Sven Awaweka Kando Ajibu, Kichuya Simba
KUFUATIA kutoonekana uwanjani katika michezo ya Ligi Kuu Bara kwa wachezaji wa Simba, Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya, kocha mkuu wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck amefunguka kuwa uwezo mkubwa unaoonyeshwa na wachezaji wengine katika kikosi chake ndiyo chanzo cha wachezaji hao kukaa benchi.
Mara ya mwisho Ajibu na Kichuya kucheza ilikuwa katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Stand United, Februari 25, mwaka huu ambapo Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 3-2.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Sven alisema ubora wa wachezaji wanaoanza katika kikosi cha Simba unawafanya wachezaji hao kukaa benchi, hivyo wanatakiwa kuboresha viwango vyao ili wawe kwenye ushindani wa kugombea namba katika kikosi hicho.
“Ajibu na Kichuya ni wachezaji wazuri sana, siyo kwamba wanakaa benchi kwa kuwa nataka wakae benchi ila wachezaji wanaocheza wanastahili kuanza, wananishawishi kutokana na uwezo wanaouonyesha katika michezo wanayaoanza kila ninapowapa nafasi.
“Wanachotakiwa ni kutambua kuwa Simba ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, hivyo wanatakiwa kupambana hasa ili ninapowapa nafasi wazidi kunishawishi na hiyo itakuwa ni faida kwao na kwa timu,” alisema kocha huyo.
Stori na Marco Mzumbe, Dar es Salaam



