Trilioni 281 Zilizoibwa Ishu ya Mchanga wa Dhahabu, Huyu…Msaliti?

Viongozi wa ngazi ya juu katika Kampuni ya Acacia.

STORI: MWANDISHI WETU | RISASI JUMAMOSI | HABARI

DAR ES SALAAM: Wakati wananchi wakiendelea kushangazwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho nchi inapoteza kupitia usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi, kunakofanywa na kampuni za uchimbaji madini za kigeni, Mtanzania Deo Mwanyika, ambaye ni ofisa wa ngazi ya juu katika Kampuni ya Acacia, amezua maswali lukuki! Kwa mujibu wa kamati ya kuchunguza kiasi cha madini yaliyopo kwenye mchanga unaosafirishwa katika makontena 277 yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam, iliyowasilisha taarifa yake kwa Rais Dk John Magufuli katikati ya wiki hii ikulu jijini, kiasi cha madini kilichogundulika ni chenye thamani ya shilingi trilioni 1.147 kwa shehena hiyo pekee.

Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika (wa pili kushoto waliokaa) wakati akitiliana saini ya Makubaliano (MoU) na wawakilishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime.

DEO MWANYIKA NI NANI?

Deo Mwanyika ni Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwa na shahada ya kwanza ya sheria na pia ana shahada ya uzamili ya sheria aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza.

Ni Mwanachama wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na Afrika Mashariki. Kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Acacia barani Afrika, akiwa amejiunga nao Machi mwaka 2010, akitokea Kampuni ya Barrick Gold, ambao walimuajiri tangu mwaka 1999 na kupata nafasi mbalimbali za juu za kiuongozi kwa miaka 12, akipanda hadi kuwa Meneja Mtendaji Mkuu, mwaka 2008.

Ni mmoja wa Watanzania wachache wasomi, ambao wamewahi kuaminiwa na kufanya kazi na kampuni kutoka nje kwa muda mrefu, tena akiwa katika nafasi za juu. Anasemwa na baadhi ya watu aliowahi kufanya nao kazi kuwa ni mtetezi mkubwa wa masilahi ya Watanzania katika kampuni anazofanya kazi.

Makamu wa Rais wa Acacia barani Afrika, Deo Mwanyika akiwa amejiunga nao Machi mwaka 2010, akitokea Kampuni ya Barrick Gold.

ANA NAFASI GANI KATIKA MENEJIMENTI?

Deo ni Mtanzania pekee katika watu waliokamata nafasi za juu kwenye menejimenti ya kampuni hiyo yenye kumiliki migodi kadhaa nchini, ikiwemo Bulyanhulu, Nyanzaga na North Mara.

Akishikilia cheo cha Makamu wa Rais wa Acacia Tanzania. Ni afisa wa juu kuwemo katika viongozi wa juu ambao wote ni Wazungu, wakiwemo Andrew Wray, Mark Morcombe, Charlie Ritchie, Peter Geleta, Peter Spora ambao wote wanawajibika kwa bosi mkuu, Brad Gordon ambaye ndiye Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Acacia. Licha ya Tanzania, Acacia pia inamiliki migodi katika nchi za Mali, Kenya na Burkina Faso kwa nchi za Afrika.

NI MSALITI KWA WATANZANIA?

Baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo ya kamati ya usafirishaji wa mchanga wa madini, baadhi ya wananchi wa kada mbalimbali wamehoji ni vipi udanganyifu huo wa kiasi cha madini yaliyomo ndani ya mchanga huo uliweza kufanyika kwa muda mrefu bila kujulikana, kulingana na maelezo ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Mruma, ilihali ndani ya kampuni hiyo yumo Mtanzania mwenzao? Baadhi yao walikwenda mbali na kuuliza ni kwa nini Mtanzania aliyepo katika nafasi ya juu ndani ya menejimenti ya kampuni hiyo ya kigeni, alishindwa kuwa mzalendo kwa ‘kuitonya system’ juu ya udanganyifu huo kama kweli utadhihirika ulikuwepo?

KWA NAFASI YAKE, NI NGUMU KUTOJUA

Samson Thrimas, ambaye alijitambulisha kuwa mwanafunzi wa mojawapo ya vyuo vikuu kilichopo Dar es Salaam, alisema makamu wa rais wa kampuni ni mtu mkubwa, ambaye siyo rahisi jambo kama hilo lifanyike bila yeye kujua. “Hata kama tunasema wale Wazungu wanaweza kuwa walikuwa wanapiga dili, ni jambo gumu kidogo kuamini kuwa yeye kama Mtanzania alikuwa hajui kinachoendelea.

