The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 13

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Nilimuelekeza na kweli muda mfupi baadaye tayari tulikuwa tukipita kwenye njia ya kuelekea nyumbani lakini safari hii tulikuwa tukienda kwenye mwendo wa taratibu kwa hiyo hata muungurumo ulikuwa wa chini. Safari iliishia nje ya nyumba yetu ambapo Bonta aliniambia kwamba natakiwa kuhakikisha ikifika saa sita, tunaianza safari ya kurejea Dar.

 

SASA ENDELEA…

 

Nilimshangaa sana. Yaani tumeondoka Dar usiku, halafu tunatakiwa kusafiri tena usiku huohuo kurudi Dar, kivipi? Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.

 

Yeye aliniambia kwamba haingii ndani na badala yake anaomba nimuoneshe sehemu kwenye baa ili awe anakunywa moja moto moja baridi. Nilimwambia nitajisikia vibaya sana kama hataingia kuwasalimu wazazi wangu, hasa baba yangu ambaye alikuwa hoi kitandani. Ilibidi akubali, akavua zile gloves zake, kofia kubwa aliyokuwa amevaa na koti kubwa sasa akawa na mwonekano wa kawaida ambapo tuliingia ndani.

 

Mshtuko walioupata ndugu zangu, ulikuwa mkubwa sana, kwanza kwa sababu niliondoka bila kuaga lakini pia muda ambao tuliingia haukuwa wa kupokea wageni, hasa kijijini kwetu. Ilikuwa ni tayari saa tatu kasoro za usiku.

 

Mama alinikimbilia na kunikumbatia, akawa ananitazama usoni huku akiwa ni kama haamini. Alikuwa na maswali mengi kuanzia mahali nilipokuwa kwa nini nimechubukachubuka usoni, huyo niliyekuwa naye ni nani na usiku huo tumetoka wapi lakini niliamua kumnyamazisha kwa kutoa burungutu la fedha na kumpa.

 

“Hizi ni kwa ajili ya kumnunulia baba dawa pamoja na kununua mahitaji mengine ya hapo nyumbani, nimepata kazi na natakiwa kwenda kuanza kesho asubuhi huko Dar. Tunaondoka usiku huuhuu nimekuja tu mara moja kuwaletea fedha,” nilimwambia mama asiwe na wasiwasi wowote na mimi, niko kwenye mikono salama na nitajitahidi kuwakumbuka mara kwa mara.

 

Nakumbuka mama alilia sana, sikujua analia nini lakini katika kilio chake alinishukuru saba kwa nilichokifanya kwa sababu fedha zilikuwa zikihitajika sana kipindi hicho kuliko wakati mwingine wowote na bahati nzuri, ndani ya muda mfupi tu nilikuwa nimeweza kwenda kuzitafuta na kuzipeleka.

 

Japokuwa hakusema lakini nilimuoa mama alivyokuwa akijivunia kuwa na kijana mimi, alinichukua na kwenda naye mpaka chumbani alikokuwa amelala baba, nilipiga magoti na kumuombea kwani baba hakuwa na uwezo wa kutambua chochote kilichokuwa kinaendelea. Hakumjua mtu aliyekuwa akiingia wala aliyekuwa anatoka.

 

Nilipata uchungu sana ndani ya moyo wangu na nilijiapiza kwamba nitafanya kila kinachowezekana kuhakikisha namsaidia baba, kwa muda woye huo, Bonta alikuwa amekaa sebuleni akiwa na ndugu zangu wengene wakipiga stori za hapa na pale, akiwasimulia kilichokuwa kinaendelea jijini Dar es Salaam na wao wakimpa stori za hapa na pale kuhusu kilichokuwa kinaendelea pale kijijini.

 

Nilitoka na kwenda kumchukua Bonta, tukaingia chumbani alikokuwa amelala baba ambapo naye alipiga magoti na kumuombea kwa Mungu kwa imani yake kisha akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi na kumpa mama kwa ajili ya kusaidia vitu vidogovidogo katika kumuuguza baba.

 

Japokuwa mwenyewe alikiona kitendo hicho kama kidogo na cha kawaida lakini ndani ya moyo wangu kilinifanya nijisikie tofauti sana. Kiukweli kuanzia muda huo, nilimuona Bonta kuwa zaidi ya ndugu kwangu. Ni yeye ndiye aliyenipokea kwa mara ya kwanza katika mazingira magumu sana ambayo alinikuta nikiwa kwenye ugomvi mkubwa na kondakta wa daladala.

