The House of Favourite Newspapers

Twitter Washambuliwa na Wafuasi, Wasusa Kuitumia

WATU mashuhuri walio na wafuasi wengi sana kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter wamepoteza mamilioni ya wafuasi baada ya kampuni hiyo kuanza kuondoa ‘watu bandia’.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama ni miongoni mwa walioathirika, ambapo amepoteza watu 2.1 milioni.

Obama, ambaye babake alitokea Kenya, atazuru tena taifa hilo la Afrika Mashariki Jumatatu 16 Julai. Hiyo ni ziara yake ya kwanza nchini humo tangu andoke madarakani.

Mwanamuziki nyota kutoka Marekani, Katy Perry, ambaye ndiye mtu anayefuatwa zaidi kwenye Twitter, na Lady Gaga wamepoteza takriban wafuasi 2.5 milioni kila mmoja.

Twitter imesema imechukua hatua hiyo kutokana na juhudi zake ambazo zimekuwa zikiendelea za kujenga imani miongoni mwa wanaotumia mtandao huo.


Hii imetokea huku mitandao ya kijamii ikiendelea kuangaziwa kutokana na kuenea kwa taarifa za uzushi na watumizi feki wa mitandao ya kijamii.

Hatua mpya zilizochukuliwa na Twitter zinaathiri akaunti za Twitter ambazo zimefungwa kutokana na kutokea kwa shughuli zisizo za kawaida kwenye akaunti hizo.

Mfano wa shughuli hizi ni kufungiwa na watu, au kutuma ujumbe kwa mwingi wakati mmoja mtandaoni. Aidha, kuna akaunti za watu ambao hawakujibu walipotumiwa ujumbe wa kuthibitisha utambulisho wao.

Akaunti hizi zote zinaondolewa kutoka kwenye hesabu ya watu wanaofuata akaunti mbalimbali.

Hili limeathiri watu kote duniani. Nchini Kenya, baadhi wamekuwa wakieleza idadi ya wafuasi waliowapoteza, ingawa kwa wengine idadi inashangaza.


Idadi ya wafuasi wakati mwingine hutumiwa na watu, na zaidi watu mashuhuri mitandaoni, kuonyesha umaarufu wao.

Mkuu wa idara ya sheria katika kampuni hiyo Vijaya Gadde amesema akaunti nyingi zitapoteza kwa wastani wafuasi wanne.
Lakini ametahadharisha kwamba akaunti zinazofuatwa na watu wengi huenda zikashuhudia kupungua kwa wafuasi wka idadi kubwa.

Twitter wenyewe kwenye akaunti yao wamewapoteza wafuasi 7.7 milioni.
Twitter wamesema hatua ya sasa inalenga kujenga imani ya wanaotumia mtandao huo na inaongozwa na hali kwamba idadi ya watu wanaofuata akaunti fulani huonekana wazi.

Januari, mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la New York alisema jimbo hilo lilikuwa limeanzisha uchunguzi kuhusu kampuni ambayo inadaiwa kuuza mamilioni ya wafuasi bandia kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii.

Comments are closed.