The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life- 48

0

Wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa nikielezea namna ambavyo mabilioni ya vitambulisho vya taifa yalivyotumika kutengeneza vitambulisho ambavyo havina visivyotimia milioni mbili! Hii ni aibu. Jambo pekee ambalo Watanzania tunatakiwa kufanya ni kumuunga mkono rais wetu John Pombe Magufuli, tuweke kando itikadi na tutangulize uzalendo kwa taifa letu, mbele tukiamini kabisa tunakokwenda ni pazuri, hata kama hapa tulipo tunateseka, ASUBUHI NJEMA INAKUJA! SASA ENDELEA…

Kazi inafanyika, kila mmoja wetu ni shahidi wa kinachofanywa na serikali ya Awamu ya Tano, hakuna kisichokuwa na upungufu hasa wakati kinaanza, lakini ukweli utabaki palepale kuwa Rais John Pombe Magufuli analitendea mema taifa lake la Tanzania hata kama matendo hayo yana gharama kwetu tuliopo leo.

Najisikia sifa kuitwa Mtanzania, sioni aibu tena kusimama mbele ya mtu yeyote na kupaza sauti kwamba mimi ni Mtanzania kwa mambo ambayo yanafanyika nchini mwangu hivi sasa, hata kama yananiumiza mimi kama mfanyabiashara, ni sawa tu, ilimradi maisha ya Watanzania yatakuwa bora badala ya maisha ya mtu mmoja kuwa bora huku wengi wakiteseka.

Katika mahojiano niliyofanya na TBC kuongelea siku 100 za utawala wa Rais John Pombe Magufuli nimesema wazi kuwa, unapoona mataifa kama Kenya, Afrika Kusini ambayo watu wake siku zote wamekuwa wakijisikia wapo juu kuliko mimi wakiisifia Tanzania kwa uongozi wake na hata kuiga mambo yanayofanyika, basi elewa sifa ya taifa letu imebadilika, tukiendelea hivi, tunakokwenda ni kuzuri, hatuna sababu ya kukatishwa tamaa na watu wachache ambao wao kazi yao ni kuangalia mabaya tu katika jambo.

Nina matumaini makubwa mno moyoni mwangu na taifa hili leo kuliko ilivyokuwa mwaka jana, si kwamba hakuna mema yaliyotendeka, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, rais atakayekumbukwa kwa ucheshi na upole wake alifanya kadiri ya uwezo wake akaangushwa na wachache waliomzunguka. Nchi yetu inabadilika, Watanzania tuvumilieni katika kipindi hiki kigumu cha mpito, neema inakuja.

Lakini neema hii haitakuja kwa sisi kukaa chini tu kusubiri Rais Magufuli atuletee mabadiliko, tutasubiri sana na mabadiliko hayataonekana. Tunachotakiwa kufanya wakati rais wetu anapambana usiku na mchana pamoja na serikali yake ikiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ni kuwaunga mkono kwa kunyanyuka na kufanya kazi, Watanzania tuache uvivu, jina ambalo kwa muda mrefu tumeitwa na majirani zetu, tunyanyuke na kuchapa kazi, hapo ndipo tutayaona maisha bora yakija kwetu.

Nasema hivi kwa sababu wakati wa kampeni neno mabadiliko lilitamkwa sana, wanasiasa wakawa wakisikika majukwaani wakitamka maneno kama “nimekuja kuleta mabadiliko” wote Magufuli na Lowassa walilitumia sana neno hilo, baadhi ya watu wakaaminishwa kuwa mabadiliko wataletewa na hawatayaleta wenyewe.

Huo ni uwongo, hata katika taifa kama Marekani wako watu maskini kuliko ombaomba unaowaona mitaani kwetu ingawa Marekani ndiyo taifa tajiri duniani, hao hawakuamua kuyaleta mabadiliko maishani mwao, wanasubiri Obama awaletee ndiyo maana wanaendelea kuwa maskini, tukatae kuwa mfano wa watu wa aina hiyo, bali tunyanyuke na kufanya kazi hata kama ni kazi ndogo kiasi gani, tutakuwa tunabadilisha maisha yetu wenyewe na tunalipeleka mbele taifa letu.

Rais ameonesha njia, sote tumfuate, inawezekana kabisa kubadilisha taifa hili kuwa taifa la uchumi wa kati miaka michache tu ijayo kama sote tutatimiza wajibu wetu. Tumezaliwa katika taifa tajiri mno, lenye kila aina ya rasilimali, kamwe hatutakiwi kuendelea kubaki maskini labda kwa wale waliochagua aina hiyo ya maisha.

Chaguo langu mimi katika maisha ni kazi, siamini kabisa katika mafanikio ya kubahatisha, yaani unanunua tiketi ya bahati nasibu eti unajishindia milioni mia tano na maisha yako yanabadilika! Siamini katika hilo, pengine ndiyo sababu sijawahi hata kujishindia soda ya bure kwenye mashindano ambayo hufanywa na kampuni za vinywaji baridi, ninachokifahamu katika maisha ni kufanya kazi, hiyo ndiyo imekuwa dini yangu.

