The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 15

0

MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

ILIPOISHIA:

Nilichukua mfuko na kuuweka vizuri, nikafungua zipu na kuingia nao ndani ya lile gari ambalo lilikuwa likinuka damu, tena damu mbichi. Nilishindwa kumtazama yule mtu kwa jinsi alivyokuwa amefumuliwa kichwa kwa risasi, nikamvalisha ule mfuko huku nikiwa makini nisichafue nguo zangu na damu.

 

SASA ENDELEA…

Mwanamke mwenyewe alionesha kuwa mtu wa makamo ya kati, uzuri ni kwamba hakuwa mnene sana kwa hiyo niliweza kumudu kumtoa pale alipokuwa, nikiwa tayari nimeshamvalisha karibu nusu nzima kwenye ule mfuko, kuanzia kichwani mpaka maeneo ya kiunoni.

 

Huku nikitetemeka, nilitegua siti na kumalizia kumuingiza miguu kwenye ule mfuko, nikaufunga na kuanza kuuvuta kuutoa nje ya gari. Kwa kuwa tayari mwili wote ulikuwa ndani ya ule mfuko, kwa mtu anayetazama kwa mbali angeweza kudhani labda natoa mzigo kwenye gari.

 

Niliushusha mpaka chini na kuuburuza mpaka pembeni, nikaenda kuchukua lile toroli na kulisogeza huku nikitetemeka mno. Niliunyanyua ule mzigo kwa nguvu zangu zote na kufanikiwa kuuweka juu ya lile toroli. Jasho jingi likawa linanichuruzika mwili mzima.

 

Nikiwa bado sijui nini cha kufanya, nilishtukia sauti kali ya mtoto akilia kutoka ndani ya lile gari, nikarudi harakaharaka na kufungua mlango wa nyuma, alikuwa akilia akiwa bado palepale kwenye kile kiti chake.

 

Moyo uliniuma sana kwa sababu nilijua kabisa malaika huyu wa Mungu hana hatia yoyote na mbaya zaidi ni kwamba asingeweza kumuona tena mama yake hapa duniani.

 

Nilishindwa kuyazuia machozi yasiulowanishe uso wangu. Nikabaki namtazama huku nikiwa hata sijui nifanye nini, machozi yakiendelea kunimwagika kwa wingi. Mara nilishuhudia wanaume wawili waliokuwa wamevalia maovaroli, wakija na kuchukua lile toroli, wakawa wanalisukuma kuelekea upande wa pili.

 

Sura zao zilikuwa ngeni kabisa kwangu, wakawa wanasukuma toroli bila hata kugeuka nyuma. Mara Bonta naye alikuja na safari hii hakuwa peke yake, alikuwa na wanaume wengine wawili ambao nao sura zao zilikuwa ngeni kwangu. Bonta alikuwa katikati yao, wakanisogelea bila kusema kitu chochote.

 

Bila kuzungumza chochote, Bonta alinipa ishara kwamba nimtoe yule mtoto kwenye gari, nikafanya hivyo huku bado machozi yakiwa yananibubujika. Nilisimama mbele yao huku nikiwa nimemshika yule mtoto ambaye kwa kumkadiria alikuwa na kama miaka miwili, ambaye alikuwa akiendelea kulia huku akimuita mama yake.

 

Bonta alimpa ishara mmoja kati ya wale wanaume, nikamuona akifunua koti lake refu, katika hali ambayo sikuitegemea, nilimuona akichomoa bastola, akachomoa na kitu kama kibomba fulani kutoka kwenye mfuko wake mwingine, akawa anakifunga mbele ya mdomo wa bastola kisha akaikoki! Nikabaki nimehamaki nikiwa sijui nini kinachotaka kufanyika.

 

Nilishangaa yule mwanaume eti akinikabidhi mimi ile bastola, macho yakanitoka pima! Nikamtazama Bonta ambaye sasa hivi alikuwa amebadilika kabisa uso wake, macho yalikuwa mekundu mno.

 

“Shoot!” alisema, akimaanisha eti nimpige risasi yule mtoto, nikawa narudi nyuma huku nikitingisha kichwa, uso wangu ukiwa umejawa na wasiwasi usiomithilika. Nikiwa naendelea kurudi nyuma, nikiwa hata sijui nataka kufanya nini kwani yule mtoto alikuwa mikononi mwangu lakini pia bastola ilikuwa mkononi mwangu.