Kama yaliyosemwa na kamati iliyoundwa na rais ni kweli, basi tuna kazi kubwa sana kurejesha uzalendo ule tuliofundishwa na Mwalimu Julius Nyerere. “Pamoja na kwamba watu wanatafuta maisha, lakini unapoona wageni wanachota utajiri wetu namna hii, alipaswa kupenyeza taarifa kwa mamlaka zinazohusika ili ziweze kuchukua hatua, ni pesa nyingi sana hizi, zingeweza kusaidia katika sekta nyingi kama afya, elimu, miundombinu, kilimo na nyinginezo.

ALIOGOPA KUSALITIWA?

Akizungumzia sakata hilo, Felix Mbona aliyejitambulisha kama mwanaharakati, alisema katika ishu zinazohusu fedha nyingi kama hizo ni vigumu kwa watu kutoa taarifa kwa kuhofia usalama wao, hasa wakiwa ni waajiriwa kama alivyo Deo. “Katika dili za mkwanja mrefu kama hizi, kwanza huwa siyo mtu mmoja, hapa kuna watu wengi sana watakuwa wanakamata bahasha, sasa kutoa taarifa zinazosababisha ulaji wa watu kukatika, ni hatari, unaweza hata kuuawa bila kujali nafasi yako, sasa tusimlaumu sana Deo, huenda alijua lakini usalama wake aliweka mbele,” alisema Mbona.

DEO ATAFUTWA

Risasi Jumamosi lilifanya jitihada za kumfikia katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo katika Jengo la Tanhouse, ghorofa ya 11, katika Mtaa wa Kibisho jijini Dar, lakini watumishi walioulizwa walisema asingeweza kupatikana kwa wakati huo kwa kuwa alikuwa na vikao vingi. Kuona hivyo, juhudi za kumpata kwa simu zilifanyika, lakini msichana aliyepokea mapokezi, alimuunganisha mwandishi wetu kwa aliyedai ni msaidizi wake, ambaye hakupokea hadi ilipokatika. Juhudi za kumtafuta zinaendelea.

ANA KAZI NZITO YA KUJISAFISHA

Deo ni kati ya Watanzania wachache waliopata bahati ya kufanya kazi na kampuni kubwa za kimataifa, lakini kwa hili atakuwa na kazi kubwa ya kujisafisha aidha kwa kampuni yake kwenda mahakamani au kufanya lolote kuhakikisha anaifanya ile ripoti ya kamati kuonekana siyo sahihi, kinyume chake Watanzania walio wengi wataona amewasaliti.

ACACIA YAIBUKA, KWENDA KORTINI
Katika taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia, Brad Gordon, ilipingana na ripoti ya kamati hiyo na kueleza kuwa katika kipindi cha miaka 15 ambacho wamefanya kazi ya uchimbaji madini nchini, hawakuwahi kutoa taarifa za uongo zinazohusiana na usafirishwaji wa mchanga wenye madini kwenda nje kwa ajili ya kuchenjuliwa. Alisema wanasubiri kuipata ripoti yote ili waipitie kwa kina kabla ya kuchukua hatua, lakini taarifa nyingine zilisema kampuni hiyo inakusudia kwenda katika mahakama ya kimataifa kupinga zuio la shehena ya mchanga uliopo bandarini Dar es Salaam kwa vile kisheria, mzigo huo ni mali ya mwekezaji.

TUJIKUMBUSHE

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wake, Profesa Abdulkarim Mruma, katika makontena 277 yaliyozuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kufuatia agizo la Rais Magufuli, kuligundulika kuwepo kwa kiasi kikubwa cha madini tofauti na ilivyoainishwa awali na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA). Katika uchunguzi uliofanywa kwenye makontena hayo 277 yaliyokuwa bandarini jijini Dar, kiasi cha dhahabu kilichogunduliwa ni kati ya tani 7.8 hadi 15.5 tofauti na madai ya awali ya wasafirishaji na TMAA ya kuwepo kwa kiasi cha asilimia 0.3 cha madini kwenye makontena hayo yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi.

NENO LA MHARIRI

Gazeti hili linawataka Watanzania kuvuta subira na kutomhukumu Deo juu ya uzalendo wake kwa nchi yake kabla ya jambo hili halijathibitishwa na mahakama.

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment