SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)-23
MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:
Nilijikausha pale chini huku nikishikilia vyuma vinavyoziunganisha siti za gari na ‘chasis’, dereva akaendelea kufanya yake na kiukweli nikiri kwamba maisha yetu kwa wakati huo, yalikuwa yakimtegemea yeye.
Hata sijui alifanikiwa vipi kuwaacha wale askari ambao nao walipoona tumekimbia, waliingia kwenye magari na kuanza kulifukuzia gari letu huku wakifyatua risasi kama mvua.
SASA ENDELEA…
Dakika kadhaa baadaye, gari likiwa linakwenda kwa mwendo ambao huwezi kuuelezea kwa urahisi, milio ya risasi iliacha kusikika, nikajikaza kiume na kuinua kichwa changu kutazama kule nyuma, sikuweza kuona chochote kutokana na jinsi gari lilivyokuwa linatimua vumbi, nilichoamini ni kwamba tayari tumeshawaacha wale askari.
Bado moyo wangu ulikuwa ukienda mbio kuliko kawaida, kitendo cha kushuhudia wenzetu wawili wakipigwa risasi mbele ya macho yetu, kilinifanya niwe ni kama nimechanganyikiwa.
Niliikamata vizuri bunduki yangu, nikachomoa ‘magazine’ ambayo ilikuwa imeshaisha risasi, nikachukua nyingine kwenye koti langu na kuipachika, nikaikoki bunduki huku nikitetemeka kuliko kawaida. Niliielekezea kule nyuma kwa ajili ya kujihami, huku moyo wangu ukipiga kwa nguvu na kusababisha mwili wote ulowe kwa jasho.
Kioo cha nyuma na vile vya pembeni vilikuwa vimevunjwavunjwa kwa risasi na kama unavyojua, kioo cha gari kikikutana na kishindo cha kutosha, hakiishii tu kutoboka bali kinamwagika chote! Ndivyo ilivyotokea.
Kwa muda wote huo, sikuwa nimemtazama yule mwenzangu mmoja tuliyefanikiwa kuingia naye kwenye gari, kwa sababu nilimuona akiingia akiwa mzima, niliamini amejibanza chini ya siti kama nilivyokuwa nimefanya mimi lakini nilipogeuka na kumtazama, nilishtuka kupita kawaida.
Macho yake alikuwa ameyakodoa mpaka mwisho, tena yakitazama upande wa juu! Damu nyingi zilikuwa zimetapakaa pale alipolala, ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe naye alikuwa amepigwa risasi.
Niliiinama haraka na kujaribu kumtingisha, lakini hakutisikika! Nilijaribu kusikiliza mapigo ya moyo wake, nikagundua kwamba hayakuwa yakipiga. Ulikuwa ni mshtuko mkubwa mno kwangu, kwa tafsiri nyepesi, katika lile kundi la watu wanne kutoka kikosi B, ni mimi peke yangu ambaye nilikuwa hai mpaka muda huo na hata sikuwa na uhakika kama nitafika kambini nikiwa hai.
Nilishindwa kujizuia, machozi yakawa yananitoka huku nikiwa bado siamini, kila kitu kilitokea kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba kuna wakati nilikuwa najihisi kama nipo kwenye ndoto. Hata sikuelewa dereva amepita njia gani, akili zilipokuja kunikaa sawa, nilishtukia tukiwa getini, walinzi wakafungua geti haraka na gari likaingizwa ndani kwa kasi kubwa.
Halikupaki pale ninapofahamu kwamba magari huwa yanapaki, nilishangaa geti jingine likifunguka kutokea chini ya ardhi na kutengeneza kama ngazi fulani ya kuingilia chini, gari likaingia kisha lile geti likafungwa.
Harakaharaka niliruka kupitia vioo vilivyovunjwa, nikasimama huku nikitetemeka kuliko kawaida, bunduki ikiwa mkononi. Dereva naye aliteremka na kunifuata, naye akionesha kuchanganyikiwa sana.
“Safi sana braza!” aliniambia huku akinikumbatia na kunipigapiga mgongoni!”
“Wenzetu wote wamekufa!”
“Vitani hatuhesabu waliokufa! Tunahesabu tuliorudi salama,” alisema huku na yeye akitetemeka! Sekunde chache baadaye, tulikuwa tumezungukwa na akina Bonta, Jombi na wenzake.
“Mmerudi wangapi?” aliuliza Jombi huku akisogea kibabe, mdomoni akitoa moshi mwingi wa kile kilichoonekana kuwa ni bangi kutokana na harufu yake! Hakuna aliyemjibu. Macho yangu yalicheza kwa haraka, nikamuona Bonta na wale wengine tuliokuwa nao eneo la tukio wakiwa wameshawasili.
Walikuwepo wengine kadhaa ambao nikiri kwamba sijawahi kuwaona, Jombi akazidi kutusogelea, akasimama jirani na yule dereva tuliyekuja naye, akamkumbatia huku akimpigapiga mgongoni.
“Kazi nzuri sana! Safi sana,” alisema kisha akanifuata na mimi.
“Umewezaje kurudi salama! Umenishangaza sana,” alisema huku akinikumbatia kwa nguvu, akaninyanyua juujuu na kupiga kelele kwa nguvu!
