The House of Favourite Newspapers

Unafiki, Uroho wa Madaraka Unaipeleka TFF Shimoni

Rais wa TFF Wallace Karia.

TAKRIBANI wiki mbili sasa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hakuna jambo la maendeleo ambalo linazungumziwa badala yake mizengwe na kuchafuana.

Gumzo la nani hafai na nani anafaa ndiyo limechukua sura kubwa ya maisha mapya ya TFF ambayo ninaamini wako waliokuwa na matumaini makubwa kuhusiana na suala la maendeleo.

Kuna mambo mengi sana hayana majibu na huenda yametumika kuwabadilisha wengi walioamini chini ya Urais wa Wallace Karia, basi mambo yatakwenda vizuri kabisa.

Aliyekuwa Makamu Rais wa TFF, Michael Wambura.

Kwa sasa gumzo ni aliyekuwa Makamu Rais wa TFF, Michael Wambura ambaye amefungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka akipatikana na tuhuma kadhaa ikiwa ni pamoja na kupokea malipo ambayo yanaonekana hayakuwa sahihi, pia kushusha hadhi ya shirikisho.

 

Wambura amekuwa akipinga hilo na ametumia nguvu kubwa huku akieleza mambo mengi yakiwemo mengine ambayo yanaonekana si ya msingi kwa kuwa anayesema baada ya kuona ameondolewa wakati akiwa ndani ya TFF hakuwahi kusema jambo, kwamba mambo yanaharibika.

 

Sasa anasema kwa kuwa ametolewa na huenda kwa kuwa anaamini ameonewa na vinginevyo. Ndiyo maana kwangu naona kama anazungumza maneno ambayo alipaswa kuyasema mapema kama alipingana nayo, kwa kuwa alikaa kimya, kila kibaya anachokisema sasa, basi naye alishiriki akiwa kiongozi kwa kuwa kama aliyeharibu ni Karia, msaidizi wake ni yeye!

 

 

Msimamo wangu umekuwa hivi, kama Wambura ana hatia, achukuliwe hatua na iwe funzo kwa wengine kwa kuwa tumechoshwa na mambo yasiyoisha yanayokosa weledi ndani ya mpira.

 

Lakini kama hana hatia, basi apewe nafasi ya kuendelea na kazi yake. Naweka msisitizo, kuondoka kwake isiwe ni fitna naye asijenge njia ya kutaka kuwaonyesha watu kwamba baada ya yeye kuondolewa TFF kuna shida sana au ilikuwepo kubwa sana.

 

Maana hoja ya msingi, atueleze au agombee kurejea katika nafasi yake kwa kupita katika njia sahihi badala ya maneno mengi.

 

Lakini kama utatulia katika hiki kinachoendelea, inaonyesha wazi sasa ndani ya TFF ni vita ya madaraka, jambo ambalo limeturudisha nyuma kwa muda mrefu sana.

 

Huenda usingekuwa wakati mwafaka kusikia suala la vita ya madaraka kwa kipindi  hiki kwa kuwa TFF imefanikiwa kuwaleta viongozi wakuu wa soka duniani, ukianza na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa Caf, Ahmad Ahmad. Hii ni mara ya kwanza kabisa.

 

Heshima kubwa iliyopata Tanzania ilipaswa kuwa mfano na muendelezo sahihi. Lakini sasa gumzo ni vita ya madaraka na kusikia mambo mengi nje ya mpira kama yale mazengwe ya fulani si raia mara fulani si raia.

Inaonyesha wazi ndani ya TFF kuna chuki kubwa na makundi ambayo yakiendelea kuwa na nguvu zake, maana yake ndoto ya kuendeleza mpira wetu itabaki kuwa ya mchana na isiyo na hatua.

 

Tumechoka waungwana, tunataka maendeleo na dhamana mliyopewa ni kuendeleza mpira na si kushambuliana. Aliye mchafu aondoke, aliye na haki abaki na kusiwe na uonevu.

 

Hadi leo Fifa inashikilia zaidi ya Sh bilioni 3 za Tanzania katika suala la maendeleo ya mpira. Hii yote ilitokana na uongozi duni. Sasa tunaingia kwenye migogoro mingine ambayo kama kukifuatwa utaratibu sahihi hakuwezi kuwa na kinachoendelea.

 

TFF isimame imara ituonyeshe kama haijakosea, na kama kinachofanyika ni sahihi, kimefuata katiba basi nguvu irudishwe katika maendeleo kwa kuwa tunataka kusikia hatua zikipigwa kuujenga mpira wetu ambao kukua imekuwa ni hadithi.

 

Hi hivi, Wambura ajibu hoja za msingi atueleze zile tuhuma alizopatikana nazo na hatia ni sahihi au la na kwa nini.

Hali ilivyo, inaonyesha kila mmoja wenu anachoangalia ni madaraka anayoyataka na inaonekana ni kwa faida zenu na si kwa faida ya mpira wetu.

 

Vizuri hili linalozunguka, lifikie liishe katika njia sahihi. Halafu baada ya hapo tuanze kusikia mipango ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.

TFF wakati ikiendelea na hili la Wambura, niwakumbushe tunachotaka ni maendeleo ya mpira na si kila kitu kionekane kimesimama kwa kuwa Wambura kasimamishwa.

Kwa Wambura, kikubwa apate haki yake, iwe kufungiwa kama ana hatia au kurudishwa kama hana hatia. Lakini naye asijaribu kuvuruga mambo kwa kuwa yeye hayupo.

Tunataka mpira uendelee, tunataka maendeleo ya mpira na si maneno yasiyo na mwisho. Tumechoshwa na haya na tumeyasikia kwa miaka mingi huku mpira ukiendelea kudorora.

Stori na Saleh Ally | Championi Jumatano

Comments are closed.