 

Lakini ni yeye pia ndiye aliyenikutanisha na bosi na sasa ni yeye ndiye aliyekuwa akiongea nami wakati tukimtazama baba ambaye ama kwa hakika hali yake ilikuwa mbaya sana. Tulitoka chumbani na kwenda sebuleni ambapo mama aliagiza tuandaliwe chakula. Tulikula na baadaye tuliendelea na stori za hapa na pale, ilipofika majira ya kama saa sita kasoro, tuliaga kwamba tunaondoka, kila mtu akatushangaa.

 

“Mnaondokaje usiku namna hii?”

 

“Tuna usafiri wetu mama, isitoshe kama nilivyosema kesho ndiyo siku yangu ya kuanza kazi kwa hiyo hatuwezi kulala huku,” nilimwambia, akawa mgumu sana kukubali lakini ushawishi wa Bonta ulimfanya aamini kwamba nitakuwa kwenye mikono salama.

 

Basi tulitoka na safari ya kurejea jijini Dar es Salaam ilianza. Kama ilivyokuwa wakati tunakuja, Bonta alikuwa akiendesha pikipiki kwa fujo, yaani usipoinama, ule upepo unavyopiga unajikuta uso wote ukiwa umejawa na machozi. Hakuwa anajali mashimo wala mawe na uzuri ni kwamba pikipiki ilikuwa na nguvu, kwa hiyo akawa anafukia tu.

 

Saa sita kama na dakika arobaini hivi, tayari tulikuwa tumeshafika Gongo la Mboto, mimi mwenyewe sikuamini, Bonta akazidi kuichochea pikipiki yake na muda si mrefu tayari tulikuwa tumewasili Kipawa. Mpaka nashuka kwenye pikipiki na kuingia ndani kwake kulala, miguu yote ilikuwa ikitetemeka huku masikioni nikiwa nasikia mvumo wa sauti ya pikipiki.

 

Nilifika kwenye sofa na kujibwaga, Bonta akafungua friji na kutoa chupa ya pombe kali, akapiga funda moja na kunimiminia glasi moja, akanipa na kuniambia kwamba nipige funda moja nitajisikia vizuri ndani ya moyo wangu na kupunguza uchovu, jambo ambalo kweli nililifanya.

 

Japokuwa nilikunja uso kutokana na ukali wa pombe hiyo, lakini ndani ya moyo wangu nilijisikia poa kabisa kwa sababu ule uchovu wote uliyeyuka. Bonta akaingia chumbani na alipotoka, aliniambia mimi nilale yeye anatoka kidogo, akanielekeza kufunga milango yote, akaondoka na pikipiki yake.

 

Niliporudi kule chumbani, kitu cha kwanza ilikuwa ni kukagua kama ile bunduki ipo palepale lakini cha ajabu ni kwamba haikuwepo. Kwa tafsiri nyepesi ni kwamba Bonta alikuwa ameichukua, sasa amekwenda nayo wapi usiku wote huo? Sikuwa na majibu.

 

Nilipanda kitandani na kujilaza huku mawazo mengi yakipita ndani ya kichwa changu kwa kasi. Ndani ya kipindi kifupi tu, mambo mengi yalikuwa yametokea kwenye maisha yangu kiasi cha wakati mwingine nijihisi kama nipo kwenye ndoto.

 

Haukupita muda mrefu, nikapitiwa na usingizi mzito uliosababishwa na uchovu mkali niliokuwa nao. Hata sikujua Bonta amerudi saa ngapi lakini nilipokuja kuzinduka, ilikuwa tayari kumeshapambazuka na Bonta alikuwa amelala pembeni yangu, akikoroma kuonesha kwamba naye amechoka sana.

 

Niliamka kwa kunyata kwani sikutaka kumuamsha, kitu cha kwanza nikainama pale anapoihifadhi ile bunduki yake na kuigusa. Ilikuwepo mahali pake lakini safari hii ilikuwa na kama harufu ya baruti hivi. Sikuelewa hiyo maana yake ni nini.