“Mmemuona mwanaume mwenzetu?” alisema huku akiwa bado ameninyanyua, akicheka kicheko ambacho hata sijui nikiiteje! Wenzake wote wakawa wanapiga makofi. Bado machozi yalikuwa yananitoka, akanishusha na kunikumbatia tena!
Wenzake nao walisogea, kila mmoja akawa ananipongeza kwa kazi nzuri na wa mwisho alikuwa ni Bonta ambaye yeye hakusema maneno mengi zaidi ya kunipa mkono kisha akatoa ishara kama ananipigia saluti.
“Sikukosea kukuchagua,” alisema kisha akageuka na kunipa mgongo, akarudi kule kwa wenzake, harakaharaka niliwaona wanaume wengine wawili ambao sikuwahi kuwaona kabla, wakaja pale kwenye gari wakiwa na machela, wakautoa mwili wa yule mwenzetu na kutoka naye.
Hata sijui walielekea wapi lakini nadhani walimpeleka kwenye vyumba vingine kulekule chini. Kitu ambacho nilikuwa sikijui, kumbe kwenye ile kambi kulikuwa na sehemu nyingine ya chini ya ardhi ambako nako kulikuwa na watu kibao kama kule juu, nikabaki nimepigwa na butwaa.
Bado nilikuwa siamini kama hatimaye nipo salama, nikawa hata sijui nijipongeze au niendelee kulia. Bonta alinipa ishara kwamba nimfuate, basi lile kundi lote likawa linaelekea upande wa pili kulikokuwa na lile gari jingine ambalo nalo lilikwenda eneo la tukio.
Lile sanduku tuliloliiba kule benki, lilikuwa limeshateremshwa, wanaume wenye nguvu wakawa wanasaidiana kulibeba na tulitokezea kwenye chumba kilichokuwa kama karakana fulani hivi. Bosi Mute alikuwa amekaa juu ya meza, naye akivuta sigara na kutoa moshi mwingi.
Alipotuona tukiingia tu, alisimama na kuanza kupiga makofi, basi tuligawanyika makundi mawili, wale ambao sijawahi kuwaona walikaa upande wao na sisi tuliokuwa eneo la tukio tulisimama upande wetu, Bosi Mute akatusogelea na kuanza kutukumbatia, mmoja baada ya mwingine.
“Chalii umerudi salama! Aisee,” alisema huku akinikumbatia na kama ilivyokuwa kwa Jombi, naye aliniinua juujuu kwa furaha, akanipongeza sana. Nilijiuliza maswali mengi sana kwamba kauli zao zilikuwa zinamaanisha nini.
Kwa lugha nyepesi, hakuna aliyetegemea kwamba nitarudi salama, kwa hiyo walitutoa wakijua kwamba wote kutoka Kikosi B tunaenda kufa? Nilishindwa kupata majibu. Harakaharaka lile sanduku lilisogezwa kwenye mashine kama za kukatia vyuma, wanaume wanne wakawa wanasaidiana kuliweka vizuri kisha mashine ikawashwa, likaanza kukatwa pale kwenye kitasa.
Baada ya dakika chache za kuhangaika na lile sanduku, hatimaye walifanikiwa kukata kitasa na kufungua mlango, ndani kulikuwa kumesheheni noti mpyampya, za shilingi elfu kumikumi na shilingi elfu tano.
Bosi Mute ndiye aliyekuwa wa kwanza kutia mkono, akatoka na kibunda kimoja kilichokuwa kimefungwa kwa staili ya tofauti kidogo, kama umewahi kwenda benki na kuona jinsi noti mpya zinavyofungwa na kutengeneza kama ‘kiboksi’ hivi, basi ndivyo hela hizo zilivyokuwa zimefungwa.
Alikifungua kile kiboksi na kurusha maburungutu hewani, watu wote wakawa wanashangilia kwa furaha.
“Mmefanya kazi nzuri sana!” alisema Bosi Mute huku akielekeza zile fedha zote zitolewe kwenye lile sanduku na kuwekwa mezani. Japokuwa sanduku kilikuwa dogo, kwa jinsi zile fedha zilivyokuwa zimepangwa, ilionesha zilikuwa nyingi kwelikweli kwani zilipowekwa pale mezani, zilitengeneza kama kamlima fulani.
“Nawaruhusu mkapumzike ila kila mmoja anatakiwa kuwa makini sana,” alisema Bosi Mute huku akimpa kila mmoja kibunda cha fedha. Alipofika kwangu, alinipa vibunda viwili kwa furaha na akaniambia nimemfurahisha sana.
Baada ya hapo, kila mmoja akiwa na fedha zake, tulitoka na kupanda mpaka kwenye kile chumba cha mikutano, tukabadilisha nguo na kukabidhi vifaa vyote tulivyoondoka navyo, tukatoka kila mmoja na njia yake.
Kiukweli bado nilikuwa na hofu kubwa mno ndani ya moyo wangu, kumbukumbu za tukio lililotokea zilikuwa zikiendelea kujirudia kwenye kichwa changu, ikafika mahali kichwa kikawa ni kama kinataka kuchanganyikiwa.
“Vipi mdogo wangu, hebu twende huku,” alisema Bonta baada ya kuniona nasuasua pale juu nikiwa hata sielewi nini cha kufanya.
Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.
