The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya AY: Baba yake afariki akiwa hajamuona kwa miaka 7

0

Ambwene Yesaya (2)Alhamisi iliyopita tuliishia pale AY aliposimulia kuhusu Kundi la ECT kutokuwa na nyimbo zake na kuongeza kuwa nyimbo walizokuwa wakizitoa ni za msanii King Crazy GK. Endelea naye kufahamu ni kwa nini?

“Kama kundi hatukuwa tunaangalia ishu ya kuwa na nyimbo zetu zaidi ya kuujenga ushirikiano wetu. ECT ilikuwa kama vile unavyoona umoja wa Afrika ambao una nchi nyingi ndani yake ila kila nchi inatumia pesa yake. Ndivyo ilivyokuwa kwa ECT.

“Tuliendelea na ECT kama kawa ila baadaye tukashindwana kibiashara, kuna mtindo f’lan wa biashara ambao sisi (AY na F.A) tulikuwa tunautaka kwa hiyo ikawa ni ngumu kwa ECT kukubaliana basi ikabidi tujiengue na wala hatukugombana kwa vitu vingine, ila undugu na urafiki wetu bado uko palepale hata jana (Ijumaa ya wiki iliyopita) nilikuwa nazungumza na GK ila F.A, tunawasiliana mara nyingi kwa sababu ya mtindo wetu wa kazi kufanana kwa mengi.

“Nashangaa watu wanaosema simfanyii mpango wa kolabo na mastaa wa nje, kiukweli hata yeye hushangaa kwa sababu watu hawafahamu ni namna gani tunashirikiana katika kazi zetu.

“Huwezi amini mimi (AY) na F.A haipiti siku bila kuzungumza na kama itatokea basi ni mara moja moja inategemeana na majukumu ya kazi na yeye hawezi kurekodi wimbo wake wowote bila mimi kuusikiliza, kuchangia mawazo au kuboresha chochote kile katika wimbo husika.

“Hata kama nitakuwa nimesafiri atanisubiri, vivyo hivyo kwangu, siwezi kurekodi wimbo iwe audio au video bila kumshirikisha na wakati mwingine kwenye nyimbo hizo huwa tunachombeza vineno vya mbali ambavyo mtu kuvifahamu unahitaji umakini zaidi.

“Niliendelea na haso za hapa na pale mwaka 2003 baba yangu mzazi alifariki dunia, kiukweli kama nilivyotangulia kusema toleo la nyuma kuwa sikulelewa na wazazi wote wawili zaidi ya mama yangu, kwa hiyo hata wakati baba yangu anafariki dunia nilikuwa sijaonana naye miaka 7 nyuma.

“Nilipopata taarifa nilikuwa niko Mwanza kwenye shoo ila nikajitahidi kupanda ndege ili niwahi mazishi ya mzee ikashindikana kwani nilipofika Dar nikakuta msafara umeshaondoka kuelekea Mbeya, nikakodi teksi kuufukuzia ule msafara lakini sikuupata ikabidi nighairi na kwenda siku nyingine, kwa kifupi sikumzika baba yangu mzazi.

“Baadaye nilifanya Wimbo wa Machoni Kama Watu nikiwa nimemshirikisha Stara Thomas , nakumbuka kipindi hicho nilimsikilizisha wimbo huo marehemu Saimon Sayi ‘Complex’ akakubali staili yangu na tukakubaliana tufanye remix ya Wimbo wa Raha Tu kupitia Studio ya Backyard ambapo Complex alikuwa akifanya kazi kama mtayarishaji wa muziki.

“Kipindi hicho Backyard kulikuwa na mtayarishaji mwingine mkali akifahamika kwa jina la Cossu huku madj wakali waliotikisa miaka hiyo walikuwa kina Bon Love, Venture na wengine wengi, kiukweli watu hao wamechangia sana mimi kufika hapa nilipo nawakumbuka na kuwapenda sana kila siku.

“Miongoni mwa matukio ambayo ni ngumu kuyasahau ni pamoja na la mwaka 2008, nilipopata pigo jingine bada ya kufiwa na mama yangu mzazi ambaye ndiye alikuwa mlezi wetu, maana sisi tuko watoto wanne na mimi ni mtoto wa tatu kuzaliwa. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana ila ninachokumbuka siku mbili kabla ya kifo cha marehemu mama alikuwa haachi kutuchekesha wanawe, naamini alikuwa anafanya hivyo ili kutuondoa wasiwasi kwani alifahamu dhahiri ataiaga dunia muda si mrefu.

“Inauma, inasononesha sana kama mtoto kuondokewa na mtu uliyempenda, uliyemtegemea kwa ushauri na mambo mengine ni maumivu makali sana kuishi bila wazazi ila hatuna budi kukubaliana na kila jambo kwani kila mwanadamu ataonja umauti, sote tu wapitaji, kwa hiyo nilikubaliana na kifo cha mama na kuamua kuendelea na maisha kama kawaida huku nikiendelea kumuombea huko aliko.”

Tukutane tena wiki ijayo katika gazeti hilihili katika simulizi hii ya AY nzuri na ya kusisimua…

Leave A Reply