Global Ilipowatembelea Wafungwa Gereza la Ukonga Dar es Salaam
Katika kuadhimisha miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, Gereza Kuu Ukonga kwa kushirikiana na Kampuni ya Global Publishers limefanya tamasha la michezo mbalimbali kwa wafungwa wa gereza hilo.
Akiongea katika tamasha hilo, Mkurugenzi wa Global Publishers aliyekuwa pia mgeni rasmi, Eric Shigongo, amewaambia wafungwa kuwa dhamra ya ujio wao gerezani hapo ni katika kuonyesha kuwathamini, kuwahurumia na kuwatia moyo kwamba kuwa kwao gerezani siyo kwamba wametengwa na dunia.
Shigongo aliwatia moyo wafungwa hao kuwa hawatakiwi kukata tamaa na bado wanayo nafasi ya kubadilika na kuwa raia wema.
“Kila mwanadamu anao wajibu wa kubadili maisha yake, Mwalimu Nyerere tunayemuadhimisha leo alizaliwa kama mimi na wewe na kutengeneza maisha yake na leo tunamkubuka, kwa nini wewe ushindwe?” aliuliza Shigongo.
Aliongeza: “Najua wengi wenu mko hapa mkiwa mmeitwa majina mengi kwa kuwa mmehukumiwa, hizi ni hukumu za wanadamu, mnao uwezo wa kuandika kurasa mpya katika maisha yenu na siku mkitoka duniani waseme mtu mwema ameondoka. Siku moja inatosha kubadili maisha yako, kila siku andika ukurasa mpya wa maisha yako na Mungu atakuongoza.”
Wadau wengine walioungana na Global Publishers katika tukio hilo ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu nchini ikiongozwa na mwenyekiti wake Thom Nyanduga na Rajab Maranda (aliyewahi kuwa mfungwa gereza hilo la Ukonga) ambao kwa pamoja walileta zawadi mbalimbali kwa wafungwa hao vikiwemo vifaa kama sabuni, soda na kikombe ambacho kilitolewa kwa timu iliyofanya vizuri katika mpira wa miguu.
Katika tamasha hilo wafungwa walishiriki michezo ya kukimbia katika magunia, kukimbia na yai katika kijiko, mbio za mita 100 vijana kwa wazee, mita 400 kupokezana vijiti, kuvuta kamba, mieleka, mpira wa miguu, mashairi, kuonesha vipaji vya uchekeshaji, kuimba kwa mtindo wa kufokafoka, ngoma za jadi na burudani kwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Twanga Pepeta.
Picha zote na ASP Deodatus Kazinja wa Jeshi la Magereza.
Comments are closed.