The House of Favourite Newspapers

Tajiri Aliyedaiwa Kuuawa na Nyumba Ndogo Giza Nene

NI Majonzi! Ndilo neno pekee unaloweza kulitamka kufuatia kifo cha tajiri mmoja aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Exaud Makyao ambaye ameondoka duniani kwa madai ya kuuawa na mwanamke aitwaye Maureem aliyedaiwa kuwa ni nyumba ndogo yake.

Msiba huo ulitokea Juni 14, mwaka huu huku maelezo ya awali yakieleza kuwa, Emmanuel ambaye ni mmiliki wa Kampuni iitwayo Me Company Ltd, kifo chake kilitokana na ajali ya gari ya makusudi iliyosababishwa na Maureen.

KIFO CHAACHA GIZA NENE

Baada ya msiba huo kutokea huku nyumba ndogo ya Emmanuel ikihusishwa, ikidaiwa kuwa kulikuwa na mgogoro kati ya wawili hao kabla ya umauti kumfika.

Waandishi wetu walifika msibani, Bunju jijini Dar ili kupata ukweli wa tukio hilo lakini ndugu wa marehemu walikuwa wagumu kutoa ushirikiano.

Lengo la waandishi wetu kufika msibani hapo ni kujua ukweli wa namna Maureen alivyohusika kwenye kifo cha Emmanuel na uhalali wake kwa marehemu kwani madai ya awali yalieleza kuwa, mwanamke huyo ni mkewe na walikuwa wamekorofishana.

“Maureen na marehemu walikuwa walitofautiana, siku ya tukio walipokutana baada ya kukwaruzana sana, Emma alisimama mbele ya gari alilokuwa akiendesha Maureen ili kumzuia asiondoke, lakini Maureen akaiondoa na kumburuza marehemu kwa umbali flani na kumsababisha kifo,” ndiyo maelezo ya awali yaliyotolewa baada ya tukio hilo.

Akizungumza na Amani, mmoja wa ndugu wa marehemu aliyegoma kutaja jina lake alisema: “Msiba umeshatokea, tuacheni tukampumzishe ndugu yetu, hayo ya kwamba sijui kauawa na nani siyo wakati wake huu, tumeshaongea kwamba habari zilizosambaa awali hazina ukweli.”

Hata hivyo, wengi waliokuwa msibani hapo, walishindwa kuelewa kwamba aliyehusika katika kifo cha Emmanuel ni mke, nyumba ndogo au ni nani kwa marehemu maana katika zoezi la kuuaga mwili wa marehemu, mke anayetambulika eneo hilo aitwaye Mama Fey alikuwepo huku akionekana kuwa na majonzi makubwa.

Akizungumza na Amani, jirani wa mama Fey alijitambulisha kwa jina la Felister Edward ‘Mama John’ alisema: “Msiba huu umetuacha kwenye giza nene, huyo anayedaiwa kusababisha kifo cha shemeji yangu Emma, wala simjui lakini wanasema eti ni nyumba ndogo, mara mkewe… kikubwa tumuombee marehemu, ndicho kilichobaki, hayo mengine tuiachie familia na vyombo vya dola.”

Mwili wa marehemu ulisafirishwa kwenda Mwika, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi na taarifa ambazo Amani ilizipata (si kutoka vyanzo vya polisi) ni kwamba Maureen anashikiliwa na jeshi la kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Boniphace Ngumije na Memorize Richard

Stori: Waandishi Wetu, Amani

Comments are closed.