 

Bonta akanipa ishara nitazame upande wa juu, macho yangu yakatua kwa mwanaume aliyekuwa amesimama ghorofani, akiwa ameegamia mabomba ya kwenye ‘balcony’, akivuta sigara na kutoa moshi mwingi. Kwa ilivyoonesha, alikuwepo pale kwa muda mrefu, akifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea. Hakuwa mwingine bali bosi Mute.

 

“Huu ni mtihani wa mwisho kwako, bosi anataka kukupima kama una moyo wa kiume,” maneno aliyoniambia Bonta muda mfupi uliopita yalijirudia kichwani mwangu, nikamtazama Bonta kisha nikamtazama Bosi Mute kule ghorofani, nikawatazama na wale wanaume wengine wawili.

 

Niligeuka na kutazama huku na kule, kila mtu alikuwa ameacha kila alichokuwa anakifanya na kugeukia pale tulipokuwepo kutazama kilichokuwa kinaendelea. Japo Bonta alikuwa kimya lakini uso wake ni kama ulikuwa unasema ‘mbona unataka kuniangusha?’

 

Nikiwa bado sijui cha kufanya, nilishtukia wale wanaume wawili wamefyatuka kwa kasi ya upepo, mmoja akanipokonya yule mtoto ambaye bado alikuwa akilia na kumkalisha chini, akamuegamiza kwenye jiwe kubwa la zege, yule mwingine akanishika kwa nguvu na kunirudisha nyuma umbali wa hatua kadhaa.

 

“Unaishika hivi… kisha unavuta hiki kitufe ukiwa umelenga unapotaka kupiga, vuta pumzi na usizitoe mpaka usikie mlio au mtingishiko kuonesha risasi imetoka,” alisema Bonta ambaye naye alikuwa ameshanisogelea mwilini kabisa na kunishikisha vizuri ile bastola, akakichukua kidole changu kimoja na kukiingiza kwenye ‘trigger’ ya kufyatulia risasi. Kila kitu kilikuwa kikifanyika kwa kasi kubwa mno mpaka nikawa najihisi pengine nipo kwenye ndoto ya kutisha.

 

“Unatakiwa kufuata maelezo niliyokwambia, vinginevyo kinachoenda kutokea hapa kitakuwa kibaya sana kwenye maisha yako, hebu mtazame tena Bosi Mute,” alisema Bonta, nikageuza shingo na kumtazama kule juu, nikamuona akiwa ametoa bastola na kuielekeza pale tulipokuwepo, Bonta akawageukia wale vijana na kuwapa ishara, wote wakasogea pembeni kabisa.

 

“Unaweza! Unaweza kabisa, nitazame usoni,” aliniambia Bonta, nikageuka na kumtazama huku nikiendelea kulia, akanipa ishara fulani usoni ya kunitoa wasiwasi na kunihakikishia kwamba ninaweza, akaniambia nielekeze akili zangu pale kwenye tukio vinginevyo bosi Mute atanipiga mimi risasi kwa sababu hawezi kukubali nikatoka nje na kwenda kutoa siri, kwa hiyo sikuwa na cha kufanya zaidi ya kutekeleza nilichoambiwa.

 

Nilimtazama yule mtoto, bado alikuwa akilia sana huku na yeye akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake, kufumba na kufumbua, Bonta naye alikuwa ameshasogea hatua kadhaa na kuniacha nikiwa nimesimama palepale, bastola ikiwa mkononi mwangu na Mute naye akiwa ameshaunyoosha mkono wake weye bastola kunilenga mimi.

 

“Eeh Mungu wangu, wewe ndiyo unaojua ukweli wa moyo wangu, nisamehe kwa hii dhambi kubwa ninayoenda kuitenda,” nilisema huku nikilia kwa uchungu usiomithilika. Sikuwahi kudhani hata siku moja na mimi nitakuwa muuaji lakini mpaka hapo tulipokuwa tumefikia, nilitakiwa kuchagua jambo moja tu, kuwa muuaji au kuuawa!

Bonta akaanza kunihesabia: “Moja… mbili… ta…!”

