The House of Favourite Newspapers

SKENDO YA PENZI NA DIAMOND… NDOA YA MTANGAZAJI KIMENUKA!

DAR ES SALAAM: KIMENUKA! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia, ndoa ya Mtangazaji wa Kipindi cha Profile and Style kinachorushwa kupitia Televisheni ya Channel Ten, Zein Aklan kutikisika baada ya mrembo huyo kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

ISHU ILIPOIBUKA

Sakata la ndoa ya mrembo huyo kupumulia mashine liliibuka hivi karibuni katika mtandao wa Instagram, baada ya ‘page’ mbalimbali kuposti kuwa mrembo huyo ana uhusiano na Diamond.

Mitandao hiyo ilienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, mtangazaji huyo ndiye kipenzi cha mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ na kwamba ndiye atakayeolewa na Diamond.

“Jamani huyu ndiyo kipenzi cha mama Diamond na ndiye atakayeolewa badala ya Zari,” mitandao mbalimbali iliandika huku ikiunganisha picha za mrembo huyo, Diamond na Zari.

 

WATU WAHOJI KULIKONI

Wachangiaji mbalimbali wa kurasa za udaku katika mitandao ya Instagram walihoji kulikoni mtangazaji huyo aingie kwenye skendo ya penzi na Diamond wakati ana ndoa yake ya muda mrefu. “Kulikoni huyu dada jamani, si ana ndoa yake? Inakuwaje tena aolewe na Diamond au ndio keshaachika?” alihoji mmoja wa wachangiaji mtandaoni.

MITANDAO YASHUSHA DATA

Mitandao hiyo ilishibisha madai yao kwa kueleza kuwa, uhusiano wa mtangazaji huyo na Diamond umeibuka mara baada ya mrembo huyo kufanya kazi na Diamond kama mtu wa kuwapamba wasanii wa Kruu ya Wasafi Classic Baby (WCB).

 

SASA KIMENUKA!

Chanzo makini kilipenyeza habari kuwa, mara baada ya mitandao hiyo kuandika uhusiano wa Diamond na mrembo huyo bila kuwa uthibitisho, ndoa ya Zein iliwaka moto baaada ya mumewe Arif Aklan kuona ubuyu huo mtandaoni.

“Unaambiwa baada ya mumewe kuona habari hizo mtandaoni na kuona mkewe ameunganishwa picha na Diamond na Zari, alimcharukia kweli mkewe maana aliamini kuwa haiwezekani watu waibue tu ishu pasi na ukweli,” kilidai chanzo.

HUYU HAPA ZEIN

Akizungumza na Gazeti la Amani huku akitokwa na machozi kwa uchungu, mtangazaji huyo ambaye amedumu kwenye ndoa yake kwa takriban miaka nane, alisema anaumia kuona mtu ameamua kumchafua kwenye mitandao ya kijamii kuwa ana uhusiano na Diamond huku wakidai kuwa ameshaachana na mumewe muda mrefu.

“Yaani hapa nilipo nipo kwenye tabu kubwa sana na mume wangu kwa sababu haelewi ni kitu gani hiki na isitoshe hajawahi kuona mambo kama haya kwenye mtandao tangu tumeishi hivyo habari hizo zimeleta mtafaruku mkubwa sana. “Ndugu wa mume wangu nao hawanielewi na mimi sijaachana na mume wangu kama watu wanavyosema mitandaoni, naumia jamani maana habari hizo hazina ukweli na zimeniweka kwenye wakati mgumu sana,” alisema Zein.

 

AZIDI KUTIRIRIKA

Aliendelea kueleza kuwa kwa mara ya kwanza aliona kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram akajua kuwa labda watu wamekosea lakini siku zilizidi kusonga, ndiyo akaona watu wakizidi kusambaza habari hiyo.

“Unajua hata mwanzo mume wangu alivyoona alielewa na akaachana nayo akajua wazi kuwa labda watu walikosea lakini bado waliendelea kukomalia kuwa mimi na Diamond ni wapenzi.

AWAOMBA WAACHE

“Nawaomba wanaosambaza skendo hiyo waache jamani maana ndoa yangu inaweza kuvunjika wakati wowote kwa sababu ya kitu ambacho hakina ukweli wowote, sina hata mazoea ya kivile na Diamond,” alisema Zein.

Alipoulizwa kama amewahi kufanya kazi na Wasafi, mrembo huyo akasema hajawahi kabisa kufanya nao licha ya kwamba Diamond wanafahamiana.

 

DIAMOND ANASEMAJE?

Ili kusikia upande wa pili, Amani lilimtafuta Diamond ili kumsikia anazungumziaje ishu hiyo lakini simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa. Jitihada za kumtafuta zinaendelea ili naye atie neno kuhusiana na skendo hiyo inayomharibia Zein.

Stori Mwandishi Wetu, Amani

Comments are closed.