The House of Favourite Newspapers

Ulinzi Madawa ya Kulevya Usipime

“OOOH! Haya madawa ya kulevya wanayokamatwa nayo watu, kesi zao zikimalizika ndipo wajanja serikalini wanayauza na kujipatia fedha.” Nani anakuambia uongo wa aina hii? Kuanzia leo ufahamu kuwa, madawa hayo ulinzi wake si wa kitoto.

 

Jumanne iliyopita mwandishi wetu alishuhudia maafisa wa tume ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, idara ya mahakama, takukuru na usalama wa taifa wakishiriki katika zoezi la kuteketeza madawa hayo yenye thamani ya mabilioni ya fedha.

 

Habari zilizotolewa na Kaimu Kamishna; Jenerali James Wilbert Kaji kutoka tume ya madawa ya kulevya, zilieleza kuwa madawa yaliyokuwa yakiteketezwa ni yale ambayo kesi zake zimemalizika mahakamani na watuhumiwa kutiwa hatiani.

 

Jenerali Kaji alizitaja dawa hizo kuwa ni heroini na kokeini ambazo jumla yake ni kilo 120.91 ambazo zote zilikamatwa kwa nyakati tofauti na kwamba siku hiyo katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga kilichopo Wazo Hill, Dar ziliteketezwa kwa kuchomwa moto.

 

Zoezi hilo halikuwa jepesi bali lilifuata misingi madhubuti ya sheria na ulinzi ambapo jaji alihusika kusoma kesi ya kila mtuhumiwa na kiwango cha madawa aliyokamatwa nayo kisha vyombo vya usalama vikihakiki vifurushi hivyo na kuruhusu kutupwa kwenye tanuri la moto.

 

Kama hilo halitoshi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Biswalo Mganga naye alikuwepo kushuhudia zoezi hilo.

Aidha, maafisa kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali nao walifika eneo la tukio ili kuthibitisha kuwa kilichomo kwenye vifurushi husika ni madawa ya kulevya na si vinginevyo.

 

Maafisa wengine waliokuwepo kutimiza wajibu wao ni kutoka katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambao walikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa uteketezaji wa madawa hayo unazingatia uhifadhi mazingira na hauleti madhara kwa binadamu.

 

Kuhusu vyombo vya usalama, mahali hapo palikuwa hapatoshi kwani mbali na askari kanzu kutapakaa eneo zima, askari wengine wakakamavu wenye silaha nzito walikuwepo kuhakikisha kuwa hakuna uhalifu wowote unaoweza kujitokeza katika zoezi hilo.

 

Mwisho, Jenerali Kaji aliwaonya wale wote wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya kuachana nayo kwani katika awamu hii ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, hakuna mfanyabiashara wa madawa hayo atakayebaki salama bila kufikiwa na vyombo vya dola.

STORI: Richard Bukos, Risasi Jumamosi

Comments are closed.