ya pamoja na timu hiyo kwenye Uwanja wa Polisi Dar. Awali, kulikuwepo na taarifa za beki huyo kuanza mazoezi juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam chini ya Kocha Mkuu Mcameroon, Joseph Omog, lakini hadi jana beki huyo alikuwa hajaonekana.

 

Beki huyo, alijiunga na Simba hivi karibuni katika usajili wa dirisha dogo la usajili akitokea Lipuli FC ya Iringa huku ikidaiwa kuwa bado ana mkataba wa miezi saba ya kuichezea timu hiyo.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, beki huyo amezuiliwa kuanza programu ya mazoezi ya timu hiyo hadi pale suala la usajili litakapomalizika kwa pande zote mbili, yaani Simba na Lipuli kwa kufikia muafaka wa usajili wao.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, suala hilo limefikia pazuri na wakati wowote watafikia muafaka na Lipuli na haraka ataanza mazoezi na wenzake. “Kisheria Kwasi hawezi kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake ikiwa suala lake bado halijafikia muafaka mzuri katika usajili wake wa kutoka Lipuli kuja kuichezea Simba licha ya kumsainisha.

 

“Kama unavyofahamu suala lake la usajili lilikuwa gumu, kwani timu yake inayommiliki kusema kuwa ana mkataba wa miezi saba, hivyo ni lazima tulimalize kwa amani, hatuwezi kumruhusu kwenda Polisi kufanya mazoezi na wenzake hadi ishu yake ikamalike,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally kuthibitisha hilo, alisema: “Ni kweli Kwasi hajaanza mazoezi kama watu wanavyosema, kwa kifupi amezuliwa kuanza mazoezi hadi pale suala la usajili litakapomalizika. “Kama unavyofahamu usajili ni taratibu zote zifanyike zitakazomruhusu kwenda kuichezea timu nyingine, hivyo basi sisi viongozi tumemzuia kuanza mazoezi hadi utata wake utakapomalizika.”

Comments are closed.