The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi wa rais, wabunge Nigeria waahirishwa

 

UCHAGUZI mkuu wa urais na wabunge nchini Nigeria umeahirishwa ambapo utafanyika baada ya wiki moja. Tume huru ya kitaifa ya uchaguzi (INEC) ilitangaza hatua hiyo saa tano  kabla ya wapiga kura kuelekea katika vituo vya upigaji kura leo Jumamosi.

 

“Haiwezekani kuendelea na zoezi la uchaguzi kama ilivyopangwa,” mwenyekiti wa tume hiyo, Mahmood Yakubu, amesema, akitaja hitilafu za kimipango.

 

Amesema uamuzi huo mgumu umehitajika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki. Uchaguzi wa urais na ubunge umepangwa kufanyika Jumamosi ijayo Februari 23.

 

Uchaguzi wa magavana, wawakilishi wa majimbo na mabaraza ya manispaa umepangwa kufanyika Jumamosi Machi 9 mwaka huu.  Uamuzi huo umetolewa baada ya mkutano wa dharura katika makao makuu ya tume hiyo ya uchaguzi katika mji mkuu Abuja.

 

Yakubu amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya ‘ukaguzi wa makini’ wa ‘mpango wa namna uchaguzi utakavyofanyika’, akiongeza kwamba kuna ‘jitihada kubwa za kuhakikisha kuna uchaguzi  huru, wa haki na wa kuaminika’.

 

Amesema ni muhimu kuchelewesha uchaguzi huo kuipa tume nafasi ya kukabiliana na masuala muhimu na pia “kusalia na hadhi katika uchaguzi”, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

 

Katika wiki mbili zilizopita ofisi kadhaa za tume hiyo ya uchaguzi ziliteketezwa moto, huku maelfu ya vifaa vya kunakili kadi , na kadi za upigaji kura zikiharibiwa.

 

Pia kumekuwa na taarifa ya uhaba wa vifaa vya upigaji kura katika baadhi ya majimbo 36 ya nchi hiyo. Nigeria imelazimika kushinikiza usalama wake kuelekea katika uchaguzi huu uliokumbwa na ghasia.

 

Siku ya Ijumaa, maofisa katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Nigeria wameripoti kugundua miili ya watu 66, ambapo 22 kati yao ni ya watoto, na 12 ya wanawake waliouawa na ‘wahalifu’.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.