 

Nilitoka na kwenda sebuleni, nikafunua mapazia na kuanza kufanya usafi, ikiwa ni pamoja na kuandaa kifungua kinywa kwani Bonta jana yake alishanipa maelekezo yote kwa hiyo ugeni ulishaanza kupungua. Baada ya hapo, nilienda kuoga na kukaa sebuleni, nikawasha runinga kubwa ya kisasa iliyokuwa ukutani.

 

Muda mfupi baadaye, Bonta aliamka na kitu cha kwanza alichokifanya ilikuwa ni kwenda kwenye friji, akatoa chupa ya pombe kali na kumimina kwenye glasi, akapiga mafunda kadhaa na alipoishusha glasi, ilikuwa tupu.

 

Akajinyoosha pale kisha akaelekea bafuni kuoga. Ndani ya dakika chache tu, tayari alikuwa ameshaoga na kubadilisha nguo, akaja pale mezani, tukajumuika kwenye kifungua kinywa.

 

Baada ya kupata kifungua kinywa, tuliondoka pamoja kwa kutumia pikipiki yake na kwenda mpaka kule kazini, ambapo kulikuwa na umbali kidogo. Kama nilivyoeleza, eneo zima lilikuwa limezungushiwa ukuta mrefu na mpaka ufike ndani kabisa, ilikuwa ni lazima upite kwenye mageti mawili, lile la nje kabisa na linalofuatia.

 

Bonta aliingiza pikipiki yake mpaka ndani, tukateremka na kuanza kutembea kuelekea ndani huku akisalimiana na watu wengine wengi waliokuwa wakiendelea na shughuli za hapa na pale ndani ya eneo hilo ambalo lilikuwa bize kama gereji, karakana au kiwanda fulani.

 

“Nisubiri hapo,” alisema Bonta, nikasogea pembeni kwenye kundi la vijana wakubwa waliokuwa wakifanya mazoezi ya kunyanyua vyuma. Kila mmoja alikuwa na mwili mkubwa, kifua kipana na mikono iliyojazia kuonesha wameiva kimazoezi kisawasawa.

 

Walikuwa wakinitazama kwa macho ya chinichini huku wakiendelea na mazoezi yao, na mimi nikawa nawatazama tu. Upande wa pili kulikuwa na kundi lingine la watu waliokuwa wakifanya mazoezi ambao wao walikuwa ni kama wanacheza ‘karate’, huku wakifundishwa na kiongozi wao.

 

Kundi jingine la watu, lilikuwa bize kufanya usafi na kuhakikisha mazingira ya humo ndani yanakuwa safi, wengine wakawa wanafagia huku wengine wakimwagilia maua. Dakika chache baadaye, Bonta alirejea na kuniambia kwamba ameenda kuonana na bosi na amefurahi kusikia kwamba tumerudi na umeripoti kazini asubuhi hiyo.

 

“Amesema wewe itabidi ujifunze ufundi makenika, ameniambia nikuunganishe na mafunzi gereji wengine ili uanze kupata uzoefu,” aliniambia huku tukitembea kuelekea upande wa pili wa eneo hilo.

 

Moyoni nilifurahi sana kwa sababu sasa nilikuwa na uhakika kwamba nitakuwa na kazi ambayo itanisaidia sana maishani mwangu, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wazazi wangu, hususani baba yangu ambaye sasa alikuwa na hali mbaya sana kitandani.

 

Kweli Bonta alinipeleka kwenye gereji kubwa iliyokuwa ndani ya jengo hilo na kunikabidhi kwa mzee mmoja wa Kidigo, Shekwavi ambaye aliniambia kwamba ndiyo fundi mkuu. Mzee huyo alinipokea vizuri huku mara kwa mara akiniuliza kama kweli nitaweza kazi.

 

“Nakuona kama upo legelege sana, na hii kazi inahitaji wanaume na siyo wavulana,” aliniambia kwa kejeli, kauli yake hiyo ikauchoma mno moyo wangu. Ni kweli kwa mwonekano wa nje mtu angeweza kuamini kwamba mimi ni legelege lakini ukweli nilikuwa naujua mwenyewe kwamba mimi ni mwanaume wa shoka.

 

“Unamuona legelege huyu! Ohoo, muangalie hivyohivyo,” alisema Bonta ambaye alikuwa akizunguka huku na kule akiendelea na kazi ya kukagua kama kazi zilikuwa zikifanyika vizuri.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply