WABUNGE wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na Ester Bulaya, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, Katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar, Henry Kileo na wafuasi wengine wa chama hicho, wamekamatwa na polisi baada ya kutokea vurugu wakati wakifuatilia kuachiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kutoka Gereza Kuu la Segerea, leo Ijumaa, Machi 13, 2020.
Askari Magereza wametumia silaha za moto na kufyatua risasi hewani kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliokuwa nje ya gereza hilo kumsubiri Mbowe akiachiwa huku baadhi ya viongozi na wananchi kadhaa wamejeruhiwa, akiwemo dereva mmoja wa bodaboda ambaye inadaiwa amevunjika mguu.