 

Alipofikisha tatu, nilifumba macho na kuvuta kile kitufe cha kufyatulia risasi lakini cha ajabu, nilipofumbua macho nikiamini nitakuta maskini yule mtoto ameshasambaratishwa na ile risasi, nilishtuka kuona hakuna kilichotokea.

 

Niliisogeza ile bastola usoni na kuitazama vizuri nikihisi pengine nimekosea wakati wa kufyatua lakini hata sikuwa najua chochote kuhusu bastola. Nikamgeukia Bonta, nikamuona eti anapiga makofi kwa mbali, nikatazama kule juu ya ghorofa, nikamuona Bosi Mute akirudisha bunduki yake chini, naye akawa anapiga makofi.

 

Niligeuka na kumtazama kila mtu, nikaona karibu wote wanapiga makofi, nikashusha pumzi ndefu nikiwa sielewi kilichokuwa kinaendelea. Nilimuona Bonta akinisogelea kwa hatua za harakaharaka, akaja na kunishika mkono kisha akanikumbatia kwenye kifua chake kikubwa.

 

“Safi sana!” aliniambia huku nikiwa bado sielewi ni kwa sababu gani ananiambia vile.

 

“Huu ndiyo mtihani mgumu kuliko yote, mtihani wa pili utakuwa mwepesi sana kwako na naamini utaufurahia,” aliniambia, nikashusha pumzi ndefu na kutaka kumuuliza kitu lakini akanipa ishara kwamba huo siyo muda wa maongezi.

 

Alisogea mpaka pale yule mtoto alipokuwa amekalishwa chini akiendelea kulia, akamuinua na kumbeba kifuani kwake, akawa anambembeleza. Akamsogeza pale nilipokuwa nimesimama,, akanipa ishara kwamba nimpokee. Nikafanya hivyo huku bado machozi yakiendelea kunitoka.

 

Ni mtoto huyu ndiye eti niliyetakiwa kumpiga risasi kwa mkono wangu na kumuua! Nilimtazama usoni, naye alikuwa analia, nikambusu kwenye paji la uso kisha nikamkumbatia kwa nguvu sana huku nikiendelea kulia.

 

“Nifuate!” alisema Bonta, nikawa natembea kumfuata nyuma yake huku nikiwa nimembeba yule mtoto ambaye sasa hivi alishaanza kutulia. Tulipanda ngazi za chuma zilizokuwa ndani ya godauni lililokuwa na magari mengi yakiendelea kurekebishwa, tukatokezea juu kabisa.

 

Kumbe Bosi Mute alikuwa pia na ofisi nyingine juu kabisa ya godauni na muda ule wakati amenishikia bastola, alikuwa nje ya ofisi hiyo, kwenye ‘balcony’. Tuliingia mpaka ndani ambako tulimkuta akiwa peke yake, akiwa amekaa kwenye kiti cha kuzunguka, mbele yake kukiwa na ‘skrini’ kadhaa kubwa, zote zikiwa zinaonesha matukio yaliyokuwa yakiendelea ndani na nje ya eneo lote hilo.

 

Kitu ambacho nilikuwa sikijui ni kwamba kumbe eneo lile lote, kuanzia nje, tebna mbali kabisa mpaka ndani, kulikuwa kumefungwa kamera za ulinzi (CCTV) ambazo zilikuwa zikionesha kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Nikashangaa sana.

 

“Kazi nzuri,” alisema Bosi Mute huku akisimama na kunyoosha mkono kunipa, na mimi nikampa kwa heshima. Akaniambia siku nyingine nikipewa bunduki na kuambiwa ni-shoot, sitakiwi kupoteza sekunde hata moja.

 

Alirudi kukaa pale kwenye kiti chake, akafungua moja kati ya droo nyingi, akatoa bunda la noti za shilingi elfu kumikumi na kulitupa juu ya meza.

 

“Hakikisha huyo malaika wa Mungu anafikishwa kwenye mikono salama! Tumia akili yako kujua utafanya nini, lakini nataka awe salama lakini asiache alama yoyote inayoweza kumuunganisha na sisi,” alisema Bosi Mute, nikainamisha kichwa kwa adabu kuonesha kukubali, kisha nikachukua lile burungutu la fedha na kuliweka mfukoni.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube:

Hashpower Online.

 

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply