The House of Favourite Newspapers

Tangulia Radio…. Ngoma Zako Hatutazisahau!

“Baada ya leo utanikumbuka mimi, kama nikikupa upendo wangu utanikumbuka?… Utanikumbuka?… Utanikumbuka?”

HII ni sehemu tu ya tafsiri ya mistari ya Wimbo wa Remember ulioimbwa kwa Lugha ya Kingereza na aliyekuwa staa wa muziki Afrika Mashariki, marehemu Moses Nakintije Ssekibogo ‘Mowzey Radio’.

Radio alifariki dunia Alhamisi iliyopita katika Hospitali ya Case jijini Kampala, Uganda ambako alikuwa amelazwa baada ya kuripotiwa kupigwa hadi kupoteza fahamu kwenye klabu ya pombe ya De Bar huko Entebbe.

Katika makala haya, yanamuelezea Radio kuanzia alipoanza muziki, mchango wake kwenye tasnia ya muziki Afrika Mashariki na namna ambavyo mastaa mbalimbali wamemlilia baada ya kifo chake.

 

Safari yake ya muziki ilikuwaje?

Radio ambaye amezaliwa Januari 25, 1985, alianza muziki akimsapoti Jose Chameleone kabla ya mwaka 2004 kutoa wimbo wake wa kwanza uitwao Tujja Kuba Wamu akiwa ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere cha nchini Uganda.

Baada ya kuingia rasmi kwenye muziki, Radio alifanya kazi kwa karibu zaidi na Chameleone na kaka yake, Weasel Manizo. Baadaye walikorofishana na Chameleone ambapo yeye na Weasel waliamua kuunda kundi lao la muziki la Goodlyfe, lakini baadaye wakisainiwa kwenye label iitwayo Leone Island Music Empire.

Radio alianza kuwika zaidi kimuziki mwaka 2005 baada ya kuachia ngoma yake ya Jennifer na baadaye akaibuka na Sweet Lady uliomtambulisha zaidi na zaidi Afrika Mashariki.

 

Baada ya kuwa maarufu, Radio alibahatika kufanya ziara za kimuziki Marekani na kwenye Visiwa vya Caribbean, achana na nchi mbalimbali za Kiafrika.

Akiwa na Kundi la Goodlyfe, Radio na Weasel walifanya ngoma kali zikiwemo Nakudata, Ability, Ngamba, Akapapula, Bread and Butter, Hellenah, Juice Juicy, Lwaki Onnumya, Magnetic, Tukikole Neera, Mr DJ, Mukama Talya Mandazi, Ngenda Maaso, Nyambula, Nyumbani, Obudde, Potential, Sitaani, Zuena na Neera.

 

Kifo cha Radio kilikuwaje?

Radio alishambuliwa na baunsa wa ukumbi wa muziki wa De Bar uliopo Entebbe baada ya kutokea mzozo kati yake na mmiliki wa baa hiyo ambapo taarifa zilielezwa kuwa alipata hitilafu katika ubongo na kulazimika kuwa chini ya uangalizi wa madaktari watatu kabla ya kukutwa na umauti usiku wa kuamkia Januari Mosi, mwaka huu.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, klabu hiyo ya pombe ilifungwa ambapo mmiliki wake na baunsa aliyempiga Radio wameshikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.

 

Mastaa wengi Afrika wamlilia

Kifo cha Radio kimeo-nesha kuwa-gusa watu wengi Afrika, ambapo ukiachana na mashabiki mbalimbali wa muziki baadhi ya mastaa walionesha kuguswa na msiba wake ni pamoja na Wizkid, Jose Chame-leone, Prezzo, MwanaFA, Diamond, Weasel na wengine wengi.

 

Yoweri Museveni naye atoa la moyoni

Msiba wa Radio umeonekana kumgusa pia Rais wa Uganda, Yoweri Museven ambaye awali alitoa shilingi milioni 30 za Uganda kwa ajili ya matibabu na baada ya mauti kumkuta Radio, rais huyo aliandika katika Mtandao wa Kijamii wa Twitter: “Nimeelezwa juu ya kifo cha mwanamuziki Moses Ssekibogo a.k.a Mowzey Radio. Hivi karibuni nilitoa mchango wangu kwa ajili ya matibabu yake nikitumaini kwamba atapona. Alikuwa kijana mdogo mwenye kipaji, mwenye maisha mazuri ya mbeleni.”

 

Vipi kuhusu mazishi ya Radio?

Safari ya mwisho ya kumsindikiza mwanamuziki Radio kwenye nyumba yake ya milele ilitarajiwa kufanyika juzi huko Kagga, Nakawuka, Uganda ambako ni nyumbani kwa mama yake mzazi.

Boniphace Ngumije | IJUMAA WIKIENDA

Comments are closed.