The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Millen Magese Inaumiza Usipime

Millen Happiness Magese

SIMULIZI ya kupata mtoto ya mwanamitindo wa kimataifa, mjasiriamali na Miss Tanzania mwaka 2001, Millen Happiness Magese inasikitisha na kwake ulikuwa ni muujiza mkubwa mno kwenye maisha yake. Jifikirie miaka 24 unapambana kupata mtoto, hakika si kipindi kifupi! Millen amepambana muda mrefu mpaka anafanikiwa Julai mwaka jana kumpata mtoto huyo Prince Kairo.

IPO HIVI;

Tatizo hili lilimuanza Millen akiwa mwanadada mwenye miaka 13, punde tu alipoanza kupata hedhi. Millen amewahi kusimulia kwamba kila ulipokuwa ukifika mzunguko wake alikuwa akipatwa maumivu makali mno kiasi kwamba anaugua na baba yake anambeba na kumpeleka hospitali. Huko alilazwa siku tano mpaka saba na madaktari walimwambia kwamba ni tumbo la kawaida tu la hedhi!

LINI ALIGUNDUA TATIZO NI KUBWA?

Mara ya kwanza Millen kugundua kuwa maumivu aliyokuwa anapambana nayo kila mzunguko wake wa hedhi, kuugua mara kwa mara na afya yake kudhorota kulisababishwa na tatizo la Endometriosis, ilikuwa mwaka 2007, akiwa na umri wa miaka 26, akiishi nchini Afrika Kusini.

Ilikuwa siku moja akiwa kazini nchini humo, alipata hedhi iliyoambatana na maumivu makali mno kiasi kwamba akazimia. “Nilipelekwa hospitali na baada ya kufanyiwa vipimo ndipo nilipogundulika ninahili tatizo kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 13 na lilikuwa limekwisha kuwa kubwa sana.

“Nilikuwa nina uvimbe kwenye kibofu cha mkojo, kwenye njia ya uzazi na utumbo wangu ulikuwa umejikunja na jambo lingine ilifika hatua nikawa hata siwezi kuzuia mkojo. Nikafanyiwa upasuaji na kukatwa utumbo. Kwa mwaka huo pekee nilifanyiwa upasuaji mara tatu. Aambiwa hawezi kuzaa tena!

“Baada ya hapo maisha yaliendelea, kutokana na umri nilitamani mtoto kwa hiyo nikafanya jitihada za kumpata. Lakini kwa bahati mbaya nilibeba ujauzito mara mbili na zote ziliharibika. Nilipokwenda kufanyiwa uchunguzi tena niliambiwa na madaktari siwezi kuzaa tena.

“Niliumia mno. Lakini sikuamini kabisa kwamba nisingeweza kuzaa tena pamoja na vipimo hivyo. Niliendelea kuhangaika kutafuta mtoto. Nikalipa zaidi ya dola 23,000 ambazo ni zaidi ya milioni 50 za Kitanzania ili kupandikizwa mayai, lakini sindano 67, zote nilizochomwa kupandikiza mayai hazikuweza kufanikiwa.

“Hapo ndipo nilipofahamu kwamba tatizo langu lilikuwa siriazi na ndipo mwaka 2014, nilipoamua kuanza kulizungumza hadharani, kujitangaza na kuelimisha. Nimetumia kiasi kikubwa mno cha fedha kwenye upasuaji. Nimefanyiwa upasuaji zaidi ya mara 13, bila mafanikio. “Hata hivyo upasuaji wa 13, ambao nilifanyiwa mwaka 2015, kidogo uondoke na mimi. Kutokana na ukubwa wa tatizo lilikuwa wakati huu limefika chini ya utumbo na utumbo ukiguswa tu au kupata tatizo lolote wakati wa upasuaji lazima mtu hufariki.

“Nilikaa kwenye chumba cha upasuaji saa tano, ninamshukuru Mungu madaktari walikuwa makini nikaweza kutoka nikiwa salama. Lakini wiki moja baadaye nilipata tatizo lingine kubwa maana utumbo ulifunga na nikawa ninashindwa kupata choo. Choo kikawa kinapanda juu kifuani ikafikia wakati nikabadilika rangi na kuwa wa kijani. Nilikimbizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, nikatibiwa na Mungu ni mkubwa leo nipo hai!

ATAKA KUTOA KIZAZI

Kutokana na tatizo lake mara kadhaa amewahi kushauriwa na madaktari kwamba atoe kizazi. Kwamba akitoa kizazi afya yake haitadhorota sana, hatapata maumivu tena makali kila mzunguko wa hedhi utakapofika.“Ilifika hatua nikakubaliana na ushauri huu na kutaka kutoa kizazi. Lakini mara tatu zote nilipofanya maamuzi, nikifika hospitali nilikuwa nikiahirisha na nilibadili na kuamini ipo siku Mungu ataniona.

MAISHA YAKE HAYANA FURAHA

“Kiukweli tatizo hili limenipelekea kuishi maisha yasiyo na furaha kabisa. Ninaweza kulala mzima lakini siku inayofuata nikaamka siwezi kufanya chochote.

“Ninapambana na maumivu makali ya mgongo na mwili wote na kutokana na tatizo hili nimewahi kupoteza kazi mara kadhaa. Mbali na hilo nimewahi kuachana na wapenzi wanne, niliowapenda na kuwathamini sana.“Kisa cha kuachana ni maumivu maana hata tendo la ndoa nilikuwa siwezi kushirki vizuri, ninaumia.

“Wakati mwingine tu unakuwa huna furaha kutokana na maumivu unayoyapitia wakati mwenzio anataka umpe furaha. Kutokana na hali hiyo niliamua kujiweka pembeni na kuwaacha watu ninaowapenda ili wawatafute watu wanaowapenda na wawape furaha.”

AFANIKIWA KUPATA MTOTO!

Baada ya mapambana ya miaka 24 na tatizo hili la Endometriosis, Julai mwaka jana aliweza kufanikiwa kupata mtoto aliyempa jina la Prince Kairo, baada ya kupandikiza mbegu kwa mara nyingine.

ENDOMETRIOSIS NI NINI?

Tatizo hili ni kubwa sana duniani na linaua zaidi ya watu milioni 176, duniani kote. Kifupi ni hali ambayo inatokea kwamba seli ya ndani ya jumba la uzazi inakuwa nje ya jumba la uzazi na sehemu nyingine inayozunguka jumba la uzazi.

Seli hiyo ni Endimetriam, ambayo ni leya ambayo inampa mwanamke hedhi kila mwezi. Sasa kwa mwanamke mwenye tatizo hilo, unakuta hiyo seli inavunjika ndani na nje ya jumba la uzazi. Ambapo damu inayokuwa nje ya jumba la uzazi inakuwa haina mirija ya kuipitisha itoke nje. Inabaki na kuanza kuunda uvimbe na kusambaa sehemu mbalimbali mwilini kwa mwanamke.

Makala: Boniphace Ngumije

 

 

Comments are closed.