The House of Favourite Newspapers

Ulimbukeni wa Magari Unaaibisha Mastaa Bongo

KWA mastaa wengi, kumiliki magari ya kifahari imekuwa ni ndoto yao kubwa. Wapo ambao watajinyima katika vyote lakini wafanye kila wanaloweza kununua magari. Hili lipo kwa mastaa wengi duniani na hata hapa Bongo.

 

Najua sababu ya kutaka kumiliki magari ni ili yawasaidie kwenye mishemishe zao za kisanii, maana ukiwa staa halafu ukawa unapanda daladala au kila siku ni mtu wa kupanda bodaboda au Bajaji, hainogi sana.

 

Yaani kunoga kwa ustaa ni kumiliki mkoko wako wa maana ambao utakurahisishia kwenda viwanja, kwenye madili ya pesa na hata mizunguko ya kawaida. Ndiyo maana kwa hapa Bongo, ni mastaa wachache ambao hawana magari licha ya kwamba wengine ni ya kuazima na wengine wanakodi.

 

Lakini sasa, kwenye hili la kumiliki gari linapokuja suala la maisha yetu ya kawaida, kuna kaulimbukeni flani ambako kapo na nadhani kanawafanya baadhi ya watu waonekane hawako live na maisha yao.

 

Kaulimbukeni hako ni kale ka’ kutaka kumiliki gari kisa staa mwenzako analo.

Wakati fulani uliwahi kuibuka mjadala mzito sana kwenye kundi moja la WhatsApp ambapo mmoja aliuliza kwamba; kati ya gari na nyumba, kipi ambacho staa anatakiwa kumiliki kwanza.

 

Ulikuwa mjadala mzito sana kwani waliokuwa wakisema nyumba kwanza, walijaribu kutoa sababu za wao kusema hivyo na wale waliosema gari kwanza, nao hawakukubali kushindwa! Nao walitaka kila mmoja aamini gari kwanza, mengine baadaye!

Kwa watu wanaojali maisha, najua watasimamia kwamba nyumba kwanza kwani litakuwa ni jambo la ajabu kama utakuwa unamiliki gari la kifahari halafu pa kulipaki huna.

 

Lakini wakati mwingine tufahamu kwamba kwenye maisha kuna kitu Wazungu wanasema ‘first choice’, yaani chaguo la kwanza! Kwamba leo hii ukiweka gari na nyumba kisha ukawaita mastaa wawili na kuwataka wachague, yupo ambaye atachukua gari na kuna ambaye ataona nyumba kwanza.

 

Katika mazingira hayo, huwezi kumuona yule aliyechagua gari kwanza ni limbukeni na hajui mambo ya msingi katika maisha. Huenda wewe ukadhani kumiliki nyumba kunakupa heshima kubwa kwenye jamii licha ya kwamba utakuwa unapanda daladala lakini elewa wapo wanaoona bora waishi kwenye nyumba za kupanga lakini wakikatiza mitaani waendeshe magari ya kifahari.

 

Hapo ndipo linapokuja suala la ‘choice’, kwamba wapo wanaoona kumiliki nyumba kwenye maisha yao wala siyo ishu, badala yake wanaona kuwa na gari la kifahari ndiyo furaha ya maisha yao.

 

Lakini wakati wakiwepo watu wa aina hiyo, wewe kama staa hukatazwi kuanza kumiliki nyumba. Kama unaona ukiwa na mjengo wako wa maana, moyo wako unakuwa na amani na furaha, anza kumiliki rasilimali hiyo. Kikubwa ni kuongea na moyo wako.

 

Katika hili wala hutakiwi kufuata mkumbo wa mastaa wengine.

Kwa mfano kama staa mwenzako anaishi kwenye nyumba ya kupanga lakini anamiliki gari, hutakiwi kukopi alichokifanya. Jadiliana na moyo wako kwamba uanze kipi, ukikuambia anza na gari huku ukikupa sababu, uusikilize!

 

Ndiyo maana kuna mtu leo hii ukimuomba ushauri nini uanze kumiliki kati ya gari na nyumba atakuambia gari kwanza na atakupa sababu za msingi sana mpaka utaona ni kweli bora uanze kununua gari.

 

Lakini mwingine atakuambia angaikia nyumba kwanza. Ukimuuliza kwa nini isiwe gari kwanza, atakupa sababu. Kwa mfano, ni mastaa wangapi ambao kila siku wanakumbwa na aibu ya kufukuzwa kwenye nyumba za kupanga kwa kukosa kodi lakini wana magari ya kifahari?

 

Sasa kutakuwa na faida gani ya kumiliki gari wakati unaaibika kwa kukosa pesa ya pango? Lakini ni staa gani alishaaibika kwa kukosa gari na akaamua kupanda Bajaji au bodaboda? Kwa kifupi ni kwamba aibu ya staa kutimuliwa kwenye nyumba ya kupanga kwa kukosa kodi ni kubwa kuliko aibu ya kupanda daladala.

 

Ndiyo maana mastaa wanashauriwa kwanza kujihakikishia sehemu za uhakika za kuishi, nikimaanisha kumiliki nyumba zao kuliko kuwa na magari ya kifahari kisha wanatangatanga kwa kubadili nyumba za kupanga kila siku.

 

Kama wanavyosema huko mtaani, hakuna baba mwenye gari bali kuna baba mwenye nyumba. Msemo huu unawagusa watu wote wakiwemo mastaa.

 

Hata hivyo niwapongeze mastaa ambao wamefanikiwa kuwa na nyumba zao na magari, pia niwape big up ambao wameshajenga nyumba na sasa wanapambania magari, ila niwazodoe wale ambao pesa wanapata lakini mpaka leo wamepanga nyumba, bajaji, bodaboda na daladala vinawahusu. Hawa ni aibu yao!

Comments are closed.