Nitamuunga mkono rais wangu kwa kufanya kazi kwa nguvu, namshukuru Mungu katika kampuni yetu amenipa kundi la vijana wachapakazi ambao hushirikiana nami katika kuisogeza kampuni mbele, napenda sana kufanya kazi na watu wa kujisukuma wenyewe, sipendi kabisa kufanya kazi na watu wavivu ambao ni lazima uwaambie cha kufanya ndipo watekeleze majukumu yao, hii hunisababishia “stress”!

Siku hizi tunafanya kazi zaidi kwa sababu hali ya mambo imebadilika, changamoto ya namna ya kuwasilisha habari kwa wananchi imekuwa tofauti na zamani, mitandao ya kijamii imechukua sehemu ya wasomaji, huu ni ukweli na jambo hili lilitulazimisha kufikiria zaidi ya ilivyokuwa zamani, akili inatumika mno na “stress” zinaongezeka.

Mara kadhaa najisikia mgonjwa na kuamua kwenda hospitali kufanya vipimo, ambacho daktari huniambia ni kwamba “Eric huumwi chochote, umechoka tu na unahitaji kupumzika!” Nimeambiwa maneno haya hata na baadhi ya wafanyakazi ofisini ambao hunishauri nichukue muda wa kupumzika, natamani kufanya hivyo, lakini kila ninapoangalia malengo ya kampuni, nakosa muda.

Ninapoiangalia kesho ya vyombo vya habari, sioni habari zikiwa kwenye karatasi! Karatasi zinaondoka taratibu kwenye soko na nafasi yake inachukuliwa na mtandao wa intaneti, hapa nina maana miaka michache ijayo, watu watakuwa wanasoma habari zaidi mtandaoni kuliko kununua gazeti kwa muuza gazeti barabarani kwenye foleni.

Hii imenifanya nifikirie sana, uamuzi wangu wa mara moja umekuwa ni kuchukua hatua ya ku-digitalize au kuanza kufanya mambo kidijitali katika usambazaji wa habari, fikra zangu na wenzangu zimetufikisha kwenye uamuzi wa kuanzisha kampuni iitwayo Global Digital Ltd, ambayo itakuwa ikijishughulisha na usambazaji wa habari pamoja na kufanya biashara mtandaoni, kwetu sisi tunaona maisha ya baadaye ni dijitali, si karatasi.

Njia ya haraka ya kufika kwenye mafanikio ya kifedha ni ya kutumia dijitali au teknolojia, hiki ndicho nilichojifunza kwa vijana waanzilishi wa Tweter, Facebook, WhatsApp na Google! Utaratibu wetu wa kufanya biashara kiasili, yaani kwenda kununua kitu na kuuza, utatuchelewesha kufika kileleni kwa haraka! Fikra zangu zimenituma kutafuta fedha mtandaoni, hili nataka kulifanya kwa moyo wangu wote, nimelisema wazi ili muwe mashahidi.

Fikra hizi nyingi kwangu mimi mara kadhaa zimenikosesha usingizi usiku na kwa sababu mimi ni miongoni mwa watu wachache duniani ambao wanapokuwa na mawazo mengi vichwani mwao, njia pekee ya kuyapunguza ni kula chakula, nimekuwa nikila chakula kingi kuliko zamani wakati huohuo kupunguza mazoezi jambo ambalo limenifanya niongeze uzito mkubwa, kilo zangu zilifika 105!

Hii ni hatari kwa afya yangu, daktari mara ya mwisho aliniambia “Eric ni lazima upunguze uzito, familia yako ina tatizo la shinikizo la damu, lisije likakupata!” Maneno haya yalikuwa mazito, sikutaka kuyachukulia kwa wepesi! Niseme wazi, hakuna kitu kigumu kama kupunguza uzito, kuongeza ni rahisi sana, ni uamuzi wa kula wanga mwingi na kupunguza mazoezi, lakini kuuondoa ni mateso.

Nimedhamiria kupunguza uzito, hilo ndilo lengo langu, maana nisipofanya hivyo itafikia wakati juhudi zote ninazozitumia kutafuta fedha hazitakuwa na maana kwa sababu nitaitumia fedha hiyohiyo kujitibu au sitaifaidi! Maana daktari ataniambia “Usile mafuta, sukari wala chumvi!”

Maisha hayatakuwa na raha tena, nitakuwa nimetafuta fedha ambazo mwisho wa siku zitashindwa kunipa furaha! Huu si uwongo, furaha iko wapi kama una kila kitu lakini unakula chakula kisicho na ladha? Sasa kwa nini nisifanye mazoezi nijiepusha na magonjwa yanayosababishwa na uzito kuongezeka, nimedhamiria na lengo hili nitalitimiza ingawa ni kazi ngumu.

Ziko tabia zilizonifanya niongezeka uzito, nitaziacha, baada ya hapo ni mazoezi mtindo mmoja! Kutekeleza lengo langu la kupunguza uzito nilifikia uamuzi wa kununua baiskeli ya mazoezi, kila siku ya Jumapili huendesha kilomita 50 mpaka 60 nikitoka jasho jingi, pia nimepunguza kabisa wanga kwenye chakula changu, katikati ya wiki nafanya mazoezi ya kawaida nyumbani, kwa hili la uzito sihitaji kuombewa na mchungaji wangu, nitalishughulikia mwenyewe.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave A Reply