The House of Favourite Newspapers

Tajiri wa Madini Atua Yanga SC

ACHANA na hao wengine unaowajua au uliowahi kuwasikia. Huyu ni mpya. Bilionea wa jiji hili la Mwanza, Leorand Bugomola ameingia kuongeza nguvu ndani ya kikosi cha Yanga kuhakikisha kinamuua Mwarabu, Pyramids.

 

Yanga iko kwenye maandalizi kabambe ya kuwavaa Pyramids ya Misri katika mchezo wa mtoano wa kuwania kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa jijini hapa Oktoba 27, mwaka huu.

 

Awali ndani ya jiji la Mwanza kulikuwa na bilionea mwingine ambaye alizoeleka zaidi katika kuisaidia Yanga anayefahamika kwa jina la Yanga Makaga lakini sasa naye amepata nguvu zaidi kutoka kwa Bugomola.

 

Makaga ndiye aliyekuwa akiipokea Yanga inapokwenda kucheza mechi zake za kanda ya ziwa huku akiigharamia vitu mbalimbali ikiwemo usafiri wa ndege.

 

Akizungumza na Championi
Jumamosi, Katibu Mkuu wa Matawi ya Yanga Mwanza, Mhando Madega alisema kuwa maandalizi kuelekea michezo yao miwili ikiwemo ule wa ligi kuu dhidi ya Mbao FC utakaopigwa, Mwanza Jumanne ijayo yamekamilika.

 

Madega alisema kuwa, kuna bilionea mwingine ambaye anaitwa Bugomola ambaye ameahidi kufanya makubwa zaidi kwa kikosi hicho ili kuhakikisha wanashinda mechi hizo zote mbili.

 

“Lengo ni kuhakikisha tunapata matokeo na kuweka heshima kwa timu yetu hapa Kirumba pia kutoa zawadi mbalimbali kwa wachezaji kama motisha ya kuwapa morali ya kupambana ili wapate matokeo mazuri.

 

“Makaga na Bugomola wameahidi kufanya makubwa mara baada ya timu kutua Mwanza huku wakijiapisha kuwa lazima timu ipate matokeo mazuri nyumbani,” alisema katibu huyo.

 

BUGOMOLA NI NANI

Bugomola ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, pia ni Mkurugenzi wa Leny Hotel iliyopo mkoani Geita amekuwa akijishughulisha na biashara za madini.

 

Bugomola ni mdau ambaye ni mpenzi mkubwa wa michezo na ni shabiki wa Yanga na sasa anakwenda kushirikiana na mlezi wa matawi ya Yanga Kanda ya Ziwa, Makaga kuhakikisha timu hiyo inahudumiwa kwa kipindi chote itakachokuwa Mwanza.

Comments are closed.