The House of Favourite Newspapers

Unataka kuishi kwa amani na furaha? Haya yanakuhusu!

0

Kuna watu huko mtaani hawajui mtaji wa kuishi maisha ya furaha. Wapo wanaodhani ukishakuwa na fedha basi maisha umeyapatia.

Tambua kwamba, wapo watu wana pesa nyingi, wameoa wake wazuri, wana uwezo wa kufanya kila wanalotaka lakini bado maisha yao hayana amani, kwa nini? Kwa sababu hawajui nguzo za kujijengea maisha ya furaha na amani.

Wiki hii nimeona nikupe mambo 10 ambayo kama utayatimiza, utaishi maisha mazuri hapa duniani na pia maisha mazuri baada ya kifo (kwa wale tunaoamini kwamba kuna maisha baada ya kifo).

•Mwenza sahihi
Huwezi kuwa na maisha ya furaha kama uko na mwenza asiyekujali, asiyekuonesha mapenzi ya dhati. Tukumbuke wapo watu ambao wana kila kitu lakini mapenzi yamekuwa yakiwakosesha amani.

Ndiyo maana inashauriwa kuchagua mwenza sahihi ambaye atakuwa ni mmoja wa watu wa kukufanya uwe na furaha.

•Usipende kukopa
Hakuna jambo linalowakosesha baadhi ya watu amani kama madeni. Wapo waliofikia hatua ya kujiua kwa sababu ya kudaiwa. Licha ya kwamba kila mmoja kuna wakati anakopa, hutakiwi kuiendekeza tabia hii.

•Mazingira mazuri kazini
Maisha ya sasa bila kufanya kazi huwezi kuwa na maisha mazuri kwani ndiyo inayoweza kukupatia kipato cha kuyaendesha maisha yako.

Hata hivyo, ili kuifanya kazi yako ikupe amani, ni lazima mazingira yawe mazuri. Uwe unalipwa vizuri, mabosi wakuthamini na upendwe na wafanyakazi wenzako.

•Jihakikishie mahitaji muhimu
Binadamu yoyote lazima apate mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi, sehemu nzuri ya kulala na matibabu akiumwa. Endapo utajihakikishia yote hayo katika kiwango kinachostahili, maisha yako yatakuwa ya furaha.

•Jiwekee akiba
Inashauriwa kwamba, unapopata fedha usitumbue zote, weka akiba pale inapotokea umepata pesa ya ziada. Hiyo itakufanya uwe na amani ukiamini kwamba, uko tayari kukabiliana na tatizo lolote mbele yako litakalohitaji fedha.

•Upendo wa ndugu, majirani, wafanyakazi, marafiki
Unatakiwa kutumia gharama yoyote kujihakikisha upendo kutoka kwa ndugu zako, majirani, marafiki na watu ambao unakutana nao katika mihangaiko yako.
Ukikosea kidogo, ukachukiwa na kila mtu ni lazima maisha utayaona machungu.

•Utatuzi wa matatizo kwa wakati
Njia sahihi ya kukabiliana na matatizo ili yasitutibulie maisha yetu na kutukosesha amani, ni kuyatatua haraka.

Unapokumbwa na tatizo dogo leo, ukaliacha hadi kesho na likatokea lingine, utakuwa umejikusanyia tatizo kubwa linaloweza kukusumbua.

•Zaa watoto unaowamudu
Kweli watoto ni furaha ya ndoa lakini jitahidi sana kuzaa watoto utakaowamudu. Kuzaa watoto wengi inaweza kuwa ni kujiongezea majukumu ambayo yanaweza kukuvuruga. Zaa watoto wachache utakaomudu kuwapa mahitaji yao muhimu.

•Jijenge kiimani
Mtangulize Mungu wako katika kila siku ya maisha yako. Muabudu kwa nguvu zote, hakikisha unatenda yale yanayomfurahisha na kuepuka yanayomchukiza.
Hii itamfanya Mungu akumulikie taa kwenye maisha yako huku ukibaki na imani pia kwamba maisha yako hata baada ya kifo yatakuwa mazuri.

•Ridhika na maisha uliyonayo
Kutokana na tulivyojaaliwa na Mungu, ili kuwa na amani ni vyema ukaridhika na maisha yako. Ridhika na wala usiwe na tamaa ya mambo makubwa ambayo ni vigumu kuyafikia. Waache wengine wale nyama, wewe ona furaha kula dagaa kwani ndivyo Mungu alivyokupangia.

Leave A Reply