The House of Favourite Newspapers

Ujenzi wa Hospitali Ya Wilaya Arusha Wazinduliwa

Mhandisi wa Majengo Jiji la Arusha akitoa maelezo ya mradi huo kwa mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (kulia) na mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe Fabian Daqqaro ( katikati).

Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amezindua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha mjini katika eneo la Njiro Kontena.

Akizungumza na wananchi ambao wamehudhuria shughuli ya uzinduzi wa hospitali hiyo, Gambo amesema kwamba anafuraha kushuhudia tukio hili kwani ni moja kati ya ahadi za Rais Magufuli.

 

“Nina furaha sana kushuhudia tukio hili litakaloacha alama katika maisha ya watu wetu wa Arusha, kwani wakati wa kampeni Mhe Rais Magufuli aliahidi na tunatekeleza kwa vitendo,” Gambo.

 

Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya laki nne kutoka wilayani humo na maeneo ya jirani ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanasababisha hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kuelemewa.

Aidha Gambo ameongeza kwa kusema kuwa kwa sasa mapato yanayokusanywa na Jiji la Arusha kwa mwaka bado hayatoshelezi hata kulipa mishahara ya watumishi wake na kwa maana hiyo ni muhimu kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji wa mapato jijini humo.

 

“Jiji la Arusha mapato yake ya ndani kwa mwaka hayazidi bilioni 12 na mishahara pekee ya watumishi wa halmashauri ni zaidi ya bilioni 40, sasa hapo ukilipa tu mishahara hela yote inakwisha na bado unakua na deni, sasa hata fedha za maendeleo zitatoka wapi zaidi ya kutegemea hela zinazoletwa na Magufuli?? Gambo alihoji.

 

Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Arusha kwa awamu ya kwanza unafanyika katika moja ya maeneo ya wazi yaliyo kuwa yakimilikiwa kinyemelela na baadhi ya wajanja wachache na kwa sasa ujenzi umeanza ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 500 hii ikiwa ni jengo la Ghorofa moja kwa ajili ya wagonjwa wa nje.

Comments are closed.