The House of Favourite Newspapers

TATIZO LA UBAKAJI, ULAWITI KWA WATOTO NI JANGA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.

VITENDO vya ulawiti na ubakaji kwa watoto vimesababisha hofu kubwa katika jamii za Kitanzania na kuwafanya baadhi ya wazazi na walezi au jamii, wasijue nini cha kufanya.

Hilo linafanyika kukiwapo kundi kubwa la watu wasiojua nini hasa kinachomfanya mtu anaamua kubaka au kulawiti, ilhali anajua wazi kwamba ni kosa ambalo adhabu yake ni kali kufikia kiwango cha kifungo cha maisha.

Aliyewahi kuwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba aliwahi kusema kuwa ma­tukio ya kunajisi watoto yamekuwa yakiongezeka kwa kiwango kikubwa.

Kati ya Januari na Machi 2016, kuliripotiwa matukio 1,765 ikilin­ganishwa na matukio 1,585 katika kipindi hicho mwaka 2015. Hili ni ongezeko la matukio 180 nchi nzima.

 

Utafiti mmojawapo uliofanyika nchini, ulibainisha kwamba kuna jumla ya watoto 2,517 waliobakwa kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka jana.

Ni hesabu kubwa zinazobaini­sha kuwa katika kipindi hicho cha miezi saba, katika Manispaa ya Kinondoni peke yake kuliripotiwa jumla ya kesi 187 za ubakaji, ambazo ni wastani wa asilimia 7.4 wa matukio ya kitaifa.

Pia ikumbukwe kuwa, watoto wengi wanalawitiwa au kubakwa na wananchi wanashindwa kuripoti kesi hizo, kupitia mbada­la wa kuzimaliza katika kiwango cha familia na kumlinda mbakaji kwa sababu tu ni ndugu yake, amewalipa pesa au mali.

Kamanda Advera Bulimba

 

SABABU ZA KUBAKA

Zipo sababu kadhaa za watu kujihusisha na ubakaji na ulawiti. Dk Leopord Mwinuka anasema moja ya sababu hizo ni ‘Pedo­philia,’ huo ni ugonjwa wa akili ambao mwanaume mtu mzima, muda wote anatawaliwa na tamaa ya kufanya mapenzi na mtoto mwenye umri wa wastani wa miaka kuanzia 12 na zaidi, hata kama ana mbadala wa kufanya mapenzi na mtu mzima mwingine.

Kwa bahati mbaya, nchini kuna tatizo la uelewa mdogo kuhusu ‘Pedophilia.’ Watu kwenye jamii au kazini wanalalamika kuhusu tabia ya mtu ambaye hata wa­nawake watu wazima wamtake kimapenzi, hayuko tayari na hisia zake zimejikita kwa watoto.

Wanaougua maradhi hayo wamekuwa wakitumia pesa, zawadi au lugha za mvuto kuwarubuni watoto na inaposhindikana, wanaamua kutumia nguvu kufanikisha azma yao.

Sababu nyingine ni msukumo na tabia ya kuiga kimakundi. Kumekuwapo na tabia ya baa­dhi ya vikundi na hasa vijana wanaodhani kwamba kufanya mapenzi na watoto ni sifa. Hiyo ni tabia mbaya na potofu na baadhi yao wamekuwa wakitumia vilevi kuwapa hisia katika kufanya tendo hilo.

 

Baadhi yao, wamekuwa waki­tumia nguvu na vitisho kufaniki­sha azma yao. Sababu nyingine ni baadhi ya watu wanaodhani na kuamini kuwa ni rahisi sana kum­rubuni kimapenzi mtoto mdogo kuliko mtu mzima.

Hivyo, kwa kuwa ameshawahi kujaribu kumtaka kimapenzi mtu mzima akashindwa, anaamua kufuata watoto akihisi ni rahisi. Mtu huyo anapofanikiwa, mara moja anaendeleza tabia kwa wengine.

Pia ipo sababu inayojikita katika dhana ya kulipiza kisasi. Kuna baadhi ya watu wanaoa­mua kubaka kwa kuwa alishawa­hi kulawitiwa alipokuwa mtoto.

Pia zipo imani za kishirikina kwa waumini wa ushirikina, wal­iojenga imani kwamba, kupata utajiri kunafanikishwa kwa njia ya kufanya mapenzi na watoto ambao wengine wamewazaa.

Tofauti ya kundi hilo la waumini wa ushirikina na mengine yaliyotangulia, ni kwamba mvuto mkubwa hujikita kwenye kusaka utajiri.

Katika makundi yale mengine mali na ushirikina, kinachowavutia ni kufanya mapenzi na watoto na wanatumia pesa au mali kufanikisha tendo la ngono.

 

Dalili za mtoto aliyebakwa, kulawitiwa

Kuna dalili nyingi za kumtambua mtoto aliye­bakwa au kulawitiwa moja ikiwa mtoto kuwa na woga uliopi­tiliza kwa mtu au ndugu ambaye zamani hakuwa akimuogopa na anapoulizwa, anakuwa mzito kutoa sababu.

Anakuwa katika namna kwamba ametishwa asiseme, au kuna onyo la siri kwamba akisema ataadhibiwa na wazazi au walezi anatambua kwamba ni kitendo kibaya.

Kuna baadhi wanaogopa sana kubadili nguo mbele za watu, wakati zamani kabla ya tukio hilo, walifanya hivyo kwa uhuru mkubwa.

 

Kuna watoto ambao wak­ishabakwa au kulawitiwa, hubadili hata namna ya kulala na wanakosa usingizi wakitawaliwa na mawazo na kutafakari kilicho­watokea na hatari ya kukabiliwa tena na balaa hilo.

Watoto hao wanafikia hatua ya kuota ndoto mbaya na za kutisha. Anaota mtu anamfanyia tendo lililom­tokea, ikiwa ni pamoja na kutawaliwa na hisia za historia ambayo kitaalamu inaitwa ‘flashback.’

Pia, watoto waliobakwa au kula­witiwa wanakuwa na tabia ya kulala mchana, wakati wa masomo shuleni, yeye anabaki akisinzia au kulala, tabu ambayo hakuwa nayo huko nyuma.

Katika maendeleo ya kitaaluma, mtoto anaanguka ghafla, wakati huko nyuma alikuwa na maendeleo mazuri darasani.

 

Hiyo hutokea hata kuwa mtihani kwa walimu, wazazi na walezi kupata tabu kutambua sababu za haraka zinazofanya kutokea mabadiliko hayo.

Pia ni kawaida ya wanafunzi wenzake shuleni wanalalamika na mabadiliko yake ya tabia, kwani aliye­bakwa anapoteza kabisa hamu ya vitu au michezo ambayo alikuwa akiipenda sana huko nyuma.

Kuna baadhi ya watoto waliobakwa, hubadili namna ya kutembea au kukaa na hasa kutokana na maumivu katika sehemu zao za siri, kulingana na ma­hali alikojeruhiwa.

Itaendelea wiki ijayo.

NA MWANDISHI WETU

Comments are closed.